Prime
Nyoshi: Nilijificha darini nisipelekwe rumande
MWANAMUZIKI mkongwe wa dansi na kiongozi wa Bogoss Musica, Nyoshi El Saadat, amefichua mkasa mzito ambao hadi leo hauwezi kuufuta kwenye kumbukumbu zake, akisimulia namna alivyowahi kujificha juu ya dari kwa saa kadhaa akihofia kukamatwa na maofisa wa Uhamiaji.
Nyoshi anasema tukio hilo lilitokea mwaka 2000 wakati kulikuwa na msako wa wanamuziki raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo waliokuwa nchini bila vibali halali vya kuishi.
Baadhi ya wanamuziki wenzake wa Stono Musica ‘Wajelajela’ iliyokuwa chini ya Ndanda Kosovo (marehemu) walikamatwa na kuwekwa mahabusu, jambo lililomfanya atafute namna ya kujinusuru. Haya ni mahojiano aliyofanyiwa na Mwanaspoti.
MWANASPOTI: Nyoshi, umewahi kutueleza mkasa wako wa kujificha darini, ulianza vipi?
NYOSHI: Siku hiyo siwezi kuisahau katika maisha yangu. Wenzangu wa bendi ya Stono Musica ‘Wajelajela’ ya marehemu Ndanda Kosovo walikamatwa na kuwekwa ndani kwa sababu ya utata wa vibali vyao. Mimi nilipoona hivyo nikasema nikizubaa hapa na mimi nitakamatwa na kwenda rumande. Ikabidi nikimbilie juu ya dari kujificha. Hii ilikuwa mwaka 2000.
MWANASPOTI: Ulikuwa darini kwa muda gani?
NYOSHI: Ilikuwa ni muda mrefu sana kwangu kwa sababu nilikuwa najua nikigundulika mambo yangu yameisha. Kulikuwa na joto, vumbi na giza. Chini maofisa walikuwa wanakagua kila sehemu. Nilikuwa nimebana pumzi nisije nikasikika. Nilikuwa nasubiri tu waondoke.
MWANASPOTI: Maofisa waliondoka bila kukugundua?
NYOSHI: Ndiyo. Walikagua chini, wakaangalia sehemu mbalimbali lakini hawakujua kama niko juu. Walipoondoka ndipo nikashuka. Nilikuwa nimejaa jasho na vumbi.
MWANASPOTI: Tukio hilo lilikufundisha nini?
NYOSHI: Lilinifundisha kwamba huwezi kuishi ukikimbizana na sheria. Baada ya hapo nilianza kuweka mambo yangu sawa, kuhakikisha nyaraka na vibali vinafuatwa. Nikaona ni lazima niishi kwa amani bila kuogopa tena.
MWANASPOTI: Tanzania imekuwa nyumbani kwako kwa muda mrefu. Unajisikiaje katika nchi hii?
NYOSHI: Tanzania imenipa maisha. Niliingia mwaka 1992 na nilipapenda kwa sababu ya upendo ambao Watanzania walinionyesha. Nilijiona kama niko nyumbani Congo. Na ndiyo maana nimeendelea kubaki. Muziki, watoto wangu na maisha yangu yote yamejengeka hapa.
MWANASPOTI: Umewahi kuomba uraia wa Tanzania?
NYOSHI: Ndiyo. Nimeishi hapa kwa miaka mingi sana. Nchi hii nimeipa maisha yangu na imenipa maisha. Natamani siku moja suala hilo likamilike.
Nyoshi aliwahi kuomba kupatiwa uraia wa Tanzania mwaka 2019, na anasema wakati huo alikuwa tayari ameishi nchini kwa zaidi ya miaka 25 na ana watoto.
MWANASPOTI: Ukirudi nyuma, nani aliyekufungulia mlango Tanzania?
NYOSHI: Asha Baraka na MK Group. Nilipokuja Tanzania walinipa nafasi. Bila wao huenda ningebaki Congo na kuendelea kucheza muziki kule.
Mwaka 2025, Nyoshi alitoa shukrani hizo hadharani wakati wa maadhimisho ya miaka 30 ya Asha Baraka katika muziki akisema MK Group ndiyo iliyomleta Tanzania na kumsaidia kukuza safari yake ya muziki.
MWANASPOTI: FM Academia imekuwa sehemu kubwa ya historia yako. Unaikumbukaje?
NYOSHI: FM Academia ilikuwa sehemu muhimu sana ya maisha yangu. Tulikuwa vijana wenye nguvu, tunapenda muziki na tulikuwa na kiu ya kufanya kitu kikubwa. Tulipata mashabiki wengi na muziki wetu ukawa sehemu ya maisha ya watu.
MWANASPOTI: Sasa ukiwa mmiliki wa bendi ya Bogoss Musica, changamoto kubwa ni ipi?
NYOSHI: Kila kizazi kina changamoto zake. Zamani tulikuwa tunategemea redio, televisheni na maonyesho. Sasa kuna mitandao ya kijamii, muziki wa kizazi kipya na aina nyingi za burudani. Lakini sisi hatutaki kufa. Tunataka dansi iendelee.
MWANASPOTI: Muziki umekulipa?
NYOSHI: Kwa upande wa pesa, siwezi kusema umenilipa sana kama watu wanavyofikiria. Lakini umenipa jina, heshima, marafiki na nafasi ya kufika sehemu nyingi duniani.
Nilipata maisha kupitia muziki na nimeweza kuwasaidia watu wengi.
MWANASPOTI: Unajulikana pia kwa uvaaji wako wa gharama. Hii ni kwa nini?
NYOSHI: Mimi napenda kuvaa vizuri. Nguo ni sehemu ya maisha yangu na ni sehemu ya taswira yangu kama msanii.
MWANASPOTI: Na kuhusu mkorogo ambao nao umekuwa sehemu ya stori zako?
NYOSHI: Mkorogo karibu uniue.
MWANASPOTI: Unamaanisha nini?
NYOSHI: Nilikuwa nachanganya vipodozi bila kuchagua. Kuna kipindi ngozi yangu ilianza kubadilika na kuwa mbaya.
MWANASPOTI: Baada ya miaka yote hii, bado una nguvu za jukwaani?
NYOSHI: Muziki uko kwenye damu yangu. Mimi nikiona jukwaa siwezi kukaa. Nataka kucheza, kuimba na kuwapa watu furaha. Ndiyo maana mpaka leo naendelea.
MWANASPOTI: Unataka watu wakukumbuke kwa kitu gani?
NYOSHI: Nataka wanikumbuke kama mwanamuziki aliyependa kazi yake, aliyewapenda mashabiki wake na ambaye hakukata tamaa.
Nimepitia mengi. Nimekuja Tanzania, nimejenga maisha yangu, nimekuwa na mafanikio na nimepitia misukosuko. Hata siku ile nilipokimbilia darini ilinifundisha maisha.
Leo nikisimama jukwaani najua nimepitia safari ndefu sana.
MWANASPOTI: Na Bogoss Musica unaiona wapi miaka ijayo?
NYOSHI: Nataka iwe bendi ambayo itaacha historia. Tunataka kuendelea na muziki wa ‘live’, kuwapa mashabiki burudani na kuwapa nafasi wanamuziki vijana.
Dansi haijafa. Kinachotakiwa ni kuendelea kuipigania.