Kabla ya Mondi, Ciara kuna hawa..!
Muktasari:
- Mbali na Diamond, wasanii wengine walioshirikishwa katika albamu hiyo ni Chris Brown, Tyga, Busta Rhymes, Lil Baby, Teyana Taylor, Latto, Moliy, Normani, Jazze Pha, Big Freedia na BossMan Dlow.
STAA wa Bongo Fleva, Diamond Platnumz anafanya vizuri kwa sasa kimataifa kutokana na wimbo ‘Low’ kutoka kwenye albamu ya nane yake, Ciara wa Marekani, CiCi (2025) chini ya Beauty Marks Entertainment.
Mbali na Diamond, wasanii wengine walioshirikishwa katika albamu hiyo ni Chris Brown, Tyga, Busta Rhymes, Lil Baby, Teyana Taylor, Latto, Moliy, Normani, Jazze Pha, Big Freedia na BossMan Dlow.
Hata hivyo, hii si mara ya kwanza Diamond kuwepo katika albamu ya msanii mkubwa Marekani, Alicia Keys alimpa shavu katika albamu yake ya saba, ALICIA (2020) ambapo alisikika katika wimbo, Wasted Energy.
Vilevile Diamond amewashirikisha katika nyimbo zake wasanii wa huko kama Ne-Yo - Marry You (2017), Rick Ross, Waka (2017) na Omarion - African Beauty (2018), kazi zote hizi zikipatikana katika albamu yake ya tatu, A Boy From Tandale (2018).
Ukiachana na Diamond, wasanii wengine wa Bongo Fleva kama Ibra Da Hustler, Alikiba, AY, C Pwaa, Jay Moe, Mayunga na Harmonize, wameshirikiana na wasanii wa Marekani kama ifuatavyo.
Ibra Da Hustler & Loon, Humurak D Gritty
Kipindi Ibra Da Hustler akifanya vizuri na kundi la Nako 2 Nako Soulders, Loon kutokea Marekani alikuja Tanzania ndipo akaingia studio na kisha wakatoa wimbo wao, Worldwide Bachelor (2006).
Vilevile katika wimbo huo alisikika msanii mwingine kutokea Marekani, Humurak D Gritty ambaye aliongozana na Loon. Humurak D Gritty ndiye aliachana vesi ya mwisho ya wimbo huo uliotengenezwa na Dunga wa Madungu Digital.
Ikumbukwe Loon alikuja Bongo kwa ajili ya kufanya video ya wimbo wake mpya kwa wakati huo (Distracted, katika video ya hiyo alishirikisha warembo kadhaa wa Tanzania akiwemo Nancy Sumari, Miss Tanzania 2005.
Alikiba & R Kelly
Mkali wa RnB ambaye sasa yupo gerezani, R Kelly katika kitabu chake, Soulacoaster: The Diary of Me (2012), amezungumzia jinsi alivyokuwa na wakati mzuri kufanya wimbo na Staa wa Kings Music, Alikiba.
Wawili hao walikutana katika mradi wa One8 uliokutanisha wasanii wakubwa Afrika na kufanya wimbo wa pamoja, Hands Across The World ((2010) ambao ulifanya vizuri kwa wakati huo.
Mbali na Alikiba, wasanii wengine wa Afrika walioshiriki katika mradi huo ni Amani (Kenya), Navio (Uganda), 2Face Idibia (Nigeria), 4x4 (Ghana), Fally Ipupa (DR Congo), JK (Zambia) na kundi la Movaizhaleine (Cabon).
AY & La’Myia, Mis. Triniti
Ni wazi kuwa AY ndiye msanii wa kwanza wa Bongo Fleva kuanza kuwika kimataifa kwa kufanya kazi na wasanii wakubwa wa nje, kazi zake kuchechezwa kwenye vituo vikubwa vya televisheni vya kimataifa na kushinda tuzo kubwa za nje.
