‘Ca Va Bien’ ya Twanga yazinduliwa, wakongwe waonyesha bado wamo
Muktasari:
- Twanga Pepeta walizindua albamu ya 16, Ca Va Bien, katika usiku uliojaa muziki, ubunifu na mashabiki waliojitokeza kushuhudia moja ya matukio makubwa ya muziki wa dansi mwaka huu.
KAMA kulikuwa na swali kuhusu nafasi ya Twanga Pepeta katika muziki wa dansi nchini, basi jana, Agosti 7, 2026, bendi hiyo ilitoa jibu lake ndani ya Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.
Twanga Pepeta walizindua albamu ya 16, Ca Va Bien, katika usiku uliojaa muziki, ubunifu na mashabiki waliojitokeza kushuhudia moja ya matukio makubwa ya muziki wa dansi mwaka huu.
Ukumbi wa Mlimani City ulijaa mashabiki, huku kila mmoja akiwa amekaa katika eneo linalolingana na tiketi aliyokata, na hali hiyo ilifanya tukio hilo kwenda kwa utulivu na wakati huohuo kuonyesha ukubwa wa bendi hiyo katika kuvuta mashabiki kwenye jukwaa kubwa.
UHAMIAJI, JKT MGAMBO WATOA SOMO
Katika hatua iliyotofautisha uzinduzi huo na maonyesho mengine ya muziki wa dansi, Twanga Pepeta hawakuchagua bendi maarufu za jijini Dar es Salaam kusindikiza onyesho lao.
Badala yake, waliwapa nafasi Uhamiaji Band ya Dar es Salaam na JKT Mgambo ya Tanga.
Uamuzi huo ulikuwa kama mtihani kwa bendi hizo ambazo si miongoni mwa majina yanayoonekana mara kwa mara katika maonyesho makubwa ya muziki wa dansi. Hata hivyo, zilijibu kwa vitendo.
Bendi hizo zilianza kutoa burudani majira ya saa 2 usiku na kuendelea hadi saa 4:24, zikiweka mazingira ya kutosha kabla ya Twanga Pepeta kuingia jukwaani.
Kwa kufanya hivyo, Twanga waliweka tofauti nyingine katika uzinduzi wao, wakionyesha kujiamini na pia kutoa nafasi kwa vipaji ambavyo si lazima viwe na majina makubwa ili kufanya vizuri kwenye jukwaa kubwa.
DAKIKA MOJA KWA WALIOTANGULIA
Kabla ya Twanga Pepeta kuingia jukwaani, kulifanyika tukio maalumu la kuwakumbuka wanamuziki wa bendi hiyo waliotangulia mbele ya haki.
Mashabiki na waliokuwapo ukumbini walisimama kwa dakika moja kuwaenzi, kabla ya waratibu wa tukio, Mhe. Asha Baraka na Steve Nyerere, kutoa maneno mafupi.
Kisha, saa 4:40 usiku, muda ambao wengi walikuwa wameusubiri, Twanga Pepeta wakapanda jukwaani.
CHAZ BABA, CHOKI, VICTOR WAFANYA UBUNIFU
Twanga hawakuingia na muziki pekee, bali pia walikuja na ubunifu katika mavazi na uchezaji.
Kiongozi wa bendi, Chaz Baba, alivutia alipopanda jukwaani akiwa amevalia vazi la Kinaijeria, huku baadhi ya waliokuwapo wakilitaja kama vazi la Congo. Mpiga kinanda Victor Nkambi naye alifanya yake, akionekana akiwa amevaa wigi fupi lenye mawimbi, mwonekano uliowafanya mashabiki kumuangalia zaidi wakati akiendelea kuonyesha uwezo wake kwenye kinanda.
Kwa upande wake, Ally Choki alikuwa amevalia suti na kofia, huku akiwa ameshika fimbo mkononi, akiongeza ladha nyingine kwenye onyesho hilo. Wacheza shoo wa kike nao hawakuwa nyuma. Walibadilisha mavazi mara tatu, huku kila vazi likiongeza mvuto wa jukwaa na kulifanya onyesho lionekane tofauti kila yalipobadilika.
‘CA VA BIEN' WAANZA NA MPYA
Twanga walipanga vizuri mpangilio wa nyimbo zao. Badala ya kukimbilia kwenye nyimbo zao kongwe, walianza na kazi mpya kutoka kwenye albamu hiyo ya 16.
Miongoni mwa nyimbo zilizopigwa ni Ca Va Bien, Dear X, Usikariri na Usinitoe Roho, kabla ya kuanza kushusha mzigo wa nyimbo zao za zamani.
Katika nyimbo hizo mpya, Usinitoe Roho ilionekana kuwa miongoni mwa zilizopokelewa vizuri na mashabiki, huku Ca Va Bien, uliobeba jina la albamu, ukifanya watu wengi kuingia kwenye mdundo.
Lakini kama kulikuwa na sehemu ambayo mashabiki walionyesha wazi kuwa bado wana kumbukumbu na Twanga, ilikuwa pale nyimbo za zamani zilipoanza.
‘PASSWORD' YAFUTA VITI
Password, Mwana Dar es Salaam, Walimwengu, Mmbeya, Mtu Pesa, Saudia Injinia, Aminata na Sumu ya Mapenzi zilipoanza kupigwa, eneo la kuchezea likabadilika na kuwa uwanja wa burudani.
Mashabiki waliinuka kwenye viti vyao na kuelekea mbele ya jukwaa, wakicheza na kuimba pamoja na waimbaji.
Hapo ndipo Twanga walipothibitisha kuwa, mbali na nyimbo mpya, bado wana hazina ya kazi za zamani zinazoweza kuamsha hisia za mashabiki na kuunganisha vizazi mbalimbali.
DANSI, TAARABU, SINGELI NA BONGOFLEVA
Uzinduzi huo haukuwa wa mashabiki wa muziki wa dansi pekee.
Mlimani City ilikutana na sura mbalimbali za tasnia ya burudani, huku wasanii kutoka muziki wa dansi, taarab, singeli na Bongo Fleva wakihudhuria.
Baadhi ya viongozi wa Simba na Yanga nao walionekana ndani ya ukumbi huo, wakishuhudia usiku ambao Twanga Pepeta walitumia kuonyesha ukubwa wao.
Kwa ujumla, uzinduzi wa Ca Va Bien ulikuwa zaidi ya kuzindua albamu mpya. Ulikuwa pia ujumbe wa Twanga Pepeta kwamba muziki wa dansi bado una nafasi kubwa katika burudani ya Tanzania na kwamba bendi yenye historia, ubunifu na mashabiki inaweza kuliteka jukwaa kubwa kama Mlimani City.
Na jana, Twanga Pepeta hawakusimulia ubabe wao kwa maneno; waliuonyesha kwa muziki.