Diamond afunika tuzo EAEA2026
Muktasari:
- EAEA ni tuzo za Tanzania zinazolenga kutambua mafanikio ya wasanii na wadau wa sekta ya burudani na sanaa. Washindi hupatikana kupitia kura zinazopigwa kwenye tovuti ya tuzo hizo.
DIAMOND Platnumz ameibuka miongoni mwa washindi wakubwa wa Tuzo za Entertainment & Arts Excellence Awards (EAEA) Tanzania 2026 baada ya kutwaa tuzo nne, huku mastaa wengine wa muziki wa Bongo Fleva, akiwamo Zuchu, Nandy, Rayvanny, Jux na Marioo, nao wakiondoka na tuzo.
Diamond alitwaa tuzo ya Mtumbuizaji Bora wa Burudani wa Mwaka, Msanii Bora wa Kiume, Mtumbuizaji Bora wa Kiume na Video Bora ya Muziki kupitia wimbo wa Natulizana alioufanya na mwongozaji wa video, Director Joma.
EAEA ni tuzo za Tanzania zinazolenga kutambua mafanikio ya wasanii na wadau wa sekta ya burudani na sanaa. Washindi hupatikana kupitia kura zinazopigwa kwenye tovuti ya tuzo hizo.
Katika vipengele vya wasanii wa kike, Abigail Chams alitwaa tuzo ya Msanii Bora wa Kike wa Mwaka na Mwimbaji Bora wa Mwaka, huku Nandy akishinda tuzo ya Mtumbuizaji Bora wa Kike.
Zuchu naye alishinda tuzo ya Wimbo Bora wa Singeli-Fusion kupitia Bado Nakupenda, huku akishirikiana na D Voice kutwaa tuzo ya Wimbo Bora wa Afro-Pop kupitia Baridi.
Rayvanny aliingia kwenye orodha ya washindi kupitia wimbo Toto, alioufanya na Calad, uliotwaa tuzo ya Wimbo Bora wa Bongo Fleva-Fusion. Pia alitambuliwa kupitia ushirikiano wa kimataifa katika wimbo Champions-Fi Kol Makan, uliowahusisha Nora Fatehi na Sanjoy.
Kwa upande wa muziki wa injili na nyimbo za uhamasishaji, Nandy alishinda tuzo ya Wimbo Bora wa Injili au Uhamasishaji kupitia wimbo wake Asante. MwanaFA naye alitwaa tuzo ya Wimbo Bora wa Rap-Fusion kupitia Baraka Nyingi.
Marioo alishinda tuzo ya Albamu au EP Bora ya Mwaka kupitia kazi yake MMMCXII, huku Alikiba na Mbosso wakitwaa tuzo ya Ushirikiano Bora wa Muziki Tanzania kupitia wimbo Bhuju.
Kwa upande wa wasanii wanaochipukia, Kusslove alishinda tuzo ya Msanii Bora Anayeibukia. Criss MJ alitwaa tuzo ya Msanii Bora wa Mwaka kutoka Diaspora, huku DJ Ally B akishinda tuzo ya DJ na Mtumbuizaji Bora wa Mwaka.
Sekta ya vichekesho na utengenezaji wa maudhui nayo ilipata nafasi katika tuzo hizo. Mama Mawigi alishinda tuzo ya Chapa Bora ya Vichekesho, huku Kiredio akitwaa tuzo ya Mtengeneza Maudhui Bora wa Mwaka.
Katika sekta ya mitindo na biashara, Juma Jux alishinda tuzo ya Chapa au Mjasiriamali Bora wa Mitindo kupitia African Boy, huku Hamisa Mobetto akitwaa tuzo ya Balozi Bora wa Chapa au Mshawishi wa Mwaka. Pinela Justine alishinda tuzo ya Mwanamitindo Bora wa Mwaka.
Washindi wengine ni MC Gara B, aliyetwaa tuzo ya Mtangazaji Bora wa Matukio wa Mwaka, na Noel Mangoma, aliyeshinda tuzo ya Meneja Bora wa Chapa.
Kwa kutwaa tuzo nne, Diamond amekuwa miongoni mwa majina yaliyojitokeza zaidi katika matokeo ya EAEA Tanzania 2026. Tuzo hizo pia zimetambua mchango wa wadau wengine wa burudani, wakiwemo watayarishaji, waongozaji wa video, watengeneza maudhui na wajasiriamali wa sekta hiyo.