Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Trey Songz awataka vijana kutokata tamaa

TREY Pict

Muktasari:

  • Trey Songz alitoa kauli hiyo jana alipokuwa akizungumza na wanafunzi wa vyuo vikuu walioshiriki programu maalumu ya ujasiriamali ya iMbeju, iliyoandaliwa na Benki ya CRDB kama sehemu ya jitihada za kuwawezesha vijana kukuza vipaji na mawazo yao ya kibiashara.

MSANII maarufu wa R&B kutoka Marekani, Trey Songz, amewataka vijana wa Tanzania kutokata tamaa katika kufuatilia ndoto zao, akisisitiza kuwa kujiamini, ubunifu na uvumilivu ni msingi wa kufikia mafanikio.

Trey Songz alitoa kauli hiyo jana alipokuwa akizungumza na wanafunzi wa vyuo vikuu walioshiriki programu maalumu ya ujasiriamali ya iMbeju, iliyoandaliwa na Benki ya CRDB kama sehemu ya jitihada za kuwawezesha vijana kukuza vipaji na mawazo yao ya kibiashara.

Msanii huyo amesema vijana wanapaswa kuamini uwezo wao na kutoruhusu maoni ya watu wengine kuwafanya waachane na ndoto zao, akieleza kuwa mara nyingi watu hushindwa kuelewa ndoto za wengine kwa sababu hawawezi kuziona kwa namna mwotaji anavyoziona.

TRE 01

“Usizilalie ndoto zako. Unapoota jambo fulani, huwa ni jambo maalumu kwako. Huenda lisiwe maalumu kwa watu unaowaeleza kwa sababu hawawezi kuona rangi, ukubwa na uwezekano unaouona wewe,” amesema.

Trey Songz amesema safari yake ya muziki haikuwa rahisi, akieleza kuwa alianza kuota kuhusu kuwa msanii akiwa na umri wa miaka 11 au 12 na kuanza kurekodi muziki akiwa na miaka 15.

Amesema ilimchukua muda kufikia mafanikio aliyonayo sasa, huku akikumbuka jinsi baadhi ya watu walivyomcheka na kumwambia kuwa hatafanikiwa alipowaeleza kuhusu ndoto yake ya kuwa mwimbaji.

“Ninatoka katika mji mdogo wenye watu takribani 25,000 hadi 30,000, ukiwa na shule moja tu ya sekondari. Nilipowaambia watu kuwa nataka kuwa mwimbaji, walinicheka,” amesema.

TRE 02

Amesema hakukubali maneno hayo yamkatishie tamaa, bali aliendelea kutafuta fursa za kuonyesha kipaji chake katika maonyesho ya mitindo, mashindano ya vipaji na maeneo mengine.

“Nilijaribu kuimba kila nilipopata nafasi. Nilichekwa na kuambiwa sitaweza kufanikiwa. Nilijiuliza, ingekuwaje kama ningewasikiliza watu hao,” amesema.

Trey Songz aliwataka vijana kuifanya sauti yao ya ndani kuwa kubwa kuliko maoni ya watu wanaowazunguka.

“Sauti unayozungumza nayo mwenyewe lazima iwe kubwa kuliko mawazo ya watu wengine,” amesema.

Amesema vijana wasijifanye wadogo kwa sababu watu wengine wanawaona hivyo, akisisitiza kuwa mtu anaweza kufikia mafanikio ambayo wengine hawajawahi kuyaona.

TRE 03

Trey Songz pia alizungumzia umuhimu wa ubunifu, akiwataka vijana wanaojihusisha na sanaa kutobaki kwenye mambo waliyowahi kuyaona, bali kutumia mawazo yao kuunda vitu vipya. “Usijifungie katika aina yoyote ya sanaa kwa kile tu ulichokiona. Ruhusu akili yako kuwa na mawazo mapya na kwenda sehemu ambazo haijawahi kufika. Hicho ndicho sanaa ilivyo,” amesema.

Akizungumzia uandishi wa nyimbo, amesema kazi yake imekuwa ikichochewa na mazingira, hisia na matukio anayokutana nayo katika maisha.

Mkuu wa Kitengo cha Uendeshaji CRDB Bank Foundation, Joycelean Makule amesema benki hiyo inawajali vijana ndiyo maana imeandaa tukio la kukutana na wanafunzi kutoka vyuo mbalimbali Dar es Salaam ili kuwapa hamasa na motisha ya kujiajiri na ujasiriamali.

Amesema kupitia tukio hilo, benki hiyo inalenga kuwapa vijana nafasi ya kupata maarifa.