Katika mapambano yake alifanya kolabo na wasanii wa Marekani kama La’Myia na Mis. Triniti ambaye pia ana uraia wa Uingereza. Wawili hao aliwashirikisha kwenye wimbo wake uitwao, It’s Going Down (2014) na video yake ilifanyika nchini humo.
Kabla ya hapo alimshirikisha La’Myia na Romeo katika wimbo wake mwingine, Speak With Ya Body (2011) uliotengenezwa na Riley ambaye amefanya kazi na wasanii wakubwa Marekani kama Meek Mill, Lady Ganga, Tyga, Kanye West na Beyonce.
C Pwaa & Mis. Triniti, The Artist
Ukiachana na AY, marehemu C Pwaa ni miongoni mwa wasanii wa Bongo Fleva waliotamba sana kimataifa, naye alitoa wimbo na Mis. Triniti, Action (2010) ambao aliwashirikisha Dully Sykes na marehemu Mangwea.
Baadaye alikuja kumshirikisha msanii mwingine wa Marekani, The Artist katika wimbo wake, Mission Twelve O’clock (2012) ambao pia ulikutanisha wasanii wengine wa Bongo Fleva kama Lord Eyes, marehemu Godzilla, Mabeste na One The Incredible.
Jay Moe & Mims
Rapa Jay Moe aliyeanza muziki mwaka 1998 akiwa na kundi la Wateule, alimshirikisha Mims kutoka Marekani katika wimbo wake, You Can Never Be Me (2012) chini ya watayarishaji wawili ambao ni P-Funk Majani na Antonio.
Pia wimbo huo ulikutanisha wasanii wengine kama Avil kutoka Tanzania na Immu Cabir wa Msumbiji, ikiwa ndiyo kolabo kubwa ya kwanza ya kimataifa kwa Jay Moe, msanii wa kwanza kusainiwa Bongo Records.
Hata hivyo, wimbo huu uliofanyika kwa mtindo wa aina yake kwani Mims hakukutana na Jay Moe studio zaidi ya kutumiwa mdundo akiwa zake Marekani na kuingiza vesi yake kisha kurejesha Bongo kwa kina Majani kumalizia, na kazi ikatoka.
Mayunga - Akon (2016)
Wakati huo akiwa bado msanii anayechipukia, Mayunga alifanya kolabo na Akon msanii wa Senegal mwenye makazi yake Marekani na ndipo alipojenga himaya ya muziki wake kwa miaka yote.
Wimbo waliorekodi unaitwa, Please Don’t Go Away (2016), na hii ni baada ya Mayunga kushinda katika shindano la Airtel Trace Music Star Africa ndipo akapata nafasi ya kufanya kazi na nyota huyo ikiwa ni sehemu ya zawadi ya shindano hilo.
Mayunga aliachia ngoma hiyo Mei 2016 lakini tayari ulikuwa umerekodiwa tangu mwaka 2015 aliposhinda shindano hilo lilojumuisha nchi 12, fainali zake zilifanyika Nairobi Kenya Machi 2015, huku Akon akiwa ni sehemu ya Majaji pia.
Harmonize & Bobby Shmurda
Baada ya kufanya vizuri na ngoma, Single Again (2023), Harmonize aliamua rasmi kuendelea kulitafuta soko la kimataifa na ndipo akatoa wimbo wake, I Made It (2024) akiwashirikisha Bobby Shmurda wa Marekani na Bien kutokea Kenya.
Hata hivyo, licha ya promosheni kubwa na Harmonize kuuzungumzia wimbo huo kwa ukubwa wake huku director wa video yake, Ivan kudai imegharimu zaidi ya Sh100 milioni, bado mradi huo haukuwa na matokea makubwa.
Ikumbukwe Bobby Shmurda alivuma zaidi mwaka 2014 alipoachia wimbo wake ‘Hot...’ ulioshika nafasi ya sita chati ya Billboard Hot 100 na kupelekea kupata dili la kusainiwa Epic Records, kisha akatoa EP yake ya kwanza.