TUONGEE KISHKAJI: Filamu za kichawi mbele zinaingiza mkwanja, bongo zinafundisha uchawi
Muktasari:
- Na kama hujawahi kutazama fiamu za Harry Pooter, fahamu kwanza zinahusu mtoto yatima anayeitwa Harry Potter ambaye anaalikwa kwenda kusoma kwenye chuo cha uchawi na kinachoitwa Hogwart.
FILAMU za Harry Potter zimeingiza mapato ya zaidi ya Dola za Marekani 7.7 bilioni. Hiyo ni sawa na zaidi ya Sh17 trilioni. Hapo hatujazungumza kuhusu vitabu cha Harry Potter ambavyo ndivyo vimezaa filamu hizo. Bado hatujaongelea t-shirt, vikombe na makorokoro yote yanayoendelea kuuzwa kupitia nembo ya Harry Potter.
Na kama hujawahi kutazama fiamu za Harry Pooter, fahamu kwanza zinahusu mtoto yatima anayeitwa Harry Potter ambaye anaalikwa kwenda kusoma kwenye chuo cha uchawi na kinachoitwa Hogwart.
Akiwa huko anavumbua historia kubwa kuhusu maisha yake na wazazi wake.
Filamu ya Insyuka ni moja ya filamu zilizotengeneza njia ya kila tunachokiona kwenye kiwanda cha filamu leo. Ni moja ya filamu bora kuwahi kutengenezwa Tanzania. Hata hivyo, kwa sababu Bongo hatuna mfumo mzuri wa kufuatilia mapato ya kazi za sanaa ni ngumu kuwa na data za pesa kiasi gani zilivunwa na filamu hiyo.
Lakini ni filamu ambayo karibu kila Mtanzania aliyekuwa akiishi mjini aliitazama kipindi inaingia sokoni.
Kama hujawahi kuitazama, Insyuka ni filamu inayohusu mwanamke mgumba ambaye baada ya kuona hapati mtoto kwenye ndoa yake anaamua kwenda kwa mganga wa kienyeji.
Akiwa huko analazimishwa kutembea na mzimu unaoitwa Insyuka na kubeba mimba. Lakini, baadaye anajifungua mtoto ambaye anakuwa na mambo ya ajabu. Wakati huo huo Insyuka ule mzimu, unataka mtoto wake.
Ni hadithi ambayo inamulika changamoto za shuruba za kihisia ambazo wanawake wagumba wanapatia kwenye ngazi za familia.
Binafsi nimeshatazama filamu zote hizo mbili za kichawi, Harry Potter na Insyuka. Na sio hizo tu pia nimetazama nyingine nyingi za kichawi kama vile Shumileta, Saladini, Mzee wa Busara, Roho Mbili, Jinamizi na kadhalika.
Lakini licha ya kwanba nimetazama filamu zote hizo za kichawi hadi leo sijui jinsi ya kufanya uchawi. Hivyo pengine kichwa changu ni kizito au namna gani.
Nasema hivi kwa sababu wakati wabunge wanachangia bajeti ya Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo mmoja wa wabunge alisimama na kudai filamu za kichawi zinafundisha watoto uchawi. Pengine ni kweli sisi ni nani tumpinge mbunge. Lakini tatizo ni kwamba wakati mbunge anachangia hoja yake hakuwa na data zozote zinazounga mkono hoja yake.
Mbunge hakusema watoto wangapi wamejifunza uchawi kupitia filamu. Hakusema watoto wangapi wametamani kuwa wachawi kupitia filamu. Mbunge hakutaja majina ya filamu za kichawi anazoziongelea wala hakutaja wasanii walioshiriki kwenye kuziandaa filamu hizo. Mbunge alichokifanya tunaweza kukiita kusimama na kuzungumza hisia zake.
Mtu kuzungumza hisia zake si jambo baya, lakini kwa sehemu kama bungeni inapendeza hisia zikiambatanishwa na data. Natamani badala ya wabunge kuwa wanarusha mashambulizi, wangekuwa wanatoa maoni kisayansi.
Tasia yenyewe ya filamu ndiyo kwanza inajaribu kujipambania kuwa rasmi. Tukiaanza kuishambulia bila data namna hii ni kuionea tu.