Nandy Festival 2021 lapata udhamini mnono

MSANII wa muziki wa kizazi kipya Faustina Charles 'Nandy' ambaye kwasasa anaendelea na tamasha lake la Nandy Festival 2021 amepata udhamini wa tamasha hilo kupitia Kampuni ya mawasiliano ya TTCL.

Nandy chini ya uongozi wa tamasha hilo Eastwave Marketing wameingia mkataba na kampuni hiyo leo Jumatano, Juni 9, 2021 jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa Biashara kutoka, Vedastus Mwita amesema baada ya mchakato kukamilika sasa wamekuwa wadhamini wakuu wa tamasha hilo ambalo litaitwa TTCL Nandy Festival 2021 Watakaa tu.

Tamasha hili litafanyika mikoa 10 ambayo ni Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza, Sumbawanga, Kigoma, Shinyanga, Kilimanjaro, Tanga, Arusha na Zanzibar  huku matarajio yakiwa ni wananchi wa mikoa hiyo na visiwa vya Zanzibar wanapata burudani ya muziki  yenye ubora na kiwango cha Kimataifa.

Udhamini huo utafikia wadau kwa kiwango kikubwa katika kunogesha tamasha hilo inatoa ofa kwa wateja wapya ambao watasajili laini zao katika kipindi chote cha tamasha hilo na kwa mteja mpya atazawadiwa dakika 50 kupiga simu mitandao yote, MB 150 na sms 50 bure kwa siku saba.

“Tutafanya hivyo kwa kila mkoa ambao tutafanya tamasha hilo, hivyo wadau wajitokeze kwa wingi ili kunufaika na huduma hii," amesema Mwita

Mwita amempongeza Nandy kwa uthubutu wake wa kuanzisha hilo na kuwapa burudani mashabiki zake na wapenda burudani nchini na kwamba uthubutu huo ni ishara kuwa wanawake kupitia sekta mbalimbali wana uwezo mkubwa wa kuleta mageuzi makubwa kiuchumi, kijamii na kisiasa.  

Meneja wa Nandy, Moko Biashara amewashukuru wadhamini hao kukubali kumuunga mkono msanii huyo na kwamba tamasha hilo litakuwa chachu kwa wateja wao pamoja na mambo mengine wananchi wataweza kujisajili na kupata laini za mtandao wao.
Kwa upande wa Nandy amesema si jambo dogo na shirika hilo kukubali kumdhamini na kupitia tamasha hilo kuwarudisha Watanzania nyumbani kupitia burudani atakayoitoa mikoa iliyoandaliwa.

“Niwahakikishie tu kwamba nitafanya kazi kwa uweledi wa hali ya juu na tumeionesha mfano katika Mkoa wa Kigoma ambapo si chini ya nane ya mashabiki na wapenzi wa burudani waliingia katika tamasha letu na kupitia idadi hii tunayo matumaini ya kuwarudisha nyumbani waanze kutumia huduma zinazotolewa na TTCL” alisema Nandy

Tamasha hilo tayari limeanza kwa mafanikio makubwa mkoani Kigoma ambapo limewakutanisha mashabiki wengi na wapenda burudani mkoani humo na kuacha historia kutokana na wasanii wakubwa nchini ambao wameshiriki.