Arnelisa wa Ben Pol hatari!

Friday January 01 2021
BEN PIC
By Kelvin Kagambo

HATIMAYE ile ‘couple’ iliyokuwa ikivuruga akili za watu kwenye mitandao ya kijamii imeibuka na kuweka wazi mambo yote yaliyokuwa yanatatiza mashabiki kuhusu familia yao; hapa tunamzungumzia mwimbaji Ben Pol na mkewe mfanyabiashara kutoka Kenya, Arnelisa Muigai.

Mwanaspoti imefanya mahojiano na Arnelisa akiwa pembeni ya mume wake, ambapo ameweka wazi mambo mengi kuhusu mume wake, ndoa yao, kuachana kwao na mastori kibao; shuka nayo taratibu.

NDOA YAO ILIVYOFUNGWA

Taarifa za wawili hao kufunga ndoa ziliteka umakini wa mashabiki mwezi Oktoba baada ya picha yao wakiwa kanisani ndani ya suti na shela kusambaa kwenye mitandao ya kijamii.

Lakini kupitia eksiklusivu hii, wawili hao wamefichua kuwa ndoa yao ilifungwa mwezi wa tano, tena ni hapa hapa Tanzania, tofauti na watu wengi walivyokuwa wakidhani awali kuwa ilifungiwa nchini Kenya.

“Tulifunga mwezi wa tano, hapa hapa Tanzania, Mbezi Dar es Salaam” ameeleza Ben Pol.

Advertisement

Wakijibu kwanini waliamua kuachia picha miezi mitano baada ya ndoa kufangwa wanasema, ndoa ni kitu cha kifamilia zaidi kwahiyo hawakuona sababu za kuanika kila wazi.

“Watu wetu wa karibu walikuwa wanafahamu. Na hata baada ya kanisani tulijumuika nao kwa ajili ya chakula na vitu vingine. Sisi tunadhani ndoa ni kitu cha kifamilia ziadi.” anasema.

MAISHA YA NDOA

Walipoombwa waelezee maisha yao ya ndoa, Ben Pol amesema kwake anachukulia ni kitu cha kawaida tu, haoni tofauti na namna walivyokuwa wakiishi kabla ya kufunga ndoa. Lakini Arnelisa akaitolea ufafanuzi zaidi.

“Ni kawaida tu, iko kama zamani, hakijabadilika kitu. Unajua kama watu mkiwa marafiki kabla ya ndoa, hata mnapofunga ndoa inakuwa ni kama mmefungua ukurasa mpya tu wa kitabu, wahusika mnabaki kuwa wale wale, kwahiyo hakuna kinachobadilika.” amesema Arnelisa.

SKENDO YA KUACHANA

Siku chache baada ya picha za harusi kusambaa ikaibuka skendo kwamba wawili hao washamwagana. Mwandishi wa Jiachie akataka kufahamu, ilikuwaje? Ni kweli walipeana likizo kidogo kisha wakarudiana, au ilikuwa ni skendo tu?

Arnelisa amefunguka kuwa yeye na Ben hawakuwahi kuachana wala kupeana likizo hata siku moja tangu wameanza mahusiano, isipokuwa kilichokuwa kinaendelea ilikuwa ni maneno ya kutengenezwa na watu wasiowajua vizuri wao na penzi lao kwa ujumla.

“Haikuwa kweli, lakini hata hivyo sisi huwa hatuweki umakini kwenye maneno ya namna hiyo. Yakisemwa tunaacha yasemwe, hata hatusikilizi,” anaeleza Arnelisa.

WATOTO WATATU TU

Ben Pol mwenyewe anakwambia ukiona watu wameoana elewa kwamba kinachofuata ni watoto. Wakijibu swali la tutarajie baraka ya watoto wangapi kutoka kwenye ndoa yao, Arnelisa amesema yeye anatamani kupata watoto watatu kutoka kwa Ben Pol.

