Mume wa mwimbaji wa 'Ekwueme' akamatwa

Mume wa mwanamuziki nyota wa nyimbo za injili nchini Nigeria, Osinachi Nwachukwu aliyefariki mwishoni mwa wiki kwa madai ya ugonjwa wa saratani ya koo, amekamatwa na polisi kwa tuhuma za kuhusika na kifo cha nyota huyo wa "Ekwueme".
Nyota huyo wa injili, Osinachi Nwachukwu ,42, ambaye kibao chake cha "Ekwueme" kinaendelea kutamba barani Afrika, alifariki Ijumaa akiwa hospitalini jijini Abuja, mji ambao ni makao makuu ya serikali.
Wakati taarifa rasmi ikisema mwimbaji huyo alifariki kwa ugonjwa wa saratani, mitandao ya kijamii ilifurika tuhuma kuwa kifo chake kilitokana na ukatili wa nyumbani aliokuwa akifanyiwa na mumewe.
Jana, msemaji wa polisi wa jiji hilo aliviambia vyombo vya habari kuwa mumewe wa mwanamuziki huyo, Peter Nwachukwu amekamatwa baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa kaka wa Osinachi, tovuti ya Vanguard imeandika.
Tovuti ya Daily Trust imemkariri ofisa mahusiano wa polisi, Josephine Adeh akisema: “Hivi sasa yuko chini ya ulinzi. Mdogo wa marehemu aliripoti tukio hilo na tumeanza uchunguzi.”
Marafiki wa mwanamuziki huyo walitumia mitandao ya kijamii kueleza kuwa mwenzao alipigwa.
Katika video ya Instagram, mwimbaji maarufu, Frank Edwards, alimtuhumu mume wa Osinachi kumfanyia ukatili mara kadhaa.
“Mara moja ndani ya studio, huyu mtu alimpiga kofi kwa sababu tu alitaka kurekodi wimbo kwa lugha ya Igbo kinyume na utashi wake. (Osinachi) Hakufanya chochote peke yake," mwanamuziki huyo amesema katika video hiyo.
Dada mkubwa wa Osinachi pia alisemekana kuthibitisha kuwa mume huyo alimpiga teke kifuani na kusababishwa apelekwe hospitalini.
Dada huyo, Favour Made anadai teke hilo la mumewe lilisababisha damu kuvia kifuani na hatimaye kifo cha Osinachi, Vanguard imeripoti.
Pia Favour, ambaye alikuwa na Julieth Emmeh, amesema Osinachi alikuwa akinyanyaswa na mumewe kabla ya kifo chake.
"Hakufariki kwa saratani. Mumewe Peter Nwachukwu alimpiga na mguu wake kifuani. Yote hayo, pamoja na kupigwa kila mara, lakini dada yangu alituficha yote aliyokuwa akipitia," alisema Favour akikaririwa na Vanguard.
"Kabla tulimwambia aachane na ndoa hiyo na hawatakuwa wanatalikiana, ni kutengana tu. Lakini aliona kuwa Mungu hataki kuvunja ndoa.
"Tulimwambia kutengana si dhambi bali ni kwa ajili yake tu kuendelea kuishi na kulea watoto wake. Mara zote alituambia tutulie kwamba huyo mume atabadilika."
Tovuti ya Daily Post imemkariri ndugu mwingine ambaye hakutaka jina lake litajwe akisema "inatia uchungu kwamba licha ya ushauri wangu, huyu mwanamke mzuri ambaye ni dhahiri alikuwa zawadi kutoka kwa Mungu kuja duniani, aliamua kufia ndani ya ndoa. Kila mtu anajua kuwa amekuwa akipitia machungu makali".
“Nyuma ya tabasamu lake, kila mara unaona madhabahu wakati anapoimba ibadani au kwenye video. Kama mwinjilisti wa injili, hakupenda kile ambacho watu wangesema na mara zote aliendelea kumuamini Mungu hadi kifo chake," tovuti ya Daily Post imemkariri ndugu huyo.
Alisema baada ya kumpiga teke, mumewe alimpeleka hospitalini, lakini Osinachi hakuwaambia ndugu zake kilichotokea.
"Walikuwa ni rafiki zake wanaoishi karibu naye Jimbo la Ebonyi waliompigia pacha wake na kumuuliza, ‘dada yako amekuambia kuwa Peter alimpiga kifuani? Akamjibu kuwa hapana," alisema Favour akikaririwa na Vanguard.