MZEE WA UPUPU: Swali linarudi kwako sasa Mwana FA, ingekuwa vipi isingekuwepo Februari

NAJARIBU kujenga tafakuri kupitia uteuzi wa Hamis Mwinjuma ‘Mwana FA’ kwa kulinganisha na utunzi wake wa ‘Ingekuwa Vipi’ wa mwaka 2002.
Matukio yote haya mawili, kutoa wimbo na kuteuliwa, yametokea mwezi Februari, yakitenganishwa na miaka zaidi ya 20.
UTEUZI
Februari mwaka huu, 2023, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, alimteua Mbunge wa Muheza, Hamis Mwinjuma maarufu kama Mwana FA, kuwa Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Mwana FA kama msanii, ametupwa kwenye wizara ambayo inamhitaji zaidi katika kusogeza mbele gurudumu la maendeleo ya sanaa.
INGEKUWA VIPI
Februari 2002, jina la Mwanafalsafa lilisikika kwa mara ya kwanza kwenye masikio ya Watanzania. Ilikuwa kwenye kipindi cha Bongo Flava cha Clouds FM, mtangazaji akiwa Steve B. Wakati huo hiki ndicho kilikuwa kipindi cha taifa cha muziki wa kizazi kipya.
Steve B alipiga wimbo huo kisha akatuacha wasikilizaji na maswali...ni nani huyu aliyeshirikiana na Jay Moe kwenye huu wimbo?
Jay Moe halikuwa jina jipya kwa sababu lilishasikika sana huko nyuma kupitia kundi la Wateule. Lakini huyu wa pili ni nani?
Ndipo Steve B akatufungulia Code kwamba huyu ni Mwanafalsafa...na huo wimbo ni wake, lakini amemshirikisha Jay Moe.
Kwa kweli jina lake na wimbo wake ni kama viliendana. Falsafa ni maarifa au elimu au uwezo wa kutafakari, kuelewa na kueleza mambo au kujenga hoja zenye mantiki na tafakuri kubwa. Na Mwanafalsafa ni mtu mwenye kuweza kufanya hayo.
Kwa namna mtunzi wa mashairi ya Ingekuwa Vipi alivyoyapangilia, alikuwa na haki kujiita Mwanafalsafa kwa sababu alitumia falsafa kubwa sana.
Lakini licha ya sifa zote za kifalsafa, wimbo huu uliimbwa kichokozi (diss na beef) kwa sababu kila mstari ulikuwa na kijembe kwa mtu fulani.
Na hii utaiona tangu kwenye aya ya kwanza.
Ingekuwa vipi angekuwa hai D-Rob na Chief Rhymson angekuwa Bongo,
Y-Thang bila kidato na umrudishe K-Singo.
Kwanza ingekuwa mfano au tayari ingekuwa chongo
Kati yao nani angekuwa wido na nani angekuwa mzigo?
Hapa yalitajwa majina makubwa sana katika historia ya muziki wa kizazi nchini Tanzania, tangu unaanza miaka ya 1980.
Majina yaliyotajwa hapa yalikuwa ya baadhi ya wasanii wa kundi la Kwanza Unit (KU Crew), moja ya makundi yaliyojenga misingi ya muziki wa kizazi kipya, Bongo Flava.
Hata hapo kwenye mstari wa tatu anaposema Kwanza ingekuwa mfano, hiyo Kwanza ndiyo KU Crew, yaani Kwanza Unit.
Yawezekana fika kuwa Mwanafalsafa kama kijana mwingine yeyote aliyekulia katika zama za mwanzo za muziki wa kizazi kipya, Kwanza Unit walikuwa moja kati ya makundi aliyoyafuatilia sana.
Lakini alipoanza kuandika mashairi ya wimbo huu mambo mengi hayakuwa kama yalivyokuwa zamani.
i. Kundi lenyewe lilikuwa tayari limesambaratika.
ii. D-Rob alikuwa ameshafariki.
iii. Chief Rhymson alikuwa akiishi Canada.
iv. Y-Thang alikuwa masomoni UK.
v. K-Singo alikuwa akiishi Afrika Kusini.
Kwa hiyo katika kuwaza kifalsafa, Mwanafalsa alitaka kutufikirisha sisi hadhira yake kama hawa wote wangekuwepo, yaani KU Crew ingerudi, bado wangeendelea kubamba au zingebaki stori? Na je kati yao nani angekuwa bado mkali na nani angekuwa wa kawaida?
Pia alimchokoza Dully Sykes ambaye wakati huo alikuwa akitamba na staili ya mwanasesere (Rap Cartoon). Lakini pia aliwachokoza Balozi Dola Sol na Mr. II na wengine wengi.
Hao wote hawakumjibu chochote, lakini kuna vichwa vibovu viwili havikumuacha salama.
Kwanza walikuwa watoto fulani kutoka Temeke, walioitwa Walume Ndago, ambao aliwagusa moja kwa moja kama wao lakini pia na taifa lao la kiumeni.
Ingekuwa vipi maisha ya Temeke yangekuwa juu kidogo
Unadhani wasanii wangejiita Walume Ndago?
Temeke ilikuwa wilaya ya watu wa kipato cha kati na cha chini katika wilaya zote tatu za Dar es Salaam za wakati ule.
