Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kumbukumbu ya Banza Stone, miaka 11 bila ‘Mtaji wa Maskini’

BANZA Pict

Muktasari:

  • Banza Stone alikuwa na sauti ya kipekee, uwezo mkubwa wa kutunga mashairi na ujumbe wenye mafunzo. Nyimbo zake kama Mtaji wa Maskini, Kumekucha, Elimu ya Mjinga, Angurumapo Simba, Mtu Pesa, Falsafa ya Maisha na nyingine nyingi zilimjengea heshima kubwa katika tasnia ya muziki wa Tanzania. 

JULAI 17, 2026, ilikuwa imetimia miaka 11 tangu kufariki kwa mmoja wa waimbaji mahiri wa muziki wa dansi Tanzania, Ramadhani Masanja maarufu kama Banza Stone, ambaye alifariki dunia mwaka 2015 baada ya kuugua kwa muda mrefu. Ingawa amefariki miaka 11 iliyopita, lakini kazi zake bado zinaendelea kusikika kwenye redio, majukwaa ya kidijitali na katika nyoyo za mashabiki wa muziki wa dansi.

Banza Stone alikuwa na sauti ya kipekee, uwezo mkubwa wa kutunga mashairi na ujumbe wenye mafunzo. Nyimbo zake kama Mtaji wa Maskini, Kumekucha, Elimu ya Mjinga, Angurumapo Simba, Mtu Pesa, Falsafa ya Maisha na nyingine nyingi zilimjengea heshima kubwa katika tasnia ya muziki wa Tanzania. 


BANZ 01

SAFARI YAKE YA MUZIKI ILIANZIA UTOTONI 
Banza Stone alizaliwa Oktoba 20, 1972 jijini Dar es Salaam. Baada ya kumaliza elimu ya msingi, mapenzi yake kwa muziki yalimvutia kujiunga na vikundi mbalimbali vya burudani, ingawa wazazi wake mwanzoni hawakuunga mkono uamuzi huo.


Alianza kwa kujaribu muziki wa Hip Hop kabla ya kuamua kuelekeza nguvu zake katika muziki wa dansi. Pia alipata mafunzo ya muziki katika Jumba la Utamaduni la Korea, hatua iliyomsaidia kujenga taaluma yake ya muziki.


NJIA ALIZOPITA KABLA YA KUNG'ARA 
Kabla ya kuwa nyota mkubwa, Banza Stone alipitia bendi mbalimbali zikiwemo The Heart Strings, Twiga Band, Achigo Band, Afri-Swez, kabla ya kujiunga na Twanga Pepeta, ambako kipaji chake kilianza kutambulika kwa kiwango kikubwa.


Baadaye alijiunga na TOT Plus, akarudi tena Twanga Pepeta, kisha Extra Bongo, huku pia akianzisha bendi yake ya Bambino Sound, ambayo haikudumu kwa muda mrefu. Safari hiyo ilimjengea uzoefu mkubwa na kumfanya kuwa mmoja wa waimbaji waliokuwa wakiheshimika zaidi katika muziki wa dansi. 

BANZ 03

NYIMBO ZILIZOACHA HISTORIA 
Kilichomtofautisha Banza Stone ni uwezo wake wa kuandika nyimbo zenye mafunzo ya maisha, mapenzi na changamoto za jamii.

Wapenzi wa muziki wa dansi bado wanazikumbuka kazi zake kama Mtaji wa Maskini, Elimu ya Mjinga, Kumekucha, Angurumapo Simba, Mtu Pesa, Falsafa ya Maisha, Hujafa Hujasifiwa, Jahazi, Euro na nyingine nyingi ambazo hadi leo zinaendelea kupigwa kwenye vipindi mbalimbali vya muziki.


DAKIKA ZA MWISHO
Katika miezi ya mwisho ya maisha yake, afya ya Banza Stone ilianza kudhoofika. Alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa uliomfanya ashindwe kutembea na hata kujihudumia mwenyewe bila msaada wa ndugu zake.


Wakati huo kulikuwa na taarifa nyingi za uzushi kuhusu kifo chake, lakini familia yake iliendelea kuzikanusha hadi Julai 17, 2015 alipofariki nyumbani kwao Sinza Kijiweni, Dar es Salaam, baada ya kuugua kwa muda mrefu.

BANZ 04

KIFO KILICHOACHA SIMANZI 
Taarifa za kifo chake zilienea haraka kwenye mitandao ya kijamii na kusababisha viongozi wa muziki, wasanii na mashabiki wengi kutoa salamu za pole.

