Lava Lava kafumania mara tatu!
Muktasari:
- Akiwa tayari ametoa albamu mbili, Lava Lava amejijengea jina kama msanii mwenye nidhamu na bidii ya kazi licha ya changamoto za tasnia ambazo amekumbana nazo. Fahamu zaidi.
KWA miaka yote Lava Lava anafahamika kama mwanamuziki wa Bongofleva mwenye sauti nzuri na mtunzi mwenye uwezo mkubwa wa kuandika nyimbo zenye hisia kali hasa kuhusu mapenzi na maisha.
Akiwa tayari ametoa albamu mbili, Lava Lava amejijengea jina kama msanii mwenye nidhamu na bidii ya kazi licha ya changamoto za tasnia ambazo amekumbana nazo. Fahamu zaidi.
1. Alitambulishwa na WCB Wasafi Mei 2017 akiwa ni msanii wa tano kusainiwa baada ya Harmonize (2015), Rayvanny (2016), Rich Mavoko (2016) na Queen Darleen (2016) ambaye awali alisainiwa G Records.
2. Extended Playlist (EP) yake ya kwanza, Promise (2021) iliwashirikisha wasanii wawili - Mbosso na Diamond Platnumz, na ya pili, Time (2025) nayo wasanii wawili - Billnass na Yammi.
3. Kabla ya kutoka kimuziki chini ya WCB Wasafi, Lava Lava tayari alikuwa amefanya kolabo na wasanii wakali Bongo kama Linex (Waoo!!) na Young Dee (Natafuta).
4. Hadi anaondoka WCB Wasafi alikuwa hajatoa albamu ila waliomkuta waliweza kufanya hivyo, Mbosso akitoa Definition of Love (2021), Zuchu, Peace and Money (2024) na D Voice, Swahili Kid (2023).
5. Shilole ndiye staa wa kwanza Bongo kuwa karibu na Lava Lava ambaye baadaye alimwandikia wimbo wake, Nyanganyanga (2016) kwa lengo la kutafuta njia ya kutoka.
6. Tangu alipotambulishwa kupitia wimbo wake, Tuachane (2017), hadi anaachana na WCB Wasafi huo ndio wimbo wake uliofanya vizuri zaidi YouTube ambapo video yake imetazamwa mara milioni 27. Kitu hiki kipo kwa Lava Lava pekee, wasanii wote walioanzia WCB Wasafi na kuja kuondoka, wameweza kutengeneza nyimbo nyingine kubwa zenye namba kubwa zaidi mbali na zile walizotambulishwa nazo awali.
7. Msanii wa kwanza wa kike kusaini katika lebo ya MJ Records, Shaa ana wimbo wake unaitwa Lava Lava (2013) uliotayarishwa na Giggz katika studio za MJ Records kwa Master J.
8. Lava Lava ni msanii mwingine aliyeondoka WCB Wasafi na kwenda kufungua lebo yake, ambayo ni Bite Gang inayosimamia kazi zake zote kwa wakati huu. Hivyo ameungana na Rich Mavoko (Billionea Kid), Harmonize (Konde Music), Rayvanny (Next Level Music) na Mbosso (Khan Music).
9. Na hadi anaondoka WCB Wasafi, Lava Lava alikuwa ameshirikiana na Bosi wake, Diamond katika nyimbo kama Zilipendwa (2017), Jibebe (2018), Quarantine (2020), Far Away (2021), Bado Sana (2021), Tuna Kikao (2023) na Kibango (2024).
10. Ukitazama video za nyimbo zake Tuachane (2017), Kilio (2018) na Gundu (2018), kuna matukio ya kufanana, nayo ni kufumania. Kwenye kila video, Lava Lava anamfumania mpenzi wake akiwa na mwanaume mwingine.