Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Miaka 10 ya Billnass katika Bongofleva ilivyotimia

MSANII wa Hip Hop Bongo, Billnass mwaka huu anatimiza miaka 10 katika muziki tangu atoke rasmi na kwa muda huo amefanikiwa kutengeneza ngoma nyingi kubwa, kushirikiana na wasanii wengine, kushinda tuzo, kuanzisha lebo na familia.

Jina la ‘Billnass’ limetokana na jina lake la kuzaliwa, William Nicholaus, yaani William (Bill) na Nicholaus (Nass) ambalo ni la Baba yake, ni kama walichofanya watu maarufu duniani kama Bill Clinton na Bill Gates ambao majina yao ya mwanzo ni William.

Utakumbuka Billnass alitoka rasmi kimuziki chini ya lebo ya Rada Entertainment baada ya kuachia wimbo wake, Raha (2014) ambao aliwashirikisha TID na Naziz, mwanachama wa kundi la Necessary Noize kutokea nchini Kenya.

Inaelezwa Mwana FA (Hamis Mwinjuma) ambaye sasa ni Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, alitakiwa kuwepo kwenye wimbo huo ikashindikana, ila Mwana FA alikuja kusikika katika wimbo mwingine wa Billnass, Mazoea (2017).

Baadaye Billnass alitoka Rada Entertainment kisha kufanya kazi na lebo nyingine kama L.F.L.G (Live First Live Good) na Rooftop Entertainment kabla ya kufungua yake, Mafioso Inc ambayo tangu mwaka 2021 imekuwa ikisimamia kazi zake.

Kwa kufungua lebo, Billnass aliungana na wasanii wengine wa Hip Hop Bongo waliofanya hivyo kama Joh Makini (Makini Label), Fid Q (Cheusi Dawa Entertainment), Moni Centrozone (Majengo Sokoni), Darassa (Classic Music Group (CMG)) n.k.

Bilnass alianza kuwika kimuziki akiwa bado mwanafunzi wa Chuo cha Biashara (CBE) ambapo mwaka 2017 alihitimu na kupata Shahada ya Ugavi na Manunuzi (Procurement and Supply Management). Na hapo chuo ndipo alikutana na mkewe Nandy kwa mara ya kwanza.

Katika mahojiano na Podcast ya Swahili Radio by Audiomack mwaka 2021, Billnass alisema hajafikiria kuajiriwa kutokana kuona kwenye muziki anapata fedha ambazo kuna muda zinaingia akiwa amelala tu, kwa mfano mauzo ya muziki mtandaoni.

“Kwanza wakati nasoma sikulenga sana kuajiriwa ila nilipohitimu nilifikiri kuhusu kuajiriwa. Unajua kuajiriwa si kile unachokipata bali ni ile nguvu yako unayotoa ili ile kazi ifanikiwe, sasa huo muda sitakuwa nao halafu nitaonekana sitimizi majukumu,” anasema.

“Ila kwa ngazi ambayo nimeisomea, na sio kwa ubaya nikisema niajiriwe sasa hivi unakuta fedha wanayotaka kukulipa ni moja ya fedha ambayo nikiwa balozi (influencer) wa kampuni au bidhaa moja unaweza kuitengeneza tu,” anasema Billnass.

Utakumbuka mastaa wengine Bongo wenye shahada na sasa wanafanya muziki ni pamoja na Jux, Nahreel, Roma (Sayansi ya Kopyuta), Feza Kessy (Usimamizi wa Biashara), Aika Navy Kenzo (Uongozi wa Biashara), Vanessa Mdee (Sheria) n.k.

Mwaka uliopita Billnass alikuwa ni msanii wa pili wa Hip Hop nchini aliyetazamwa zaidi katika mtandao wa YouTube akipata ‘views’ zaidi ya milioni 25.9, huku akiwa ametanguliwa na Darassa mwenye ‘views’ zaidi milioni 28.6.

Chini ya Darassa na Billnass katika 10 bora kuna Nay wa Mitego, Kontawa, Professor Jay, Roma Mkatoliki, G Nako, Stamina, Rosa Ree na Young Killer.

Kwa mujibu wa ripoti ya mwaka kutoka Boomplay Music, wimbo wa Billnass, Puuh (2023) akimshirikisha Jay Melody ndio wimbo wa Bongofleva uliosikilizwa zaidi katika jukwaa hilo kwa mwaka uliopita ambapo uliongoza kwenye chati kwa wiki sita.

Wimbo huo ambao hadi sasa umesikilizwa (streams) mara milioni 51 Boomplay na kuwa wimbo wake wa pekee Billnass kufikia mafanikio hayo, unafuatiwa na nyimbo kama ‘Utaniua’ wa Zuchu na ‘Mahaba’ wa Alikiba.

Ikumbukwe wimbo huo ndio ulimuwezesha kushinda tuzo yake ya kwanza ya muziki Tanzania (TMA) kama Msanii Bora wa Kiume wa Hip Hop 2022 akiwabwaga washindani wake ambao ni Kala Jeremiah, Country Boy, Fid Q na Joh Makini.

Wasanii wengine walioshinda TMA kwa mara ya kwanza kama Billnass baada ya kusota kwa muda ni pamoja na Rayvanny, Rosa Ree, Zuchu, Jay Melody na Mbosso, huku Gachi na Kontawa wakishinda kama Wasanii Bora Chipukizi.

Billnass alifikia mafanikio hayo mwaka 2023 bila kuachia kolabo na mkewe Nandy tangu walivyoanza utaratibu huo miaka minne iliyopita, wawili hao tayari wameshirikiana katika nyimbo nne, Bugana (2019), Do Me (2020), Party (2021) na Bye (2022).

Kwa mtiririko huo utaona tangu 2019 walikuwa wanatoa wimbo mmoja kila mwaka ila kwa mwaka 2023 hawakufanya hivyo, kwa kifupi tangu wamejaliwa mtoto wao kwanza, Naya aliyezaliwa Agosti 2022 hawajatoa wimbo wa ushirikiano.

Hadi sasa Billnass katika nyimbo zake amewashirikisha wasanii kama Nandy, Marioo, Jay Melody, Roma, Rayvanny, Whozu, Meja Kunta, Barnaba, Ril Vin, Mwana FA, TID, Nazizi n.k, huku akiwa bado hajatoa albamu wala EP katika miaka yake 10 ndani ya tasnia.