“Mimi ningependa kupata watoto watatu, tumezungumza na wote tumependa iwe hivyo,” anasema Arnelisa.

“Ben Pol ambaye wakati wote wa mahojiano alikuwa pembeni ya mkewe alimtania kwamba anataoa siri za familia, kisha akakiri kilichosemwa na mkewe na kuongeza kuwa hiyo ni matamanio yao lakini mengine yatakayotokea ikiwa vitaendana na mipango ya Mungu.

“Ni kweli, tunapenda kupata watoto watatu pamoja. Lakini hiyo ni mimpango yetu, kama Mungu atapenda iwe hivyo itakuwa shwari,” anasema Ben.

BEN KUPAKA RANGI

Hii sasa ndiyo kali! Kama na wewe ulikuwa ni mmoja wa watu waliokwazika baada ya Ben Pol kupost picha akionekana amepaka rangi kwenye kucha zake, nakushauri kunywa maji utulie tu, kwanini? Kwa sababu mwenye mume amesema kwake yeye ni poa na alimpeleka mpaka saluni wanapopaka rangi.

Akisimulia ishu nzima ilivyokuwa Arnelisa anasema siku hiyo yeye na Ben walikwenda saluni kwa ajili ya Spa, walipofika huko, yeye na mume wake walikuwa wanatengeneza kucha, kwahiyo Ben alipomuona mkewe anapaka rangi kucha naye akapa wazo la kupaka pia.

“Akasema nikipaka nitapendeza, nikamwambia ndiyo. Ndiyo akapaka rangi Bendera ya Tanzania,” anasema Arnelisa.

Anaongeza kuwa kwake haoni tatizo kwa sababu kupaka rangi ni kama urembo mwingine ambao umekuwa ni kawaida kwa vijana wa kiume kuutumia, urembo kama vile kuvaa hereni, kusuka na kadhalika.

BEN ANAPIKISHWA JAMANI

Arnelisa anakiri kwamba Ben Pol ni mwanaume sahihi zaidi kwake kama ambavyo alikuwa akimtarajia kabla hawajawa wapenzi. Na ili kuthibitisha hilo anakwambia wakiwa nyumbani Ben Pol anamsaidia mpaka kupika.

“Alikuwa hajui kupika chakula kabisa lakini amejifunza na anaweza kwa sasa. Hata hivyo nikiwa jikoni ananisaidia sana, utakuta anakata vitunguu. Na hata kama tukiwa na wageni yeye mimi nikiwa bize jikoni yeye ananisaidia kuandaa kwa ajili ya wageni,” anasema.

KUCHUNWA NA BEN

Moja ya mashambulizi makubwa dhidi ya Ben Pol na mpenzi wake ilikuwa ni kwamba eti Ben Pol yupo na Arnelisa kwa ajili ya kumchuna mwanamke huyo. Hata hivyo hilo limepanguliwa na Ben Pol mwenyewe pamoja na Arnelisa.

Ben Pol anasema yeye yupo kama wanaume wengi, kwamba wanapenda mwanamke mzuri lakini pia anayejituma pia. Na hata hivyo, kabla hata hajawa na Arnelisa alikuwa na maisha yake yanayoridhisha.

“Niambie mwanaume gani hapendi mwanamke anayejituma? Hizo zingine ni maneno ya watu wasiotujua. Mimi niwashauri wanawake, wakati wanapambana kuwa wazuri, pia wapambane kufanya kazi. Wanaume tunapenda wanawake wa aina hiyo,” anasema.

Wakati Arnelisa yeye anateta kwamba kinachosemwa ni maneno ya watu wasiomjua yeye wala Ben Pol.

“Ben anafanya muziki na unamlipa, ana bendi, pia ni mfanyabiashara na mkulima, analima zabibu na mboga mboga lakini pia hivi karibuni atatangaza product yake. Kwahiyo ni mtu anayejiweza sana, hana sababu ya kuja kunichuna.”

Advertisement