Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

MIAKA 3 KIFO CHA KANUMBA: Wasanii wamepoteza ajira

Muktasari:

Steven Charles Kanumba alikuwa ni msanii, mwongozaji na mtayarishaji wa filamu aliyeifanya tasnia ya filamu nchini kuwa hai.

ILIKUWA Aprili 7, 2012 pale nyota iliyong’ara katika tasnia ya filamu ilipozimika ghafla.

Steven Charles Kanumba alikuwa ni msanii, mwongozaji na mtayarishaji wa filamu aliyeifanya tasnia ya filamu nchini kuwa hai.

Kanumba, alikuwa ni zaidi ya mwigizaji kutokana na uwezo wake wa kutengeneza uhalisia wa kile alichokuwa akikifanya katika filamu.

Katika miaka yake ya mwanzo kaburini kila ilipofika Aprili 7 ya kila mwaka kulikuwa na tukio kubwa kwa ajili ya kumbukumbu yake.

Lakini mwaka huu hilo halikufanyika zaidi ya mama yake mzazi, Frola Mtegoa kwenda katika kaburi la msanii huyo akiwa na wasanii wachache wanaoliona pengo lake.

Wasanii hao na mama Kanumba waliambatana katika makaburi ya Kinondoni jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kumkumbuka shujaa wao huyo aliyejijengea sifa kubwa Afrika Mashariki na kwingineko.

Uchunguzi uliofanywa na Mwandishi wetu, umebaini mambo yalitokea katika tasnia baada ya kifo cha Kanumba.

Moja ambalo lina athari kubwa ni kwa wale wasanii wote waliokuwa wakifanya kazi na marehemu kutengwa na watayarishaji.

Wengi wao hawashirikishwi katika filamu nyingine kulingana na kazi walizokuwa wakifanya kabla ya Kanumba kufariki dunia.

Ndani ya miaka mitatu wasanii hao waliokuwa wakimilikiwa na Kampuni ya Kanumba The Great Film hawana kazi kutokana kampuni hiyo kufa sababu kubwa ikiwa ni gharama za pango.

Kampuni imeshindwa kuzalisha filamu na aliyekuwa meneja wake Novatus Mayenja ‘Nova’ anakiri kuwa kifo cha bosi wake kimebadili kila kitu.

Nova amesema hali imekuwa mbaya, kwani hata wale watayarishaji waliokuwa wakiwahitaji hawawapi tena kazi na haelewi kuna uoga gani hadi imekuwa hivyo.

“Kwetu kila inapofika siku ya kumbukumbu ya Kanumba inatuuma sana, kwani karibu wote tuliokuwa katika kampuni yake, hatuna ajira za kudumu kama alivyokuwepo, tumebaki kuwa wanyonge,”anasema.

“Angalia mimi, Zakayo Magulu, Mayasa Mrisho ‘Maya’, Kiuno, Steve hatuna ajira njaa itatuua, nazungumzia njaa ya sanaa siyo ya tumbo, sasa ndio rahisi kugundua rafiki wa kweli,” anasema Nova.

Siyo hao tu, hata wasanii wachanga waliotolewa na Kanumba hasa watoto wadogo kama Hanifa Daud ‘Jennifer’, Patrick na wengineo hawajatumiwa na watayarishaji katika filamu zao na kuviacha vipaji vyao vikifa.

Ni wazi hakuna kitu cha kumuenzi Kanumba pamoja na kwamba alishirikilia uhai wa tasnia ya filamu achilia mbali kulitangaza taifa lake nje ya mipaka.

Hali ya soko

Hali ya soko ni mbaya kwani tangu kifo cha msanii huyo soko limetikisika, kumbuka alipofariki ghafla, filamu zote alizocheza ziliuzwa pasipo kuchagua kama ni ya zamani au mpya.

Siku ya mazishi yake ni siku iliyokuwa ya neema kwa wengi, kwa kila kitu kilichomhusisha Kanumba kiliuzwa, kuanzia fulana, vitabu nk.

Baada ya soko kuwa baya, hivi karibuni kampuni iliyokuwa ikifanya kazi ya usambazaji na marehemu, ilinunua filamu kutoka Mbeya ambayo marehemu aliwahi kuicheza na kuibadilisha jina kutoka Lethal Poison na kuiita Yamenikuta.

Filamu hiyo ilifanya vizuri sokoni jambo linalotufanya tukubaliane na imani za wale wanaoamini kuwa baada ya kifo chake soko limeyumba.

Kanumba ndiye msanii pekee aliyekuwa akiangalia soko na kulinyanyua kwa kutafuta wasanii wanaofanya vizuri nje ya nchi, ameweza kushirikiana na wasanii kama Ramsey Noah, Mercy Johnson, Emmanuel France kutoka Nigeria lakini tangu kifo chake hakuna msanii aliyefanya juhudi hizo zaidi ya kurekodi sinema zetu Morogoro.

Hata msanii ambaye alikuwa kama mpinzani wake katika tasnia ya filamu, Vincent Kigosi ‘ Ray’ amekiri kwamba kukosekana kwa Kanumba kumesababisha soko la filamu kudorora.

Ni miaka mitatu tangu kifo chake, filamu hazina ubora tena, ubabaishaji umekuwa mwingi na bei ya filamu inashuka siku hadi siku.

Lakini maswali ya kujiuliza ni inakuwaje mtu mmoja ndio anaongoza soko? Kwani watu wengine hawana ufahamu wa kutosha? Hivi watu waliokuwa wakishindana na Kanumba kwa nini wasiendelee kushindana na kutoa upinzani sokoni?