Diamond atwaa tuzo ya ushawishi Afrika
Muktasari:
- Mchanganyiko huo wa muziki na biashara umekuwa sehemu ya safari yake ya kujitanua, huku ushirikiano na wasanii wengine ukiendelea kuwa nyenzo muhimu katika kupanua muziki wa Bongo Fleva.
SUPASTAA wa Bongo Fleva Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ ameendelea kuimarisha nafasi yake kwenye ramani ya burudani ya Afrika baada ya kutajwa mshindi wa tuzo ya Top African Celebrity of the Year 2026.
Awali kabla ya tuzo hiyo Diamond alikuwa ameshatwaa tuzo nyingine ya kolabo yake na Juma Jux.
Top African Celebrity imekuwa ikifanya kazi na wasanii wakubwa duniani wakiwemo Davido, Ne-Yo, Omarion, na Alicia Keys, huku rekodi ikionyesha huyu ni msanii wa kwanza kuchukua tuzo hiyo.
Diamond, ambaye ni kiongozi wa lebo ya WCB Wasafi ametajwa kutwaa tuzo hiyo ya Africa Golden Awards 2026, inayohusishwa na ushawishi wa watu mashuhuri barani Afrika.
Mafanikio hayo yanaongeza uzito wa jina lake katika tasnia ya burudani ambako amejijengea nafasi kupitia muziki, biashara na shughuli mbalimbali zinazomfanya kuendelea kuwa miongoni mwa majina yanayofuatiliwa kwa karibu zaidi na mashabiki.
Kwa miaka kadhaa, Diamond ambaye hadi sasa ana albamu nne amekuwa akitumia muziki wake kujitanua nje ya Tanzania akishirikiana na wasanii wa mataifa mbalimbali wakiwemo Koffi Olomide, Rick Ross, Morgan Heritage, Tiwa Savage, Ne Yo, Davido pamoja na Kundi la P-Square na kushiriki katika miradi inayolenga kufikisha Bongo Fleva kwenye masoko mapana zaidi.
Katika tuzo hiyo, jina lake linaendelea kuhusishwa na mjadala wa ushawishi wa wasanii wa Afrika hasa katika kipindi ambacho muziki wa Afrika unazidi kupata nafasi kwenye majukwaa ya kimataifa.
JOY YAMPA TUZO
Kama hiyo haitoshi, Diamond ambaye ni msanii maarufu zaidi nchini ameendelea kuonekana kwenye orodha ya washindi wa tuzo za kimataifa kupitia wimbo wa Joy, aliomshirikisha Juma Jux alipokea tuzo ya Best Collaboration katika African Muzik Magazine Awards (AFRIMMA) 2026, zilizofanyika Dallas, Texas, Marekani, hadi sasa ikiwa imepita miezi sita wimbo huo kwenye mtandao wa You Tube umetazamwa na watu milioni 19.
Ushindi huo umeongeza heshima kwa wawili hao ambao wameunganisha nguvu zao katika kazi inayowakutanisha wasanii wawili wa Tanzania wenye mashabiki wengi.
Kolabo hiyo pia inaonyesha umuhimu wa ushirikiano katika tasnia ya muziki ambako wasanii wanaweza kubadilishana mashabiki na kuongeza usikivu wa kazi zao kupitia mitandao na majukwaa mbalimbali.
DIAMOND NA NGUVU YA USHAWISHI
Mbali na mafanikio yake ya kimuziki, Diamond ambaye yupo kwenye tasnia ya muziki kwa zaidi ya miaka 16 huku wimbo wake wa kwanza ukiwa Kamwambie uliotoka mwaka 2010, amejenga jina kutokana na shughuli za kibiashara na uwekezaji katika sekta ya burudani, zikiwamo shughuli zinazohusishwa na WCB Wasafi.
Mchanganyiko huo wa muziki na biashara umekuwa sehemu ya safari yake ya kujitanua, huku ushirikiano na wasanii wengine ukiendelea kuwa nyenzo muhimu katika kupanua muziki wa Bongo Fleva.