Isarito: 'Bunji' haikuwa kazi rahisi, mazuri yanakuja!
Muktasari:
- Zipo nyingi ingawa kwa viwango tofauti ikiwamo ya Eonii iliyotoka mwaka jana ikiwa ni muvi iliyokuja na mapinduzi ya teknoloji. Sasa kuna hii ya Bunji. Huko ndani kuna mapigano, visa vingi vikiwemo usaliti, mapenzi na mambo mengine.
WENGI wamezoea kuona filamu hasa tamthilia za mapigano kutoka mataifa yaliyoendelea Ulaya na Marekani. Hata hivyo, hata hapa nchini kwa sasa zimeanza kushika kasi.
Zipo nyingi ingawa kwa viwango tofauti ikiwamo ya Eonii iliyotoka mwaka jana ikiwa ni muvi iliyokuja na mapinduzi ya teknoloji. Sasa kuna hii ya Bunji. Huko ndani kuna mapigano, visa vingi vikiwemo usaliti, mapenzi na mambo mengine.
Nyota wa tamthilia hiyo inayorushwa na chaneli ya Sinema Zetu kwenye king’amuzi cha Azam TV ni Isarito Mwakalindile na balaa lake kwenye tathilia hiyo limemfanya azidi kuwa maarufu baada ya kutamba awali kwenye tamthilia za Jua Kali, Mpango Mbaya, Mlinzi na nyingine.
Mwanaspoti lilimtafuta na kufanya naye mahojiano na hapa anafunguka mengi kuhusu tamthilia hiyo na maisha yake kwa jumla na baada ya salamu mwandishi anaenda moja kwa moja kwenye kujua kuhusu changamoto katika kazi ya kuandaa tamthilia hiyo.
Mwanaspoti: Moja ya matukio yanayoonekana mwisho wa sehemu za mwanzo za tamthilia hiyo, mmnaonekana mnalinasua basi kwenye matope. Pamoja na hilo, changamoto gani nyingine mlizipata kwenye kushuti tamthilia hiyo.
Isarito: Changamoto ni nyingi. Gari kukwama tulitumia saa tatu kulitoa kwani Mbeya tunakofanyia kazi hii kuna udongo mfinyazi na mvua ilinyesha. Tuliomba msaada tukafanikiwa.
Wakati wa mvua pia inabidi msubiri ipite kwani kunaweza kukatokea ukungu ukafunika taa, hivyo kushindwa kuona na hata watu hamuonani na kusababisha picha zisitoke vizuri.
Mwanaspoti: Hizo nyingine ni zipi?
Isarito: Kuna kama kubadilisha waigizaji. Imetokea kwa wa mwanzo kupata shida hivyo ikabidi tumbadilishe. Aliyekuwa Mzee Mwake mwake na huyu wa sasa ni tofauti. Wa mwanzo ni wa hukuhuku Mbeya. Alipata matatizo kwani alikuwa ana mshono kwenye nyonga na ilitubidi wakati wa kushuti matukio ya kwanza twende naye taratibu lakini baada ya kuzidiwa aliomba apumzike. Kuna muda mwingine alizimia tukiwa ‘location’.
Pia akienda kusafisha kidonda kliniki inabidi kusubiri na kujikuta tunatumia muda mrefu kushuti na kwa sababu ni mzee wetu tulimsubiri ili pia tumalize msimu wa kwanza.
Mwanaspoti: Huyo mwingine mmemtoa wapi?
Isarito: Hii ni biashara, watu wasingetuelewa kwa nafasi hiyo. Ilibidi kutafuta mtu wa kuibeba na tukwamweka Mwake Mwake mwingine kutoka Kenya, anaitwa Mdhamir Sele.
Mwanaspoti: Mlifahamiana wapi?
Isarito: Mdhamir nilikutana naye Kenya. Kuna kazi nilienda kufanya huko. Pia nimeona sio mbaya kuchanganya watu wa nchi nyingine, ni nzuri kisoko na tunataka kuteka soko la Kenya kama mimi nilivyoenda kule wakateka la Tanzania.
Mwanaspoti: Ulitoa wapi wazo stori ya Bunji?
Isarito: Nilikaa na Director Lamaa. Tukiandaa stori lazima tujue kwa nini tunashuti. Mfano filamu ya Mlinzi, ni ya mapigano. Tumeonyesha maisha ya mlinzi nje ya kazi yake. Wengi tunawaona wakiwa kazini ‘getini’ ila hatujui maisha yao halisi. Huwa tunawadharau tu lakini huyo mlinzi tunayemdharau ana familia na watoto wanaomtegemea.
