40 ya mtoto wa Wema Sepetu yageuka kitendawili
Sherehe ya siku 40 ya Ollie ambaye ni mtoto wa staa wa filamu, Wema Sepetu, iliyokuwa inasubiriwa kwa hamu kufanyika Julai 24, 2026 katika ukumbi wa The SuperDome, Masaki jijini Dar es Salaam, imeahirishwa ghafla na kuwaacha mashabiki wengi wakijiuliza kulikoni.
Hafla hiyo ilikuwa imepata umaarufu mkubwa kabla ya kufanyika, baada ya Wema na Whozu ambaye ni baba wa mtoto huyo kuitangaza kupitia kurasa zao za mitandao ya kijamii huku waandaaji wakianika viwango tofauti vya tiketi vilivyozua mjadala mkubwa.
Tofauti na matarajio ya wengi, siku ya tukio imewadia bila sherehe kufanyika, huku kukiwa hakuna tamko rasmi lililotolewa mapema kueleza sababu ya mabadiliko hayo.
Chanzo cha karibu na ndugu wa Wema, kimeiambia Mwanaspoti kuwa familia iliamua kuisogeza mbele hafla hiyo kwa kuzingatia afya na ustawi wa mtoto ambaye bado ni mdogo sana.
"Mtoto bado ni mdogo, ndiyo maana familia imeona ni bora hafla isogezwe mbele kwanza," kimesema chanzo hicho.
Mbali na maelezo hayo, Mwanaspoti pia imezipata taarifa nyingine kutoka kwa baadhi ya watu waliohusika katika maandalizi ya hafla hiyo zikidai kuwa michango ya kufanikisha sherehe ilikuwa bado haijakamilika kwa wakati. Hata hivyo, taarifa hizo hazijathibitishwa rasmi na Wema, Whozu wala waandaaji wa hafla hiyo.
Mwanaspoti imemtafuta Wema Sepetu kwa njia ya simu ili kupata ufafanuzi kuhusu taarifa hizo. Alipopokea alisema kwa kifupi kwa wakati huo alikuwa bize akimnyonyesha mtoto.
"Nipo bize namnyonyesha mtoto, nitakupigia tuongee," amesema Wema.
Hadi habari hii inaandikwa, Wema alikuwa bado hajarejea kutoa ufafanuzi kuhusu sababu halisi ya kuahirishwa kwa hafla hiyo wala kutangaza tarehe mpya ya kufanyika kwake.
Kilichozidi kuwachanganya mashabiki ni ukimya wa Wema na Whozu katika siku ambayo sherehe hiyo ilipaswa kufanyika. Wawili hao hawakuchapisha taarifa yoyote kupitia kurasa zao za Instagram kueleza kuwa hafla imeahirishwa, licha ya kuwa awali walikuwa wakitumia majukwaa hayo kuhamasisha mashabiki kushiriki siku ya 40 ya mtoto wao.
Ukimya huo umeibua maswali mengi mitandaoni, huku baadhi ya mashabiki wakihoji kilichojiri dakika za mwisho, na wengine wakisubiri tamko rasmi kutoka kwa wazazi hao.
Kabla ya kuahirishwa, hafla hiyo ilikuwa tayari imevuta hisia za wengi kutokana na viwango vya viingilio vilivyotangazwa. Tiketi zilikuwa zikiuzwa kuanzia Sh100,000, Sh300,000, Sh500,000, huku kifurushi cha juu zaidi kikiwa Sh5 milioni.