Watu wanaoishi kwenye kipato cha chini hupitia mapambano mengi na magumu ya kutafuta riziki, na katika mapambano hayo hujipachika vyeo vya kishujaa wakijiona kama makamanda wa jeshi katika kupambana na matatizo yao
Hapo ndipo majina kama Walume Ndago yalipokuja. Walume Ndago maana yake ni wanaume ngangari au wanaume wa shoka...na ni Temeke huko huko ndiko lilikoibukia kundi la Wanaume miaka ya baadaye.
Walume Ndago au Wandago, hawakukubali unyonge, wakamjibu Mwanafalsafa kwa kutunga wimbo waliouita Ingekuwa Poa.. ambao walitumia mashairi yale yale ya Ingekuwa Vipi, lakini kwa kutoa majibu katika maswali ambayo Mwanafalsafa alikuwa akijiuliza.
Ingekuwa poa maisha ya Temeke yangekuwa juu kidogo
Lakini bado wasanii wangejiita Walume Ndago
Je unaelewa maana halisi ya neno Walume Ndago?
Nadhani huelewi bwana mdogo tuliza kipago
Lakini shida kubwa zaidi aliipata kutoka kwa mwanadada aliyeibuka kwa kasi sana wakati huo, kutoka Mwananyamala, Sister P.
Kwenye Ingekuwa Vipi, Mwanafalsafa hakumuacha salama Sister P. Alimpiga na mstari mmoja mfupi ambao ulijirudia mara mbili kuonyesha msisitizo.
Angeimba nini Sister P asingekuwepo Zay B
Ingekuwa wapi R&B asingekuwepo Jay Dee
Angeimba nini Sister P asingekuwepo Zay B
Ingekuwa wapi R&B asingekuwepo Jay Dee
Sister P ni msanii aliyepata jina kwa kumpiga kimistari msanii mwingine wa kike aliyeitwa Zay B. Mashairi yake mengi aliyaimba kumzungumzia Zay B ambaye wakati huo alikuwa na ugomvi mkubwa sana na Inspekta Haroun.
Zay B alipata jina alipomshirikisha Inspekta Haroun kwenye wimbo wa Niko Gado. Lakini baadaye wakatofautiana na Zay B kuhamia kwenye kambi ya hasimu wa Inspekta, Juma Nature. Huko wakafanya madurufu (remix) ya wimbo huo na ndani yake alimtukana sana Inspekta Haroun.
Ndipo alipoibuka Sister P kwa kumshambulia sana Zay B, naye akapata jina ghafla. Na hicho ndicho kisa cha Mwanafalsafa kusema Angeimba nini Sister P asingekuwepo Zay B?
Sasa katika majibu yake, Sister P kupitia wimbo wake wa Hey Dee Jay, alimpiga Mwanafalsafa na kitu kizito, namna hii
Mpu***vu anauliza ningeimba nini Sister P asingekuwepo ZayB (ikapita mistari miwili mitatu hapo, kisha akaendelea)
...swali linarudi kwako sasa heh heh...
Ungeimba nini Mwanafalsafa tusingekuwepo wasanii
Au ungekuwepo wewe bubu katika fani hii
Hadhira haijakuelewa sasa umeielimisha nini jamii
Au tukuite Fredro Starr kwa wimbo uliotafsiri?
Kimsingi wazo la wimbo wa Ingekuwa Vipi liligongana na wazo la wimbo wa mwanamuziki wa Marekani, Fredro Starr, ambaye Sister P amemtaja hapo.
Fredro Starr aliimba wimbo wa What If, ambao tafsiri yake ya Kiswahili ndiyo hiyo Ingekuwa Vipi.
Na katika What If, Fredro Starr alijiuliza maswali haya haya ambayo Mwanafalsafa amejiuliza kwenye Ingekuwa Vipi.
Tofauti kidogo ni kwamba, Fredro Star alizungumzia mazingira ya Kimarekani na Mwanafalasafa alizugumzia mazingira ya Kitanzania.
Kwa mfano, pale Mwanafalsafa aliposema ingekuwa vipi D-Rob angekuwa hai. Fredro Starr alisema: what if Notorious was here?
Na kwa kuwa wimbo wa Fredro Starr ulishatoka tangu mwaka 2001, jibu la wengi lilikuwa wazo la Mwanafalsafa lilichagizwa na wimbo wa Fredro Starr ...yaani alitafsiri, na ndicho alichomaanisha Sister P kwenye Hey Dee jay.
Hata hivyo, wakati ule kutafsiri nyimbo a mbele ilikuwa kawaida kwa sababu hata Mnyalu na wimbo wake wa Sintobadilika, alitafsiri wimbo wa Same Ol’ G wa Guinewine.
Lakini hayo yote yalitokea baada ya Mwanafalsafa kutoa wimbo wake ndani ya mwezi Februari mwaka 2002. Na miaka zaidi ya 20 baadaye, anateuliwa kuwa Naibu Waziri.
Kama alivyosema Sister P, swali linarudi kwako sasa heh heh...Ingekuwa Vipi Kusingekuwa na Februari, ungetoa singo yako au je ungepata uteuzi?
Anyaway, hii yote ni katika kusherehekea uteuzi wako Binamu. Tuko pamoja na tunatarajia mengi kutoka kwako.
Kila la heri!