Linex: Miaka 30 ya Bongo Fleva ni somo kwa wasanii
Muktasari:
- Linex ambaye wimbo uliompa umaarufu zaidi ni wa Mama Halima aliouachia mwaka 2016, amesema kuna nyimbo za wasanii wa zamani ambazo zikipigwa hadi sasa zinaimbwa na rika zote.
MSANII wa Bongo Fleva, Linex Sunday Mjeda, amesema wasanii wa sasa bado wana mambo mengi ya kujifunza, ili baadaye watakapokuja wengine nyuma yao, wawe wanatajwa kama mfano wa kuigwa.
Linex ambaye wimbo uliompa umaarufu zaidi ni wa Mama Halima aliouachia mwaka 2016, amesema kuna nyimbo za wasanii wa zamani ambazo zikipigwa hadi sasa zinaimbwa na rika zote.
Katika kukazia hilo, Linex amesema tamasha la Miaka 30 ya Bongo Fleva limeendelea kuwa somo kwa wasanii wa kizazi cha sasa.
"Kilianza kizazi cha baba zetu ambao walikuwa wanarekodi laivu, tofauti na sasa ukiingia studio unaimba mstari wa kwanza unaacha na kuurudia tena, wao waliimba moja kwa moja, mfano mzuri wimbo wa Kitambaa Cheupe ukipigwa una vaibu, kila mtu anaimba," anasema na kuongeza;
"Mfano mwingine mzuri hao kaka zetu wa miaka 30 ya Bongo Fleva, mashairi yao wakipanda jukwaani wakiimba mashabiki wanaitikia na kuimba nao, ukisikiliza unahisi kuguswa na ujumbe wao, kwanza walifanya kazi katika mazingira magumu ambayo wazazi hawakuamini kama muziki ni kazi.
"Kama sisi ambao ni kizazi cha tatu kutoka kwao bado ilituwia ugumu wazazi wetu kukubaliana na kazi ya muziki, mjiulize hao wengine walipitia njia ngumu zaidi kiasi gani, maprodyuza walikuwa wachache kina P Fank, Master Jay na wengine, hivyo msanii alikuwa akiipata nafasi ya kurekodi anaitumia vizuri.
"Kwa sasa msanii ana studio nyumbani kwake, inakuwa rahisi kuimba mashairi mengine ambayo ilimradi na wakati mwingine unasikiliza baadhi ya maneno huelewi yanalenga kuacha alama gani kwa jamii, ieleweke siwadharau bali nawakumbusha waendelee kujifunza."
Anasema lazima msanii ajue kuna wakati wa jina kuwa juu na kutajwa kila sehemu pia kuna muda ambapo jamii itatakiwa isalie na nyimbo zao za kusikiliza hata wakati umaarufu unaposhuka.
"Mfano kaka zetu walikuwa na uwezo wa kutoa wimbo mmoja unaweza kukaa hadi miaka miwili bado akawa maarufu katika jamii, basi miaka ya 30 ya Bongo Fleva, iwe somo kwao." amesema.