Wanamuziki Bongo waliotoka kupitia mashindano ya kuimba
Muktasari:
- Tangu miaka ya 1990 hadi sasa, ni jambo ambalo limekuwa likiendelea kufanya katika tasnia na kutuletea majina makubwa wakiwemo hawa wafuatao.
KUNA wanamuziki wengi wa Bongofleva ambao walianza kutambulika na mashabiki baada ya wao kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali ya kusaka vipaji vya muziki.
Tangu miaka ya 1990 hadi sasa, ni jambo ambalo limekuwa likiendelea kufanya katika tasnia na kutuletea majina makubwa wakiwemo hawa wafuatao.
1. Gangwe Mobb - Kundi hili linaloundwa na Inspector Haroun na Luteni Kalama, waliibuka washindi katika shindano la rap katika nviwanja vya Don Bosco, na ndipo DJ Boniluv akawapa nafasi ya kurekodi. Wimbo uliowatoa unaoitwa Ngangari (1999), ulitengenezwa na watayarishaji watatu, DJ Boniluv, Rajab Marijani na P-Funk Majani, ila wimbo wao wa kwanza kuachia ni 'Mauzauza' uliorekodiwa Mawingu Studio.
2. Lady Jaydee - Baada ya kuibuka mshindi wa shindano la DJ Show ya Radio One, alipewa fursa ya kurekodi MJ Records kabla ya kuja kutoka na wimbo wake, Machozi (2001) uliobeba jina la albamu yake ya kwanza. Nyimbo zilizompa ushindi Lady Jaydee ni Keep On wa Mc Lyte, Stranded wa Lutricia McNeal na Gotta Get You Home wa Foxy Brown.
3. Banana Zorro - Alishiriki mashindano ya Tanzania Pop Idol 2001 na kuibuka mshindi na kuwakilisha nchi katika mashindano ya Afrika huko Afrika Kusini. Ushindi huo ulipelekea Smooth Vibes chini ya Prime Time Promotion kumsaini Banana Zorro kabla ya kutoka kupitia wimbo wake, Yangu (2003) uliotayarishwa na Miikka Mwamba.
4. Wakilisha - Kundi hili liloundwa na Shaa, Witness na marehemu Langa, ndio waliibuka washindi wa Coca-Cola Popstar East Africa 2004 upande wa Tanzania, kisha akatoka na wimbo wao 'Hoi' chini ya MJ Records. Kwa upande wa Kenya washindi walikiwa ni kundi la Sema, na Uganda, Blu 3, kundi lilovuma na kibao chao, Where You Are (2009) wakiwashirikisha Radio & Weasel (Goodlyfe Crew).
5. Nikki Mbishi - Alishiriki shindano la Kilimanjaro Emcee Shujaa 2008 ambapo alishika nafasi ya pili nyuma ya Lusajo huku marehemu Godzilla akishika nafasi ya tatu. Baadaye Nikki akaja kusainiwa M Lab na kufanya vizuri kupitia ngoma yake, Play Boy (2011) iliyotayarishwa na Duke Tachez, na ulijumuishwa katika albamu yake ya kwanza, Sauti ya Jogoo.
6. Young Killer - Alikuwa amesharekodi nyimbo kadhaa kabla ya kuibuka mshindi wa Fiesta Super Nyota 2012. Baada ya hapo ndipo akavuma na wimbo wake 'Dear Gambe' ulitayarishwa na Mona Gangster. Ikumbukwe kufanya vizuri kwa wimbo huo kulipelekea Young Killer kushinda Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) kama Msanii Bora Chipukizi 2013.
7. Nandy - Baada ya kushika nafasi ya pili katika shindano la kwanza la karaoke Afrika, Tecno Own The Stage 2015, ndipo akaja kutoka na wimbo wake, Nagusagusa (2016) uliotayarishwa na Emma The Boy. Katika shindalo hilo ambalo fainali yake ilifanyika Lagos nchini Nigeria, Nandy alizawadia Dola15,000, pia alipewa nafasi ya kupata mafunzo chini ya lebo ya Chocolate City.
8. Phina - Alishiriki Bongo Star Search (BSS) 2018 na kuibuka mshindi, kisha akaja kuvuma zaidi kwa mara ya kwanza kupitia wimbo wake, Upo Nyongo (2022) ukitayarishwa na Aloneym.
Kwa sasa Phina ni mmoja wa wanamuziki wa kike wanaofanya vizuri katika Bongofleva akiwa tayari ameshinda tuzo nne za muziki Tanzania (TMA) ndani ya misimu miwili pekee.