Johari ataja sababu kuchelewa kuolewa
Muktasari:
- Johari amesema anafahamu umri wake umeenda na anahitajika kufunga ndoa, ila kamwe hawezi kuwa mke wa pili kutokana na kutoweza vita za ukewenza na wivu alionao.
Muigizaji wa filamu, Blandina Chagula 'Johari' amesema anachelewa kuolewa sababu wanaume wanaojitokeza wengine wanataka wamuoe mke wa pili.
Johari amesema anafahamu umri wake umeenda na anahitajika kufunga ndoa, ila kamwe hawezi kuwa mke wa pili kutokana na kutoweza vita za ukewenza na wivu alionao.
"Mimi ni mkubwa kiumri jamani, na najua kiu ya Watanzania ambao ni mashabiki wangu kutaka kuona nimeolewa na wengi nikikutana nao huwa wananiambia niolewe, ila wajue kwamba wanaume wapo wengi wanaotaka kunioa ila wote unakuta washaoa wanataka niwe mke wa pili, mimi kwa kweli siwezi," amesema Johari.
Johari aliendelea kusema yuko tayari kuolewa na mwanaume ambaye anaweza kumsaidia na kumsapoti katika kila jambo analolifanya.
“Kwasasa nahitaji mwanaume wa kunioa mwenye kunithamini na kuwa mwaminifu, huku akinijali kwa kunisapoti katika kila jambo ambalo nitakalolifanya, sababu katika maisha yangu nimejifunza mambo kwenye mapenzi ikiwamo kuumizwa na furaha," amesema
Johari, staa alijaaliwa kipaji cha kuuvaa uhusika katika uigizaji akijua kuonyesha tofauti kati ya huzuni na furaha, alianza kuigiza tangu enzi za kundi la sanaa za maigizo la Kaole.
Mwigizaji huyu Desemba 1, 2024 kupitia tamthilia ya Yolanda nchini Afrika Kusini alinyakua tuzo mbili za ZIKOMO katika kipengele cha Msanii Bora na Tamthilia Bora. Kisha, usiku wa kuamkia Septemba 15,2024 nchini Nigeria alinyakua tena tuzo ya MVAA kama Mwigizaji Bora Afrika.