Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Billnass, Nandy katika dunia ya Jay-Z na Beyonce

MWANDISHI Zack O’Malley Greenburg katika kitabu chake cha Empire State of Mind; How Jay-Z Went from Street Corner to Corner Office (2011) (Himaya ya Fikra; Namna Jay-Z Alivyotoka Mtaani Hadi Ofisini), ameeleza megi kuhusu rapa Jay Z na familia yake.

Moja ya mambo aliyoeleza Greenburg ni jinsi ndoa ya Shawn Carter ‘Jay-Z’, 54, na Beyonce Knowles, 42, iliyofungwa mwaka 2008 inavyovutia zaidi kampuni, taasisi na mashirika kuwekeza au kufanya nao kazi kitu kinachowapatia fedha nyingi nje ya muziki.

Anasema ni watu waliopatana vizuri, kama Beyonce ataonekana kwenye runinga akifurahia bidhaa fulani, ni wazi Jay-Z naye anaipenda, na hilo linaweza kuwa na athari chanya katika soko na ndicho hasa kampuni nyingi zinatarajia wanapofanya nao kazi.

Utakumbuka Jay-Z na Beyonce ambao wamejaliwa watoto watatu Blue Ivy Carter (2012) na mapacha Rumi na Sir Carter (2017), ndio wanandoa mastaa tajiri zaidi duniani. Kwa pamoja utajiri wao unafikia zaidi ya Dola3 bilioni (takriban Sh7.5 trilioni).

Mastaa wa Bongofleva, Billnass na Nandy wamekuwa wakifananishwa na Jay-Z na Beyonce kwa namna walivyoweka maisha yao ya muziki, biashara, uhusiano hadi ndoa iliyofungwa Julai 2022 katika kanisa la KKKT Mbezi Beach, Dar es Salaam.

William Lyimo ‘Billnass’ (29) na Faustina Mfinanga ‘Nandy’ (30) kwa mara ya kwanza walikutana 2016 katika Chuo cha Biashara (CBE) Dar es Salaam ambapo walikuwa wanasoma, lakini uhusiano rasmi ulikuja kuanza kwenye Tamasha la Fiesta mkoani Mbeya.

Kama ni akili ya utafutaji fedha, basi Billnass na Nandy ni pacha waliokutana kuanzia jinsi wanavyotoa nyimbo, kuandaa shoo na matukio ya burudani ni wazi wanajua jinsi hii biashara inavyokwenda. Kwa kifupi wanaujua mchezo na wanaucheza kwa kanuni zao.

Mathalan wakati Billnass anatoa video ya wimbo wake wa mwisho, Maokoto (2023) ft. Marioo aliandaa shoo kwa ajili ya uzinduzi wa video hiyo na watu wakalipa viingilio kushuhudua tukio hilo ambalo alitumbuiza pia. Ni wasanii wachache wanaofanya hivi kwa sasa.

Kwa upande wake Nandy ana tamasha lake ‘Nandy Festival’ ambalo kwa misimu zaidi ya minne ameliendesha kwa mafanikio.Anatoa fursa za kazi kwa wasanii wenzake, na mumewe Billnass ni miongoni mwa wasanii waliowahi kutumbuiza.

Na katika muziki wameshirikiana katika nyimbo nne Bugana (2019), Do Me (2020), Party (2021) na Bye (2022). Kuanzia 2019 kila mwaka wamekuwa wakitoa wimbo mmoja wa ushirikiano. Ndivyo walivyoamua kuipangilia biashara yao.

Ikumbukwe Nandy ndiye aliingiza sauti za chini (back vocal) katika wimbo wa Billnass ‘Sina Jambo’ (2017) uliotoka kipindi tetesi za kuwa wapo pamoja kiuhusiano zimeshika kasi katika mitandao ya kijamii. 

Kila mmoja ana biashara zake moja au mbili anazojishughulisha nazo. Nandy ana lebo yake ya muziki, The African Princess, anauza bidhaa zake za lipstick na ana kampuni inayohudumia maharusi, huku Billnass akiuza bidhaa za kieletroniki hasa simu janja.

Agosti 2022 ndipo walijaliwa mtoto wao wa kwanza, Kenaya (Naya Bill). Waliamua kumficha mtoto huyo mbele ya mitandao ya kijamii hadi alipotimiza umri wa mwaka mmoja, Agosti 2023 ndipo sura yake ikaonekana mtandaoni kwa mara ya kwanza.

Basi Nandy na Billnass walipotambulisha ukurasa rasmi wa Naya kwa mashabiki wao katika mtandao wa Instagram, ndani ya siku moja tu uliweza kupata wafuasi (followers) zaidi 100,000 na sasa wamefikia zaidi ya 170,000.

Utakumbuka Nandy ni miongoni mwa wanamuziki 10 Tanzania wenye wafuasi wengi Instagram akiwa nao milioni tisa, huku Diamond Platnumz akiwa anaongoza kwa wafuasi akiwa nao milioni 16.6, kisha Hamisa Mobetto (10.5) na Shilole (10.1).

Na muda mfupi baadaye Nandy alisema mtoto wake, Naya amepata dili sita za ubalozi ambazo atakuwa anazitangaza katika ukurasa wake wa Instagram na sasa tayari anafanya hivyo. Mara nyingi anatangaza bidhaa kwa ajili ya watoto.

Huyu ni mtoto wa mwaka mmoja tayari wamemtengenezea mazingira ya yeye pia kuingiza fedha. Ni wazi hilo linaonekana kuwa rahisi kutokana na nguvu ya ushawishi waliyonayo wazazi wake katika jamii.

Wamevunja ile dhana kuwa wasanii wakioa au kuolewa ushawishi wao unapungua. Billnass hakuwahi kushinda tuzo hadi pale alipofunga ndoa na Nandy ndipo akashinda tuzo ya kwanza ya Muziki Tanzania (TMA 2022) kama Msanii Bora wa Hip Hop.

Ni kama ilivyo kwa Jay-Z na Beyonce, mafanikio makubwa kibiashara waliyapata baada ya ndoa yao. Hii ina maana ushawishi uliongezeka, Jay-Z alifikia hadhi ya ubilionea miaka 11 baada ya ndoa.

Ikumbukwe ziara yao ya mwisho “On the Run II Tour” iliyoanza Juni 6, 2018 hadi Oktoba 4, 2018 huko Ulaya na Amerika Kaskazini ambapo walitumbuiza shoo 48 mbele ya mashabiki milioni 2.1, walilipwa Dola 254.5 milioni (takriban Sh636.3 bilioni).