Bongo Movie igeni suala la matangazo kwenye kampeni
Muktasari:
- Sijui wanalipwa au wanasambaza upendo tu, lakini ninachojua ni kwamba wana jambo moja kubwa la kujifunza kwenye kampeni hizo ” jinsi ya kufanya matangazo.
KUSEMA kweli Bongo Movie wamezipamba kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka huu kuliko mwaka wowote ule. Kwenye mikutano ya kampeni utawaona makumi kwa makumi wamejazana ama kuunga mkono kwa kumsindikiza mgombea wanayempenda au kupanda jukwaani na kutoa burudani za hapa na pale.
Sijui wanalipwa au wanasambaza upendo tu, lakini ninachojua ni kwamba wana jambo moja kubwa la kujifunza kwenye kampeni hizo ” jinsi ya kufanya matangazo.
Filamu na tamthilia za Bongo zimepiga hatua sasa hivi kwenye upande wa uzalishaji. Picha nzuri, sauti bora na unaandaji kwa ujumla umenyooka.
Lakini pamoja na maendeleo hayo, kuna mambo ya msingi bado yanapuuzwa. Moja kubwa ni suala la matangazo. Waandaaji wengi wa filamu nchini hawalipi kipaumbele tofauti na wenzetu waliotutangulia ambao wana sera thabiti ya kutenga sehemu kubwa ya bajeti kwa ajili ya promosheni.
Kwa mfano, katika nchi zilizoendelea kwa viwanda vya filamu wanashauri angalau nusu ya gharama ya kutengeneza filamu itumike kwenye matangazo. Yaani ukitumia Sh50 milioni kutengeneza filamu, basi hakikisha matangazo yako si chini ya Sh25 milioni. Wengine wanafika mbali zaidi bajeti ya matangazo na ile ya utengenezaji zinafanana.
Kwa Bongo huenda si rahisi kufuata sera hiyo kwa asilimia zote, lakini waandaaji wanaweza kuja na mbinu zinazowasaidia kufanya matangazo yenye mvuto na uelewa na kuhakikisha wanalipa watu kuyasambaza yakafika mbali kama ambavyo wanasambaza matangazo ya kampeni za wagombea wanaowaunga mkono.
Mara nyingi msanii akitaka kutangaza kazi utakuta anaposti makava mara mbili tatu Instagram halafu anaona inatosha. Tena anaposti peke yake na watu wake wawili watatu. Lakini, kwenye kampeni unakuta tangazo moja linapostiwa na wasanii 100 kwa wakati mmoja. Staili na nguvu kama hiyo ingetumika kwenye kutangaza kazi zao hata kwa nusu ya nguvu inayotumika huko, naamini wangepata zaidi ya wanachopata hivi sasa.
Na kama wanaona ni kipengele wanaweza kujifunza kwa wasanii wa Bongofleva. Hawa wamekomaa mno kwenye masuala ya matangazo kuanzia makava mazuri ya nyimbo, chalenji mitandaoni hadi mikakati ya kushirikisha mashabiki. Msanii wa Bongofleva anapotoa ngoma anahakikisha anapata ‘ukoo’ wa kumsaidia kuposti. Wasanii wa Bongofleva wana magrupu ya wadau ambao kazi yao ni moja tu - msanii anapoachia kazi wao wanaichukua na kuisambaza kwa fujo utadhani vichaa. Pengine hiyo ndo sababu kazi za muziki zinakwenda zaidi.
Mfano mwingine mzuri ni Lamata Leah kupitia tamthilia yake ya Jua Kali. Ametumia mikakati mingi kuhakikisha kazi yake inafahamika, ameweka mabango, kuandaa matukio ya watu kutazama sehemu mpya kwa pamoja na kufanya kampeni ndogondogo mitandaoni. Haya yote yamefanya kazi yake ionekane tofauti na nyingi zinazotoka Bongo. Kwa hiyo ni kitu ambacho kina mifano ya wazi.