Sanaa ya Kibongo ni kunyonyana
Muktasari:
- Na kama ni wasanii ambao wanajisimamia wenyewe utasikia wakilalamika kuhusu unyonyaji wanaofanyiwa na wanaoandaa matamasha.
UKIZUNGUMZA na wasanii wa muziki kwa saa mbili tatu ghafla utasikia wanaanza kukuambia jinsi wanavyonyonywa kimaslahi na lebo. Watakuambia jinsi ambavyo menejimenti inachukua asilimia 40 nzima ya mapato wakati hawaandiki nyimbo, hawakeshi studio kurekodi wala hawana sauti za kuimba.
Na kama ni wasanii ambao wanajisimamia wenyewe utasikia wakilalamika kuhusu unyonyaji wanaofanyiwa na wanaoandaa matamasha. Waandaaji matamasha bila aibu wanaweza kumpigia msanii mkubwa simu na kutaka kumlipa pesa mbuzi kwenda kwenye tamasha bila kujali gharama za uwezekaji alizofanya msanii na thamani ya ustaa wake. Na unakuta samtaimu msanii anaamua kukubali kwa sababu ya njaa.
Na kama si malalamiko ya waandaaji matamasha, basi yatakuwa malalamiko dhidi ya wanaowasaidia kuweka ngoma zao kwenye mitandao ya kidijitali kama vile Youtube, Spotify na kadhalika, kwamba nyimbo zinaweza zikakaa huko miaka nenda rudi wakienda kuomba mapato wanapewa pesa dusko. Na wakihoji wanapewa majibu ya juu juu tu kwamba ndo kilichopatikana.
Wakati wasanii wanalalamika kunyonywa na lebo, waandaaji wa matamasha na watu wao wa mitandao ya kidijitali… na wao pia wanalalamikiwa unyonyaji na maprodyuza wa muziki, waandishi wa nyimbo na madairekta wa video.
Maprodyuza kibao wameacha kufanya kazi na wasanii wa muziki kwa sababu ya unyonyaji. Maprodyuza wanaacha kufanya muziki wanaamua kukimbilia kutengeneza matangazo na redio drama kwa sababu wasanii hawawalipi.
Msanii anakuja studio anataka mkeshe usiku kucha mkitengeneza wimbo kisha baada ya hapo akupe elfu hamsini ya umeme na kukunulia pombe kubwa moja na pakti la sigara. Yeye akitoka hapo anakwenda kutengeneza mamilioni na wimbo huohuo ambao prodyuza ametumia muda na ubunifu kuutengeneza. Yaani unyonyaji tu.
Ukigeuka upande wa pili waandishi wa nyimbo wanalalamika kunyonywa na wasanii ile mbaya. Ukiona mwandishi wa nyimbo Bingo anahojiwa na media tegemea kumsikia akilalamika jinsi ambavyo amemuandikia msanii ngoma BUREEE na hawajawahi kupata hata senti kumi ya ziada kutoka kwenye mapato ya ngoma yake aliyoiandika. Lakini mbali tu na mapato, muda mwingine hata kutajwa kwamba wameandika hizo ngoma hawatajwi. Yaani unyonyaji tu.
Madairektra wa video nao wembe ni uleule… wanakwambia jinsi msanii anavyokuja na wazo kubwa la video, lakini bajeti mbuzi. Au muda mwingine wanalipa nusunusu au kwa kuchelewa. Madairekta wanabaki na madeni ya kukodi vifaa vya uzalishaji kama kamera na kadhalika, na mwisho wa siku wao ndio wanaonekana matapeli.
Ukiniuliza cha kufanya nitakuambia hapa tatizo sio wasanii kuwanyonya maprodyuza, madairekta na waandishi wa nyimbo. Na wala tatizo sio lebo na watu wa mitandao ya kidijitali kuwanyonya wasanii. Hivyo ni viashiria au matokeo ya mzizi wa tatizo ambalo ni ukosefu wa mfumo bora kwenye sekta ya sanaa nchini.
Sehemu walizotutangulia wana mifumo ambayo mtu huwezi kunyonywa waziwazi kiasi hicho. Yaani hata kama mtu atakuibia basi ni hadi afanye kazi kwelikweli - atumie usomi na makaratasi ya kutosha na bado hata akifanya hivyo kuna uwezekano wa kutokewa puani na matendo yake. Kwa hiyo, kwa sasa tusihangaike na kumaliza unyonyaji, bali tuhangaike na kutengeneza mfumo wa sanaa kuufanya uwe bora kisha haya mengine yote yatajimaliza yenyewe.