Ruby hana mpango na lebo za muziki

Muktasari:
- Akizungumza na Mwanaspoti, msanii huyo alisema chaguo lake lilitokana na nia ya kulinda uhuru wake wa kisanii, hasa kwa sauti yake ya kipekee inayofanya mchanganyiko wa muziki wa Kitanzania na Kiafrika.
NYOTA wa Bongo Fleva, Ruby amefunguka kuhusu uamuzi wake wa kubaki huru licha ya kupokea ofa nyingi kutoka lebo mbalimbali za muziki zikitaka ajiunge nao.
Akizungumza na Mwanaspoti, msanii huyo alisema chaguo lake lilitokana na nia ya kulinda uhuru wake wa kisanii, hasa kwa sauti yake ya kipekee inayofanya mchanganyiko wa muziki wa Kitanzania na Kiafrika.
“Nimekuwa msanii wa kujitegemea kwa miaka mingi sana na ina faida na hasara zake, sema kitu watu hawakijui baada ya kuachia wimbo wangu wa kwanza 'Na Yule' mwaka wa 2016, lebo kadhaa za rekodi zilinifikia, lakini nilikuwa na shaka kwa sababu sikutaka mtu yeyote aniondolee uhuru wangu wa ubunifu,” alisema Ruby.
Ruby aliongeza, wakati huo lebo zilizoanzishwa hazikuwa aina inayokubalika na wengi na alihofia lebo zingemlazimisha kubadilisha muziki wake ili kuendana na mitindo ya kibiashara.
"Ustadi wangu binafsi ambao unafafanua sauti inayobadilikabadilika. Najisikia vizuri kujulikana kama msanii wa kujitegemea, imemsaidia pia kuwa na mashabiki waaminifu licha ya shaka ya awali kuhusu maisha marefu ya muziki wangu," alisema Ruby.