R.Kelly agonga mwamba, agomewa kuachiwa gerezani

Muktasari:
- Timu ya mawakili wa nyota huyo wa zamani wa R&B iliwasilisha ombi Juni 17, ikitaka apewe kifungo cha nyumbani badala ya kusalia gerezani kutokana na 'tishio la moja kwa moja la maisha yake.'
CHICAGO, MAREKANI: MKONGWE wa muziki wa R&B, Robert Kelly maarufu kama R.Kelly, amekataliwa ombi lake la kuachiwa kutoka gerezani siku chache baada ya mawakili wake kudai kuwa alizidishiwa dawa kutokana na njama ya kumuua iliyokwama.
Timu ya mawakili wa nyota huyo wa zamani wa R&B iliwasilisha ombi Juni 17, ikitaka apewe kifungo cha nyumbani badala ya kusalia gerezani kutokana na 'tishio la moja kwa moja la maisha yake.'
Hata hivyo, Jaji Martha Pacold ameamua kuwa 'hakuna msingi wa kisheria kwa mahakama kushughulikia ombi hilo' na kulitupilia mbali.
Mawakili wa Kelly walidai wiki iliyopita kuwa msanii huyo alizidishwa dawa baada ya walinzi wa gereza kumpa makusudi dozi kubwa ya dawa kupuga wasiwasi na maumivu.
Pia walidai R. Kelly mwenye umri wa miaka 58, ambaye jina lake halisi ni Robert Sylvester Kelly aliondolewa hospitali kwa nguvu licha ya madaktari kugundua kuwa kulikuwa na tatizo kwenye damu yake na miguuni ambako anatakiwa kufanyiwa upasuaji.
Waendesha mashtaka wa serikali walikataa madai hayo wakati huo wakisema ni 'mambo yasiyo na maana' na wakasema ombi la hivi karibuni linadhihaki mateso waliyopitia waathirika matukio ya unyanyasaji wa ngono ambayo nyota huyo aliyafanya enzi zake.
Hata hivyo, mawakili wake walidai, 'kila muuaji, mbakaji na gaidi aliyepatikana na hatia atakuwa na nafasi mpya ya kupata uhuru' kama Kelly angeachiwa.
Pamoja na hilo na kukataliwa kwa ombi la kifungo cha nyumbani, wakili wake Beau Brindley alisisitiza kwamba yeye na timu yake ya sheria wangewasilisha ombi jipya wakidai kuwa kuna 'ushahidi mpya uliogunduliwa.'
Brindley alisema ombi hilo pia litaomba dhamana ya haraka wakati shauri hilo likiendelea na kwamba, " Hatukushangazwa na uamuzi huu kwa kuwa tulijua kuwa suala la mamlaka ya kiufundi lingekuwa changamoto katika mazingira haya."
Brindley akizungumza na USA TODAY, alisema: "Awali, hata hivyo, hatukuwa na chaguo bali kuchukua hatua mara moja kutokana na ushahidi wa wazi wa tishio kwa maisha ya Robert Kelly."
Kulingana na USA TODAY, hadi Juni 19, Brindley na timu yake walikuwa hawajawasilisha ombi jipya, lakini R.Kelly alidaiwa kuwekwa katika kifungo cha peke yake 'kinyume na mapenzi yake' kufuatia ombi jingine la mawakili wake lililodai kuwa maofisa watatu wa gereza walipanga njama ya kumuua kupitia genge la ubaguzi wa rangi la Wazungu.
Timu yake ya sheria ilinukuu kiapo cha mgonjwa wa saratani gerezani aitwaye Mikeal Glenn Stine aliyedai kuwa maofisa wa gereza walimtaka amuue mwanamuziki huyo.
R.Kelly aliomba apewe kifungo cha nyumbani kutokana na makosa aliyohukumiwa nayo yakiwemo ngono dhidi ya watoto na kushawishi wasichana wadogo kufanya nao ngono. Waendesha mashtaka waliita jaribio lake la kutaka kuachiwa kwa makosa ya kingono kuwa 'la dharau.'
Stine, ambaye ni mfuasi wa genge la Aryan Brotherhood, alidai maofisa waandamizi wa gereza walimpa fursa ya kutoroka na kuishi miezi yake ya mwisho akiwa huru kabla ya ugonjwa wa saratani kumuua na katika maelezo hayo, ilidaiwa zaidi kuwa alilazimishwa kutekeleza mauaji hayo Machi alipohamishiwa kwenye sehemu anayoishi R.Kelly gerezani akiambiwa na watumishi wa gereza 'unapaswa kufanya kile ulichokuja kufanya hapa.'
Alisema alimvizia R.Kelly kwa miezi kadhaa akifikiria namna ya kutekeleza njama hiyo, lakini alibadili mawazo na kumwambia kuhusu mpango huo, kulingana na nyaraka zilizotajwa na The Independent.
Mawakili wa mwanamuziki huyo pia walisema walipata taarifa za njama ya pili Juni, mwaka huu ya kumshawishi mfuasi mwingine wa Aryan Brotherhood kuwaua R.Kelly na Stine na pia mawakili waliomba msamaha kutoka kwa Rais Donald Trump, wakisema kuwa msanii huyo 'hana muda wa kusubiri haki kutoka kwa mahakama ambayo itakuja baada ya kufichuliwa kwa rushwa iliyopo katika kesi zake.'
Awali, mawakili hao walidai 'wana mazungumzo na watu kadhaa wa karibu na Ikulu ya Marekani na Rais Trump.'
R.Kelly alipatikana na hatia mwaka 2021 na 2022 kwa makosa hayo na mengine ya usafirishaji watu kingono.
Mahakama ya Shirikisho New York ilimhukumu kifungo cha miaka 30 gerezani mwaka 2022, na mwaka uliofuata akahukumiwa miaka 20 zaidi na Mahakama ya Shirikisho iliyopo Chicago.
Ushahidi wa kesi ya New York ulijumuisha ushuhuda wa waathirika zaidi ya 10 pamoja na video na vielelezo vya DNA.
Katika kesi ya Chicago ilibainika kuwa R.Kelly aliwavutia wasichana wadogo kufanya nao ngono ambapo alirekodiwa ikidaiwa kwamba alikutana na waathirika mwishoni mwa miaka ya 1990 wakiwa na umri wa miaka 14, 15 na 16.
Msanii huyo amekuwa gerezani tangu Julai 2019, na kwa sasa yuko katika gereza alilowahi kufungwa aliyekuwa tapeli maarufu Bernard Madoff. R.Kelly atakuwa na umri wa miaka 78 atakapokuwa na sifa ya kuachiliwa huru mwaka 2045.