Z Anto ataja silaha dhidi muziki wa AI
Muktasari:
- Katika mahojiano aliyofanya na Mwanaspoti, Z-Anto anatofautisha kati ya muziki wa vipaji halisia na AI, jambo la msingi analosisitiza ni binadamu aendelee kuaminiwa na kazi yake ipendwe na jamii anahitaji ubunifu na uwekezaji wa muda.
JE, unataka kujua wasanii wanafanyaje kazi katikati ya teknolojia ya uimbaji wa muziki wa AI inayotamba kwa sasa, mkongwe wa Bongo Fleva, Ally Mohamed almaarufu kama Z-Anto amelifafanua hilo.
Katika mahojiano aliyofanya na Mwanaspoti, Z-Anto anatofautisha kati ya muziki wa vipaji halisia na AI, jambo la msingi analosisitiza ni binadamu aendelee kuaminiwa na kazi yake ipendwe na jamii anahitaji ubunifu na uwekezaji wa muda.
Z Anto aliyefafanua jina hilo linatokana na kuunganisha vitu, Z ni herufi ya mwisho inayotokana na kuwa mtoto wa mwisho kati ya sita waliozaliwa katika familia yao, A inawakilisha jina lake la Ally, To inamaanisha Tony, jina lake la kwanza la kisanii wakati anaanza kuimba muziki.
Katika mahojiano hayo amezungumzia na ukimya wake kwa sasa, ingawa ana kazi ambazo hajaanza kuziachia unatokana na kufanya shughuli nyingine za kumtengenezea kipato.
“Ukimya wangu kwa sasa nimewekeza muda wangu kwenye shughuli ya uuzaji wa viwanja, tuna kampuni ya familia inayosimamia ishu hiyo, ndiyo maana umeona kuna ukimya,” anasema na kuongeza;
“Nafanya uandishi kwa sasa nina EP yangu ina nyimbo tano, nikianza kuzitoa zitanirudisha kwa mashabiki kwa kishindo, ndiyo maana nimesema nahitaji muda mwingi wa kufuatilia, hicho ndicho kinachonisubirisha kwa sasa.”
MUZIKI WA AI
Anasema pamoja na mabadiliko ya sayansi na teknolojia yaliyopo kwa sasa, bado waimbaji wenye vipaji vikubwa wana nguvu ya kufanya muziki wenye ushawishi mkubwa mbele ya muziki uliotengenezwa na AI.
“Muziki wa AI una toni zinazofanana, tofauti na akili ya binadamu ambayo ndani yake kuna ubunifu na hisia zinazogusa moja kwa moja jamii, hivyo wanaotumia akili na uwekezaji wa akili bado wanatikisa kwenye kiwanda cha muziki,” anasema Z-Anto shabiki wa Yanga lialia.
Anasema wasanii wa sasa wana uwanja mpana wa kufanya muziki kama biashara, tofauti na zamani ambao waliishi kishikaji zaidi: “Kwa sasa kila kitu ni pesa, kikubwa wanamuziki wenyewe waendelee kufanya sanaa kwa ubunifu, maana soko lipo wazi na linampa kila mtu uhuru wa kipaji chake kuonekana na jamii.”
Jambo la msingi analowashauri, wasiingie studio kwa kulipua ili mradi waendelee kusikika muda wote katika jamii, badala yake wahakikishe wanaacha legasi kwa jamii.
“Wakati mwingine muziki mzuri unajitambulisha wenyewe bila kuwa na vitu vya kandokando, ingawa jamii ya sasa inapenda kufuatilia zaidi vitu ambavyo siyo halisi,” anasema.
BINTI KIZIWI
Anasema wakati anauandika wimbo wa Binti Kiziwi alioutoa mwaka 2007 alitumia muda mwingi kuufanya uwe mkubwa: “Niliandika sikuingia studio kuurekodi nikaufuta, baada ya mwaka mmoja nikaandika tena na nikatumia mwaka mmoja kuumaliza, maana nilikuwa naandika naacha, baada ya kuukamilisha ukapendwa na kupokelewa kwa ukubwa, ilinichukua miaka mingi kuandika mwingine mkubwa wa Kisiwa Cha Malavidavi ambao ulinitambulisha kimataifa.
Anasema: “Wakati wa kurekodi video nilifanya machaguzi ya warembo tisa, wa tisa tulikuwa hatufahamiani nikamkuta lokesheni, nikamsalimia kama mara mbili hakuniitikia alinionyesha dharau za juu, baada ya kuja mabosi zangu wakaniambia atakayekucheza kwenye video yako ni huyu, ndipo akaanza kujichekesha ila kwa kuwa alionyesha rangi zake kabla hazijaonekana za kwangu nilimkataa.
“Hiyo ndiyo ikawa sababu ya kufanya na mtu ambaye nilikuwa naye kwenye mahusiano na baadaye nikamuoa kabla ya kuachana, kitu ambacho tunazingatia kwenye kuchagua watu wa kushuti nao ni ujumbe uliopo kwenye nyimbo.”
Unapomuuliza Sandra Khan almaarufu Binti Kiziwi aliyekuwa mkewe anamzungumziaje, Z-Anto anajibu: “Kwa sasa sijui ni mtu wa aina gani, ana maisha mengine nina maisha mengine, tofauti na ambavyo ningeweza kumzungumzia kwa enzi zile za utoto.”
Anaongeza: “Ipo hivi katika mahusiano tabia hubadilishwa na mtu, ingawa wakomavu wa akili hawawezi kubadilishwa na chochote, ukiwa na mtu leo kama aliishi na mtu mwenye tabia tofauti na mkaachana basi anaenda kuishi naye siyo yule wa zamani, atakuwa na tabia zilizoongezeka kwake.”
Kuna wakati alikuwa kwenye mahusiano na msanii wa Bongo Movie, Wastara Juma anapoulizwa kuhusiana na hilo anasema: “Tabia yangu ni kunyamaza, ukiona hadi nafikia hatua ya kukaa pembeni na kitu chochote ujue nimevumilia hadi nimeshindwa, mapenzi yanapoisha inaweza ikawa wivu, au kuchokana, mnaweza mkaachana kwa amani au uadui, sasa kuhusiana na hilo naomba nisilizungumzie.”
ANAVYOTUNZA MWILI WAKE
Msanii huyo anasema kitu wasichojua watu wengi, katika maisha yake hakuna chakula anachokipenda, analazimika kula pindi anapojisikia njaa.
“Asubuhi napenda zaidi kula vyakula vya kuchemsha, inaweza ikawa viazi, majimbi, mchana kuna muda sili kabisa nisiposikia njaa, nadhani hilo linachangia nisiwe na mwili,” anasema na kuongeza;
“Jambo lingine situmii kilevi cha aina yoyote ile, siyo mtu ninayependa starehe nisipokuwa na kazi napenda kupumzika zaidi, lakini napenda zaidi kuswali hivyo naona kila kitu ni neema za Mungu.”