Lulu, Majizo kama ya Ronaldo, Rodríguez
Muktasari:
- Lulu na Majizo walifunga ndoa Februari 16, 2021 katika Kanisa la St Gasper, Mbezi Beach, Dar es Salaam, baada ya uchumba wa takribani miaka miwili.
KAMA ilivyo kwa mastaa wa kimataifa Cristiano Ronaldo na Georgina Rodríguez waliofunga ndoa yao kwa watu wachache, ndivyo ilivyokuwa kwa msanii wa filamu Elizabeth Michael ‘Lulu’ na mumewe Francis Ciza ‘Majizo’, ambao walifunga ndoa yao kwa utulivu bila sherehe kubwa.
Lulu na Majizo walifunga ndoa Februari 16, 2021 katika Kanisa la St Gasper, Mbezi Beach, Dar es Salaam, baada ya uchumba wa takribani miaka miwili.
Ndoa hiyo ilifungwa kwa siri na kuhudhuriwa na ndugu na watu wachache, tofauti na sherehe kubwa ambazo mara nyingi huambatana na ndoa za mastaa.
Miaka kadhaa baadaye, bado kuna shauku kutoka kwa mashabiki kutaka kujua kama wawili hao wana mpango wa kufanya sherehe ya ndoa yao.
Akizungumza na Mwanaspoti, Lulu amesema kwa sasa mpango huo haupo, huku akisisitiza yeye na Majizo wanaendelea kuishi vizuri bila kufanya sherehe hiyo.
“Haya, mlionisemaga nimeolewa ndoa haina watu kama ya mkeka, haya muone sasa wengine hao Cristiano Ronaldo na mke wake walivyo,” amesema Lulu.
Lulu anaeleza kuwa pamoja na kutofanya sherehe kubwa baada ya ndoa yao, hilo halijawazuia kuendelea na maisha yao kama wanandoa.
Kwa upande mwingine, suala hilo linafanana na ndoa ya Ronaldo na Georgina, hivi karibuni, 11 Agosti 2026, walifunga ndoa kwa utulivu katika sebule ya nyumba yao Cascais, Ureno, wakihudhuriwa na watu saba pekee.
Waliohudhuria ndoa hiyo walikuwa Ronaldo na Georgina pamoja na watoto wao watano. Baada ya ndoa, familia hiyo ilielekea katika Madhabahu ya Mama Yetu wa Fátima kwa ajili ya kupata baraka.
Georgina amesema uamuzi wa kufanya ndoa hiyo kwa watu wachache uliendana na namna walivyochagua kuishi maisha yao ya kifamilia.
Kwa Lulu na Majizo, miaka imepita tangu wafunge ndoa yao bila sherehe kubwa, lakini kwa sasa msanii huyo anasema hawana mpango wa kufanya sherehe hiyo, huku maisha yao yakiendelea bila presha ya kulazimika kuadhimisha ndoa kwa shamrashamra.
Hivyo, kama ilivyo kwa Ronaldo na Georgina, kwa Lulu na Majizo inaonekana si ukubwa wa sherehe unaopima ndoa, bali maisha wanayoendelea kuyaishi baada ya kufunga ndoa.