Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hii ndiyo sababu Diamond, Zuchu kuishi nyumba tofauti

DIAMOND Pict


Mume yuko Mbezi Beach, mke naye yuko Mbezi Beach, lakini kila mmoja ana nyumba yake!


Hiyo ndiyo stori inayozua gumzo kuhusu mastaa wa Bongo Fleva, Diamond Platnumz na Zuchu, ambao licha ya kufunga ndoa, wanatajwa kuishi katika nyumba tofauti ndani ya eneo hilo hilo.

Jambo hilo limeibua maswali kwa watu wanaofuatilia maisha ya mastaa hao, huku wengi wakijiuliza kwa nini baada ya kufunga ndoa wawili hao hawajaamua kuishi chini ya paa moja.

DIAMO 01

Kwa upande mmoja, wapo wanaoona kuwa kwa kuwa ni wanandoa, wanapaswa kuishi pamoja. Kwa upande mwingine, wapo wanaosema namna wanandoa wanavyoendesha maisha yao ni uamuzi wao, ilimradi wanaelewana.

Lakini katika ndoa ya Kiislamu, je, kuishi nyumba moja ni lazima?

Jambo hilo limekuwa likiwafanya baadhi ya watu kuanza kutengeneza tafsiri zao kuhusu maisha ya wawili hao.

Wengine wameanza kujiuliza kama kuna sababu maalumu inayowafanya waishi hivyo, wakati wengine wanaona huenda huo ukawa ni mpangilio wao wa kawaida wa maisha ambao hauhusiani na matatizo yoyote ya ndoa.

Kwa Diamond na Zuchu, hata hivyo, Zuchu aliwahi kuliambia Mwanaspoti kuwa kuishi tofauti ni uamuzi ambao wameufanya wenyewe na kwamba tofauti hiyo haitokani na ugomvi, kutengana au mgogoro wa kindoa.

DIAMO 04

Kwa hiyo, si sahihi kuichukulia hali hiyo kama ushahidi kwamba ndoa yao ina tatizo.

Kinachojulikana ni kwamba kila mmoja ana nyumba yake, huku wote wakitajwa kuwa Mbezi Beach.

Lakini je, kwa mujibu wa dini, wanandoa lazima waishi nyumba moja?


SHEIKH ATHUMAN IDD AFUNGUKA

Ili kupata jibu la suala hilo, Mwanaspoti limezungumza na Sheikh Athuman Idd, ambaye ameeleza kuwa katika Uislamu, kuishi nyumba moja si sharti la uhalali wa ndoa.

DIAMO 02

“Katika Uislamu, kuishi nyumba moja sio sharti la usahihi wa ndoa na hakuna kifungu kwenye Uislamu kinacholazimisha hilo.

“Wanandoa wakielewana na kuridhiana kwa hiari yao kila mmoja kuishi kwake kwa sababu yoyote ile, ndoa yao inabaki kuwa halali 100%, na wanaendelea kuwa mume na mke halali mbele ya Mwenyezi Mungu na jamii,” anasema Sheikh Athuman.

DIAMO 05

Kwa maelezo hayo, Sheikh anasema wanandoa wanaweza kuamua kuwa na makazi tofauti iwapo uamuzi huo umefanywa kwa makubaliano yao wenyewe.


Hivyo, suala la Diamond na Zuchu kuwa na nyumba tofauti haliwezi peke yake kuwa sababu ya kusema ndoa yao imevunjika au ina tatizo.

Muhimu ni makubaliano yaliyopo baina yao na namna wanavyotekeleza majukumu yao kama wanandoa.


Hilo linatoa picha kwamba, kwa upande wa dini, nyumba mbili si lazima zimaanishe ndoa mbili.

DIAMO 03

TUJIKUMBUSHE NDOA ILIVYOFUNGWA

Kwa kumbukumbu, Diamond Platnumz na Zuchu walifunga ndoa ya Kiislamu kwa siri Januari 2025.

Uthibitisho wa ndoa hiyo uliwekwa wazi zaidi Juni 2025 baada ya aliyewahi kuwa Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Walid Kawambwa, kusema ndiye aliyewafungisha ndoa hiyo.

Juni 3, 2025, Sheikh Walid alieleza kuwa alikuwa amewafungisha Diamond na Zuchu ndoa hiyo miezi mitano iliyopita, jambo linaloielekeza kwenye Januari 2025.

DIAMO 06

Baada ya taarifa hizo kuanza kuenea, Diamond aliweka hadharani picha na video zinazohusishwa na tukio hilo, huku Zuchu naye akithibitisha hadharani kuwa ni mke wa Diamond.

Hivyo, kinachozua mjadala sasa si kama Diamond na Zuchu ni wanandoa.

Wao wenyewe na viongozi wa dini waliowafungisha ndoa hiyo wamewahi kuweka wazi hilo.

Kinachowafanya watu wageuke na kuangalia upande mwingine ni namna wanavyoishi baada ya ndoa hiyo, kwa kuwa kila mmoja ana nyumba yake, licha ya wote kutajwa kuwa wanaishi Mbezi Beach.