Nyoshi, Papii jukwaa moja la burudani
Muktasari:
- Tamasha hilo linatarajiwa kuwakutanisha Nyoshi El Saadat akiwa na Bogoss Musica, Papii Kocha, Mishi Zere aliyepata umaarufu kupitia wimbo Selina, Twaha Malovee anayefanya vizuri katika taarabu na muziki wa dansi, Hussein Yamodo akiwa na bendi yake ya Gold Musica pamoja na Freddy Midundo.
MASHABIKI wa muziki jijini Dodoma, Agosti 8, 2026 wanatarajiwa kushuhudia usiku wa burudani wa aina yake, pale baadhi ya mastaa wanaofanya vizuri katika muziki wa Bongo Fleva, dansi na taarabu watakapokutana katika tamasha litakalofanyika Arena Lounge, Nzuguni.
Tamasha hilo linatarajiwa kuwakutanisha Nyoshi El Saadat akiwa na Bogoss Musica, Papii Kocha, Mishi Zere aliyepata umaarufu kupitia wimbo Selina, Twaha Malovee anayefanya vizuri katika taarabu na muziki wa dansi, Hussein Yamodo akiwa na bendi yake ya Gold Musica pamoja na Freddy Midundo.
Mbali na burudani ya muziki, waandaaji wamesema usiku huo pia utatumika kutoa tuzo kwa baadhi ya wadau waliokuwa sehemu ya mafanikio ya Arena Lounge tangu ilipoanzishwa mwaka mmoja uliopita.
AHADI YA NYOSHI
Msanii Nyoshi El Saadat anasema amejiandaa kuhakikisha mashabiki wa Dodoma wanapata maonyesho yatakayowaacha na kumbukumbu nzuri.
“Dodoma imekuwa na mashabiki wengi wanaoupenda muziki wetu. Mimi pamoja na Bogoss Musica tumejipanga kutoa burudani ya nguvu na kuhakikisha kila atakayefika anarudi nyumbani akiwa ameridhika.”
Anasema matamasha yanayofanyika katika mikoa mbalimbali yanaendelea kusaidia kusogeza huduma ya burudani karibu na mashabiki.
“Ni jambo la kufurahisha kuona matukio makubwa hayabaki Dar es Salaam pekee. Dodoma nayo imeendelea kukua na mashabiki wake wanastahili kuona wasanii wao wakiwa jukwaani,” anasema.
MSIKIE PAPII KOCHA
Kwa upande wake, Papii Kocha anafurahia kuwa sehemu ya tamasha hilo na kuahidi kufanya kila linalowezekana kuwapa mashabiki burudani bora.
“Kila ninapokwenda Dodoma napokea upendo mkubwa kutoka kwa mashabiki. Hiyo inanipa hamasa ya kuandaa maonyesho bora zaidi kila ninapopanda jukwaani,” anasema.
Ameongeza ukuaji wa matukio ya muziki katika mikoa unaongeza fursa kwa wasanii na mashabiki kukutana mara kwa mara.
“Burudani inazidi kukua nchini. Tunahitaji kuona matamasha mengi zaidi kama haya kwa sababu yanawasaidia wasanii, wafanyabiashara na mashabiki kwa ujumla,” anasema.
WENGINE NAO TAYARI
Mbali na Nyoshi El Saadat na Papii Kocha, tamasha hilo litawakutanisha Mishi ambaye aliwahi kutamba na wimbo wa Selina akiwa na Alicom, Twaha Malovee, Hussein Yamodo akiwa na Gold Musica pamoja na Freddy Midundo.
Waandaaji wanasema wamekusudia kuwaleta pamoja wasanii wenye mitindo tofauti ya muziki ili kila shabiki apate burudani anayopenda.
TUZO KWA WADAU
Akizungumza na Mwanaspoti, Mkurugenzi wa Arena Lounge, Fadhili Dagila anasema usiku huo hautakuwa wa muziki pekee, bali pia wa kutoa shukrani kwa wadau waliochangia ukuaji wa Arena Lounge ndani ya mwaka mmoja.
“Tumefika hapa kutokana na ushirikiano wa watu wengi. Ndiyo maana tumeamua kuwapongeza na kuwatambua baadhi ya wadau waliokuwa nasi tangu mwanzo wa safari hii,” anasema.
HAKUNA KIINGILIO
Waandaaji wameeleza kuwa tamasha hilo litakuwa wazi kwa wananchi wote bila kiingilio, huku mshehereshaji akiwa ni Khamis Dacota Delavida.
Kwa mujibu wa waandaaji, lengo ni kuwapa wakazi wa Dodoma na maeneo ya jirani nafasi ya kufurahia burudani ya moja kwa moja kutoka kwa baadhi ya wasanii wanaofanya vizuri nchini.
Dagila, amebainisha kwamba, tamasha hilo linafanyika ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya mwaka mmoja tangu ukumbi huo uzinduliwe rasmi Agosti 8, 2025.
“Tulipoanzisha Arena Lounge tuligundua Nzuguni ilikuwa inakosa sehemu ya kisasa ya burudani. Tulitaka kujenga mahali ambapo watu watapata burudani salama na ya kiwango, huku tukiwapa nafasi wasanii kuonyesha vipaji vyao,” anasema Dagila.