Tuliangalia pia watu wanataka nini. Wengi wanapenda komedi na drama tukaona tuweke mapigano itawezekana na hata mazingira ni mkoani mtu anatoka sehemu moja kwenda nyingine. Lengo ni kuwaonyesha hata Bongo tunaweza kutengeneza filamu nzuri na zikapendwa.
Mwanaspoti: Vipi kuhusu malipo?
Isarito: Wadhamini ni Azam, hivyo wanachofanya wanachukua bajeti yako kisha wakiwapa pesa mtajua mnalipanaje. Kama ni projuza atajua anawalipaje watu wake aliowaajiri.
Mwanaspoti: Vipi malipo... ni kwa kila kipande ‘scene’, sehemu moja ‘episode’ au kazi nzima ‘season’?
Isarito: (Huku akicheka) Hiyo ni siri yangu mimi na Azam
Mwanaspoti: Tamthilia ina urefu gani na sehemu ngapi na itachukua muda gani?
Isarito: Nisiwe muongo. Itategemea na mapokeo ya watu kwani hii ni biashara. Kama tuliowapelekea kazi wakiona inafanya vizuri wanaongeza mkataba kwani wanaamini itazidi kuwapa matangazo. Hata kwa wenzetu ndio hivyo hivyo.
Mwanaspoti: Ni kipande gani kwenye Bunji kinakuvutia zaidi.
Isarito: Kwa kifupi ni zote. Naona zina mvuto. Watu waendelee kufuatilia Bunji wataamini maneno yangu.
Mwanaspoti: Twaha Kiduku hajawahi kuigiza, ilikuaje ukaamua kumtumia na ulipata ugumu gani kumshawishi.
Isarito: Kweli sikupata ugumu kumtafuta kwani tunafahamiana muda mrefu hata nilipompa wazo la kushiriki kwenye tamthilia, kwanza alishtuka lakini nilimwambia ajiamini anaweza na ndio kama mnavyomwona anafanya vyema.
Mwanaspoti: Nafasi ya Champo inawavutia wengi. Kwa nini uliamua kumtumia?
Isarito: (Huku akicheka) Champo ni burudani sana. Si unajua yule ni komedi, pia tulipanga kuchanganya ladha ikiwamo komedi ndio maana nikamtumia Champo.
Mwanaspoti: Nini kilikusukuma kwenye uigizaji, ulianza lini?
Isarito: Mimi nilianza kufanya maigizo kanisani wakati nilipokuwa mdogo kipindi cha ‘Sunday School’ hasa wakati wa sikukuu za Chrismas na Pasaka. Nilikuwa naandaa maigizo kwa kutoa ujumbe wowote uliopo kwenye biblia. Hata hivyo, mwaka 2017 nilianza kuingia kwenye makundi ya sanaa ya maigizo. Nilikuwa naishi Mbagala Kilungule na huko kulikuwa na vikundi vingi vya maigizo, ikarahisisha mimi kuwa mwigizaji.
Mwanaspoti: Inasaidia nini kupitia kwenye vikundi vya sanaa?
Isarito: Naamini mwigizaji kupitia huko kwa sababu kunamkomaza na kupata elimu ya sanaa. Pia vinamsaidia mwigizaji kuwa na nidhamu kwenye kazi na morali ya kupenda anachokifanya, ndio maana hadi sasa naendelea na uigizaji katika Tamthilia mbalimbali.
Mwanaspoti: Mulky (Hidaya) ni mpenzi wako kweli nje ya mchezo? Na kabla ya kuigiza pamoja mlikuwa mnafahamiana?
Isarito: Hapana, kabla sikuwa namfahamu Mulky. Nimemfahamu baada ya kuletwa kwenye tamthiliya ya Jua kali, hivyo ukaribu wetu ni kazi tu hatupo kwenye mahusiano.
Mwanaspoti: Kwa hiyo watu wanawahisi vibaya?
Isarito: Ni kweli. Unajua kazi zetu za tamthilia zinatumia muda mrefu kushuti, hivyo mnakuwa pamoja kila mahali na kila siku. Ni rahisi kwa watu kuhisi hivyo.
Mwanaspoti: Historia yako ikoje tangu umezaliwa?
Isarito: Ni mtoto wa kwanza kwenye familia ya watoto watatu wa mzee Mwakalindile. Sina mke sijawahi kuoa na wala sina mpango wa kuoa kwa sasa, kwani sina hela ya kuoa natafuta pesa kwanza.
Filamu alizoshiriki Isarito ni Bunji, Jua Kali, Mpango Mbaya, Mlinzi, Sheikh Issa, Obambo ambayo ilimpatia tuzo za Africa Magic Viewers Choice mwaka 2022 na nyingine nyingi.