Mazishi yake yalifanyika Julai 18, 2015 katika makaburi ya Sinza, Dar es Salaam, yakihudhuriwa na mamia ya waombolezaji, wakiwemo wanamuziki wa dansi na wadau mbalimbali wa sanaa waliokwenda kumpa heshima zao za mwisho.


KAULI YA FAMILIA
Katika kuadhimisha miaka 11 tangu kifo cha Banza Stone, Mwanaspoti limezungumza na kaka yake, Hassan Masanja, ambaye anasema familia imeandaa dua maalumu nyumbani kwao Sinza kwa ajili ya kumuombea marehemu pamoja na kuendelea kuenzi mchango wake katika muziki wa dansi.

"Leo (Julai 17) hatuna shughuli kubwa zaidi ya dua ya kumuombea Banza nyumbani. Kila mwaka familia hukutana kumkumbuka na kumuombea. Tunaamini hiyo ndiyo njia bora ya kuendelea kumuenzi," anasema Hassan.

Hata hivyo, Hassan amesema jambo ambalo bado linaumiza familia ni kukosekana kwa ushirikiano na mawasiliano kutoka kwa baadhi ya wanamuziki na viongozi wa bendi ambao waliwahi kufanya kazi kwa karibu na Banza Stone enzi za uhai wake.

Anasema tofauti na walivyotarajia, miaka imepita huku wengi wa waliokuwa marafiki na washirika wa karibu wa Banza wakikosa hata kufika nyumbani au kuwasiliana na familia katika siku za kumbukumbu yake.

Sio mara ya kwanza familia kueleza hisia hizo. Hata katika mahojiano ya awali na Mwanaspoti, familia hiyo ilisema tangu Banza Stone afariki dunia, mawasiliano na wengi wa wanamuziki aliowahi kufanya naye kazi yamekuwa hafifu, jambo ambalo limewaacha wakihisi upweke katika kuendeleza kumbukumbu yake.

BANZ 02

WANAMUZIKI WATOA KAULI
Kauli ya familia kwamba imekosa mawasiliano ya karibu na wanamuziki waliowahi kufanya kazi na Banza Stone iliwahi kujibiwa na baadhi ya wasanii wa muziki wa dansi kupitia mahojiano na Mwanaspoti.

Kiongozi wa bendi ya Twanga Pepeta, Luizer Mbutu, alisema anafahamu kilio cha familia hiyo, lakini akaeleza kuwa hali hiyo si ya familia ya Banza pekee.

"Ni kweli kabisa familia inavyosema mawasiliano hayapo kama alipokuwa hai. Hii ni kawaida kwetu Watanzania, si kwa Banza tu. Hata mimi siku Mungu akinichukua, familia yangu huenda isiwe na mawasiliano na watu wangu wa karibu kwa sababu mimi ndiye nilikuwa kiunganishi," amesema.

Kwa upande wake, mwanamuziki Ramadhani Mhoza 'Rama Pentagone', alisema changamoto hiyo ilitokana pia na familia ya Banza kutokuwa karibu sana na wanamuziki wakati wa uhai wake, tofauti na mama yake ambaye alikuwa na ukaribu mkubwa na wasanii wengi.

"Familia ya Banza haikuwa karibu na wanamuziki kama alivyokuwa marehemu mama yake. Hilo lilifanya iwe vigumu kuendelea na ukaribu baada ya kifo chake."

Hata hivyo, wanamuziki hao walisisitiza kuwa mchango wa Banza Stone katika muziki wa dansi hauwezi kusahaulika. Luizer Mbutu alimuelezea kama msanii mwenye vipaji vingi aliyekuwa mwimbaji, mtunzi, mpiga ngoma na mtunzi wa nyimbo zenye ujumbe wa kijamii, huku Rama Pentagone akisema Banza alikuwa miongoni mwa waimbaji wachache waliotumia muziki kuelimisha jamii badala ya kuimba nyimbo za mapenzi pekee


URITHI WAKE BADO UNAISHI 
Miaka 11 tangu afariki, jina la Banza Stone bado linatajwa miongoni mwa waimbaji bora waliowahi kutokea katika muziki wa dansi Tanzania. Sauti, mashairi na uwezo wake wa kuwasilisha ujumbe vinaendelea kuwavutia mashabiki wa zamani na kizazi kipya kupitia YouTube, vipindi vya redio na majukwaa mengine ya kidijitali.

Nyimbo kama Mtaji wa Maskini, Kumekucha, Elimu ya Mjinga na Angurumapo Simba zinaendelea kuwa sehemu ya historia ya muziki wa dansi nchini, zikithibitisha kwamba msanii anaweza kufariki, lakini kazi nzuri huendelea kuishi milele.