Nyoshi El Saadat afunguka mipango ya Bogoss Musica
Muktasari:
- Akizungumza na Mwanaspoti, Nyoshi amesema tangu alipoanzisha Bogoss Musica miaka tisa iliyopita, hajawahi kukata tamaa, badala yake kila mwaka amekuwa akiongeza nguvu katika kazi zake ili kuhakikisha bendi hiyo inaendelea kufanya vizuri sokoni.
MWANAMUZIKI na mmiliki wa bendi ya dansi ya Bogoss Musica, Nyoshi El Saadat, amesema bado anaendelea kupambana kuhakikisha bendi hiyo inazidi kuwa imara na kubaki miongoni mwa bendi bora za muziki wa dansi nchini.
Akizungumza na Mwanaspoti, Nyoshi amesema tangu alipoanzisha Bogoss Musica miaka tisa iliyopita, hajawahi kukata tamaa, badala yake kila mwaka amekuwa akiongeza nguvu katika kazi zake ili kuhakikisha bendi hiyo inaendelea kufanya vizuri sokoni.
“Toka nimeunda Bogoss Musica sitaki kubaki nyuma. Kila mwaka naendelea kujiimarisha kwa nguvu kubwa ili bendi iendelee kuonekana bora,” amesema Nyoshi.
Msanii huyo amesema siri kubwa ya mafanikio yao ni kuandaa nyimbo zenye ujumbe pamoja na video za kiwango cha juu zinazoweza kuwavutia mashabiki wa muziki wa dansi ndani na nje ya Tanzania.
Nyoshi pia ameweka wazi kuwa baada ya kutoa wimbo wa Frida pamoja na Mkorogo, sasa wamejipanga kuachia kazi nyingine tatu kwa mpangilio maalumu.
“Baada ya Frida na Mkorogo, zifuatazo ni Salima, Mapenzi Kidonda pamoja na Generique Chomeka Chomoa kwa nguvu za Mwenyezi Mungu,” amesema.
Mbali na muziki, Nyoshi amesema Bogoss Musica ipo kwenye maandalizi ya kufanya matukio matatu makubwa kwa pamoja, jambo ambalo litakuwa sehemu ya kuonyesha mafanikio na mwelekeo mpya wa bendi hiyo.
Aidha, amedokeza kuwa wamejipanga kuingiza vyombo vya kisasa vyenye thamani kubwa vitakavyosaidia kuongeza ubora wa maonyesho yao jukwaani na kuifanya event hiyo kuwa ya kipekee zaidi.
“Vyombo vya kisasa viko njiani na vitafanya event yetu ing’ae zaidi. Pia kuna sponsors wakubwa wanakuja kushirikiana nasi, hivyo mashabiki waendelee kutega sikio,” amesema Nyoshi.