Diamond, Zuchu mambo yameisha
Muktasari:
- Julai 12, Zuchu aliwashangaza mashabiki alipoweka ujumbe kwenye mitandao ya kijamii akisema yeye na Diamond wametengana na wanaendelea na mchakato wa talaka baada ya kuwa pamoja kwa miaka sita.
KAMA kuna stori iliyotikisa Burudani wiki hii, basi ni ile ya Zuchu na Diamond Platnumz. Ilianza kwa kauli nzito ya Zuchu kuhusu kutengana na mumewe na kuendelea na mchakato wa talaka, lakini wiki chache baadaye sura ya stori imebadilika baada ya wawili hao kuonekana pamoja katika hafla ya baby shower ya mtoto wao anayetarajiwa kuzaliwa.
Julai 12, Zuchu aliwashangaza mashabiki alipoweka ujumbe kwenye mitandao ya kijamii akisema yeye na Diamond wametengana na wanaendelea na mchakato wa talaka baada ya kuwa pamoja kwa miaka sita.
Zuchu alisema uamuzi huo haukuwa rahisi, lakini ameamua kuchagua, kuangalia afya yake na kuendelea na kazi zake za muziki pia alimtakia Diamond na familia yake kila la heri.
Kilichoongeza uzito wa stori hiyo ni Zuchu hakutaja sababu ya moja kwa moja iliyomfanya kufikia uamuzi huo.
Hata hivyo, kulikuwa na madai mbalimbali yaliyoibuka kuhusu changamoto ndani ya uhusiano wao, yakiwamo madai ya kutokuwa na uaminifu na sintofahamu zinazodaiwa kuhusisha familia.
Lakini madai hayo hayakuthibitishwa na Zuchu wala Diamond, hivyo hayawezi kuchukuliwa kama sababu rasmi ya kuvunjika kwa ndoa yao.
Lakini sasa mambo yanaoneka kuwa tofauti baada ya jana usiku, Julai 31, Zuchu kufanya baby shower nyumbani kwake Mbezi Beach, ikiwa ni hafla ya ujio wa mtoto wake na Diamond.
Katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na mastaa kibao akiwemo Barnaba Classic, Chinno Wanaman, Yammi, Lamata Leah na kundi lake na wengineo.
Mwanzoni mwa hafla hiyo Diamond hakuwepo kabisa lakini alikuja katikati kama sapraizi akiwa ameongozana na ndugu zake wawili, Ricardo Momo na Iddy Santos.
Zuchu hakuficha furaha yake kwa kumuona baba wa mtoto wake akishiriki katika siku hiyo muhimu.
“Kipekee namshukuru baba mtoto kwa kuja, imenifanya siku yangu imekuwa nzuri sana,” alisema Zuchu.
Diamond naye akatumia nafasi hiyo kuzungumza kwa lugha iliyotoa picha tofauti na ile iliyokuwa imesambaa kwenye mitandao ya kijamii.
Alisema anampenda Zuchu, akakiri katika maisha ya wawili kugombana na kukwazana ni sehemu ya safari, huku akisisitiza mwishowe yeye na Zuchu bado ni watu waliounganishwa na maisha yao.
Pia alimuomba Zuchu msamaha kwa sehemu yoyote ambayo alihisi amemkwaza na akamtakia uzao mwema.
"Zuuh nimwambie kwanza nampenda sana anajua lakini pia katika maisha ya wawili kugombana kupo mtakwazana, lakini kitu cha tofauti ni kwamba kwenye ugomvi lazima mlikuwa mmependana," alisema Diamond
"Kipenzi changu Zuchu nakupenda sana lakini nimshukuru sana uamuzi wa kubeba mimba ni mgumu sana hususani kwa msanii anayeimba yaani hapa maana yake hapa hawezi kutoa kazi zake kuzifanya kwa hiyo nakupenda nakushuru na nakuthamini nakupenda sana baby," alimalizia kusema Diamond
Zaidi ya hapo, Diamond alifunguka kuhusu furaha yake baada ya kujua mtoto anayetarajiwa ni wa kike. Alisema hakutaka kujua jinsia ya mtoto mapema kwa sababu alitaka iwe mshangao, lakini aliposikia kuwa ni mtoto wa kike alifurahi sana.
Pia alizungumzia ndoto yake ya kuwa na familia kubwa yenye watoto wasiopungua wanne, yenye baraka na upendo. Kauli hiyo imeongeza maswali mapya kuhusu mustakabali wa uhusiano wake na Zuchu baada ya tangazo la talaka.
FAMILIA YA DIAMOND
Katika baby shower hiyo, familia ya Diamond iliwakilishwa na ndugu zake wawili wa kiume, Ricardo Momo na Iddy Santos. Lakini kutokuwepo kwa Mama Dangote na dada yake Esma Platnumz kumezidi kuzua maswali miongoni mwa mashabiki.
Kutokuwepo kwao kwenye hafla hiyo kumeibua maswali, hasa kwa sababu tayari kumekuwa na mjadala kwa muda kuhusu uhusiano wa Zuchu na baadhi ya watu wa familia ya Diamond. Hata hivyo, hakuna kauli iliyotolewa na Mama Dangote au Esma inayosema kwa nini hawakuhudhuria.
Jambo jingine lililogusa mashabiki ni kwamba, licha ya pongezi nyingi kusambaa kwenye mitandao baada ya taarifa za ujio wa mtoto huyo wa kike, hadi wakati wa kuandikwa kwa habari hii hakuna ujumbe wa kutoka kwa Mama Dangote au Esma wa kumpongeza Zuchu na Diamond.
DIAMOND
Mtoto wa Zuchu na Diamond atakuwa sehemu ya familia kubwa ya msanii huyo. Diamond tayari ana watoto wengine, wakiwamo Tiffah na Prince Nillan aliowapata na mfanyabiashara Zari Hassan, pamoja na Naseeb Junior anayezaa na Tanasha Donna. Watoto hao wanaishi nje ya Tanzania.
Kwa hiyo, mtoto anayetarajiwa na Zuchu atakuwa sura nyingine katika familia ya Diamond, huku kauli yake ya kutamani kuwa na watoto wasiopungua wanne ikionyesha namna anavyoutazama upande wa familia yake kwa sasa.
TALAKA ITAKUWAJE?
Julai 12, Zuchu alisema wazi yeye na Diamond wametengana na wako katika mchakato wa talaka. Hakusema wamegombana kwa sababu gani, wala hakufafanua kama kulikuwa na jambo moja maalumu lililosababisha uamuzi huo.
Sasa, baada ya kuonekana pamoja kwenye baby shower, mashabiki wamebaki na maswali mengi kuliko majibu. Je, hii ni dalili ya wawili hao kurejea pamoja? Je, wanaamua tu kuweka tofauti zao pembeni kwa ajili ya mtoto? Au mchakato wa talaka bado unaendelea licha ya kushirikiana katika masuala ya mtoto?
Lakini kwa kile kilichoonekana kwenye hafla hiyo ni wazi mambo yameisha na wawili hao watakuwa pamoja kwenye safari yao ya penzi.
Ukitazama zile video zinazosambaa mitandaoni na zile kauli za msamaha wa Diamond kwa Zuchu zinaonyesha kabisa hakuna mambo ya talaka tena wote wawili wameridhiana.