Wanapita mulemule
Muktasari:
Miongoni mwao kama Kasper Schmeichel au Daley Blind, wote hao wamefanya vizuri kufuata nyayo za baba zao na kupata mafanikio makubwa kwenye soka wakicheza klabu zinazojielewa kwenye Ligi Kuu England, mmoja akiwa Leicester City na mwingine Manchester United.
LONDON, ENGLAND
MAHALI kote duniani watoto wengi wanapokua wamekuwa na ndoto za kufuata nyayo za baba zao kwa kile walichokuwa wakikifanya na jambo hilo halina tofauti kabisa linapokuja katika mpira wa miguu.
Miongoni mwao kama Kasper Schmeichel au Daley Blind, wote hao wamefanya vizuri kufuata nyayo za baba zao na kupata mafanikio makubwa kwenye soka wakicheza klabu zinazojielewa kwenye Ligi Kuu England, mmoja akiwa Leicester City na mwingine Manchester United.
Kuna watoto wengine wa wachezaji waliotamba kwenye ligi hiyo, kama vile Tom Ince, mtoto wa Paul Ince. Lakini, kama inavyofahamika duniani kote mtoto wa nyoka ni nyota.
Cheki watoto wa mastaa wa soka wanavyokimbiza katika mchezo huo kwa sasa.
Justin Kluivert - mtoto wa Patrick Kluivert
Timu: Ajax
Mmojawapo kati ya vijana matata kabisa kwenye kikosi cha Ajax. Justin Kluivert ameonyesha dalili zote za kufuata nyayo za baba yake kwa kuwa mshambuliaji hatari licha ya umri wake kuwa na miaka 18 tu kwa sasa.
Akianza kuichezea Ajax mwaka msimu uliopita tu, Justin amecheza mechi 50 kwenye kikosi hicho na kufunga mabao 10. Siku za karibuni alihusishwa na Manchester United, lakini baba yake amemtaka akajiunge na Barcelona. Enzi zake Kluivert aliichezea pia Ajax na Barcelona, huku akiifanya Uholanzi kutisha kwenye soka la dunia. Alifunga mabao 199 katika maisha yake ya soka la klabu.
Isaac Drogba - mtoto wa Didier Drogba
Timu: Guingamp
Mtoto mwingine wa mwanasoka maarufu duniani, Didier Drogba, Isaac anayecheza soka lake Ulaya. Isaac anakipiga kwenye kikosi cha Guingamp, alikojiunga Februari baada ya kuondoka kwenye akademia ya Chelsea.
Akiunga pia kwenye akademia ya Guingamp, timu inayoshiriki soka la Ufaransa, Isaac anafuata nyayo za baba yake, ambaye aliwahi kuichezea timu hiyo kabla ya kujiunga na Marseille kisha Chelsea.
Drogba amebaki kuwa kwenye kumbukumbu za kudumu katika klabu ya Chelsea baada ya kile alichokifanya katika kikosi hicho alipoisaidia kubeba ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya. Drogba amebeba Ligi Kuu England mara nne na Kombe la FA mara nne.
Timothy Weah - mtoto wa George Weah
Timu: Paris Saint-Germain
Akikulia Marekani, Timothy Weah alihamia Ufaransa mwaka 2014 na kwenda kuichezea Paris Saint-Germain kabla ya kusajiliwa kwenye kikosi cha kwanza miaka mitatu baadaye.
Akicheza sehemu kubwa zaidi kwenye mechi za rizevu na timu za vijana, straika huyo mwenye umri wa miaka 18 alicheza mechi yake ya kwanza katika kikosi cha kwanza mwezi huu wakati alipoingia kutokea benchi kwenye mechi ya ushindi wa mabao 2-0 iliyopata PSG dhidi ya Troyes.
Ameitwa pia kwenye timu ya Taifa ya Marekani. Baba yake enzi zake alicheza PSG, AC Milan na timu nyingine kubwa huku mwaka 1995 alibeba tuzo ya Ballon d’Or.
Giovanni Simeone - mtoto wa Diego Simeone
Timu: Fiorentina
Panga pangua anaanzishwa kwenye kikosi cha Fiorentina msimu huu. Straika, Giovanni Simeone ameonyesha kipaji kikubwa kwamba atakwenda kuwa mshambuliaji mmoja mkubwa sana katika klabu za Ulaya.
Amefunga mabao saba kwenye Serie A msimu huu na tayari jina lake linahusishwa na mpango wa kwenda kujiunga na Atletico Madrid, timu inayonolewa na baba yake, Diego Simeone. Diego Simeona aliwahi kusema mchezaji ambaye atapenda sana kumnoa ni mwanaye, Giovanni.
Kuhusu baba mzazi, Diego alicheza Lazio na kubeba ubingwa wa Serie na Atletico ambako alibeba ubingwa wa La Liga. Kwenye timu hizo kote baadaye alienda kuwa kocha.
Ianis Hagi - mtoto wa Gheorghe Hagi
Timu: FC Viitorul
Akiungana kwenye kundi la wachezaji watoto wa wachezaji, Ianis Hagi kwa sasa anakipiga katika kikosi cha FC Viitorul ya huko Romania, ambayo inanolewa na baba yake, Gheorghe Hagi. Alinaswa kwenye uhamisho wa Januari mwaka huu, mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 19, Ianis alijiunga na timu ya baba yake baada ya kushindwa kufanya mambo ya maana huko Fiorentina inayoshiriki Ligi ya Serie A.
Alipotua tu Viitorul, amechaguliwa kuwa nahodha. Baba yake, Hagi alicheza Real Madrid na Barcelona na alibeba mataji mengi tu Galatasaray na Steaua Bucharest. Soka la kimataifa amecheza mechi 125 na kufunga mabao 35 akifungana na Adrian Mutu.
Niall Keown - mtoto wa Martin Keown
Timu: Partick Thistle
Kama ilivyokuwa kwa baba yake Martin, Niall Keown naye ni beki wa kati na jambo hilo linamfanya alinganishwe sana mtindo wa soka lake analocheza.
Niall anacheza kwenye Ligi Kuu Scotland akikitumikia kikosi cha Partick Thistle, lakini ni baada ya kudumu kwa miaka minne katika timu ya Reading. Kwenye soka la kimataifa, Niall anaichezea Jamhuri ya Ireland, lakini bado hajaanza kukichezea kikosi cha wakubwa. Kuhusu baba yake, Martin alikuwa kwenye kikosi kile matata cha Arsenal isiyofungwa na alibeba mataji matatu ya Ligi Kuu England na matano ya Kombe la FA. Kwenye soka la kimataifa aliichezea England mechi 43.