Kutoka Miss Tanzania hadi malkia wa Afrika, safari ya Tracy Nabukeera
Muktasari:
- Nabukeera, ambaye aliwakilisha Tanzania katika mashindano hayo ya kimataifa, alitwaa taji hilo baada ya kufanya vizuri katika kilele cha mashindano yaliyofanyika Julai 31, mjini Nowy Sącz, Poland, yakishirikisha warembo 67 kutoka mataifa mbalimbali duniani.
MWANAMITINDO wa Tanzania, Tracy Nabukeera ameandika historia baada ya kutwaa taji la Miss Supranational Africa 2026 ikiwa ni mara yake ya kwanza kushiriki mashindano hayo yaliyofanyika nchini Poland.
Nabukeera, ambaye aliwakilisha Tanzania katika mashindano hayo ya kimataifa, alitwaa taji hilo baada ya kufanya vizuri katika kilele cha mashindano yaliyofanyika Julai 31, mjini Nowy Sącz, Poland, yakishirikisha warembo 67 kutoka mataifa mbalimbali duniani.
Taji la Miss Supranational 2026 lilinyakuliwa na Katrina Llegado wa Ufilipino.Nabukeera sasa anaingia kwenye orodha ya Watanzania waliofanikiwa kupata nafasi ya kutwaa taji katika mashindano ya kimataifa ya urembo.
Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi wa taji la Afrika, mrembo huyo alisema anajivunia kubeba bendera ya Tanzania na kuwakilisha nchi yake, huku akiwashukuru Watanzania waliomuunga mkono katika safari yake.
“Tanzania tumefanya tena. Ningependa kuwashukuru wote walionisapoti katika safari hii. Asante sana, sana, sana. Ni heshima kubwa kubeba bendera ya Tanzania mabegani mwangu na kuiwakilisha nchi yangu katika Miss Supranational,” alisema Nabukeera
Tracy, ambaye aliandika historia ya kuwa mwakilishi wa kwanza wa Tanzania katika Miss Supranational, alisema ushindi huo ni baraka kubwa kwake na hatua muhimu kwa tasnia ya urembo nchini.
“Ni heshima kubwa kuwa mwakilishi wa kwanza wa Tanzania na kushinda taji kubwa kama hili. Ninajivunia nchi yangu na ninawashukuru Watanzania wote ambao wamekuwa nami tangu mwanzo hadi mwisho wa safari hii. Asante sana kwa kuniamini,” alisema.
Baada ya ushindi huo, Tracy amesema anatarajia kutumia nafasi hiyo kuitangaza Tanzania kimataifa, hususan kupitia utalii, utamaduni na sekta ya ubunifu.
Nabukeera anatarajiwa kurejea nchini Tanzania usiku wa kuamkia Jumatatu, Agosti 3, saa 8:15 usiku kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam.
Kabla ya kuwakilisha Tanzania katika Miss Supranational, Tracy alikuwa Miss Tanzania 2024, taji lililomfungulia milango ya kuendelea kuiwakilisha nchi katika majukwaa ya kimataifa.