Kama utani, Kanumba kawakutanisha tena
Muktasari:
- Kanumba alifariki katika ugomvi na aliyekuwa mpenzi wake, Elizaberth Michael ‘Lulu’ Aprili 7, 2012, akiwa ameacha historia isiyofutika kwa jinsi alivyoitangaza tasnia ya filamu ndani na nje ya nchi.
HUWEZI kuamini, lakini ukweli ni kwamba imetimia miaka sita sasa tangu aliyekuwa staa wa filamu nchini, Steven Kanumba kufariki dunia.
Kanumba alifariki katika ugomvi na aliyekuwa mpenzi wake, Elizaberth Michael ‘Lulu’ Aprili 7, 2012, akiwa ameacha historia isiyofutika kwa jinsi alivyoitangaza tasnia ya filamu ndani na nje ya nchi.
Umahiri na ujanja wa Kanumba uliwezesha kuwavuta baadhi ya mastaa wakali wa filamu Afrika na duniani kama Ramsey Nouah wa Nigeria.
Kanumba aliweza kuonesha uthubutu hata pale ambapo wasanii wenzake waliona ni pagumu kufikika bila kujali jamii itamchukuliaje au itamuongeleaje.
Jambo hilo lilimfanya kujulikana kwa kasi na moja ya mambo yaliyozidi kumpa sifa ni pale alipoalikwa kuwa mmoja wa wageni katika mashindano makubwa ya ‘Big Brother Africa’, mashindano ambayo yanaangaliwa na nchi nyingi duniani.
Enzi za uhai wake kabla ya soko la filamu kuanza, Kanumba alitamba katika maigizo mbalimbali yaliyorushwa hewani katika runinga kupitia kundi lao la Kaole Sanaa.
Baadhi ya michezo iliyompaisha yeye na wasanii wenzake wa Kaole ni Jahazi, Dira, Zizimo, Tufani, Sayari, Taswira, Gharika na Baragumu na alipoingia kwenye filamu kazi kama Saturday Morning, Deception, Devil Kingdom, Ophra, The Shock, Uncle JJ, Big Daddy, Because of You, Ndoa Yangu, This is It na Love & Power zilimpaisha.
MWAKA HUU
Kuelekea kumbukumbu ya Kanumba, kama utani wasanii walioibuliwa na mkali huyo enzi za uhai wake, Othman Njaidi ‘Patrick’ na Hanifa Daud ‘Jenifer’ wamekutanishwa tena ndani ya mwaka huu wa sita.
Jenifer alinyakua Tuzo ya Msanii Bora Chipukizi mwaka 2010 katika Min ZIFF kupitia filamu alizocheza na Kanumba.
Wasanii hao walikutanishwa kwa mara ya kwanza na Kanumba alipowaibua kupitia filamu za Uncle JJ na This Is It kabla ya baadaye kuingiza katika After Death ya Jacquiline Wolper kuonyesha baada ya kifo cha ‘anko’ Kanumba wanaishije.
Lakini sasa, tofauti na miaka ya nyuma kumbukumbu ya kifo chake safari hii imebebwa na wasanii wa Kundi la Soweto ambao alikuwa mlezi wao enzi za uhai wake.
Mbali na hao pia wamejitokeza wasanii watano Wakenya kutengeneza wimbo maalumu wa kuomboleza kifo chake wakiongozwa na Paul Leornard ’Katapila’.
Wasanii wengine walio kwenye msafara huo ni Vivian Siyu ‘Viv’, Neema Selestine ‘Manyaya’, Yuster Wilfred ‘Light’ na Harrison Moega.
MPANGO MTAMU
Hata hivyo, wakati wakiwa tayari wametengeneza wimbo huo Kenya, wasanii hao walikuja kuitengeneza video Bongo na kuwashirikisha kina Patrick na Jenifer.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti Patrick anasema kitendo kilichofanywa na wasanii hao wa mbali cha kuwakutanisha na Jenifer waliopotezana kwa muda mrefu tangu Kanumba afariki kimempa faraja kubwa.
“Kwa kweli walichokionyesha wenzetu Wakenya ni kitu kikubwa, inaonesha namna gani marehemu alivyowagusa wengi kuanzia ndani na nje ya nchi. Tunajivunia kwa hili kama watu ambao tulifanya naye kazi tukiwa wadogo mpaka sasa tumekuwa watu wazima,” alisema Patrick.
MSIKIE JENIFER
Kwa upande wake mwanadada huyo anayetarajiwa kutimiza miaka 18 anasema amefarijika na jambo hilo linampa moyo ni namna gani watu wanamthamini Kanumba hata baada ya kuondoka duniani.
“Hili limejionesha hata nilipoombewa ruhusa shuleni kwa ajili ya kuja kupiga picha za video ya wimbo huu kwani mkuu wa shule alimkubalia mama bila vikwazo vyovyote,” alisema.
WAKENYA WASHANGAA
Kiongozi wa wasanii hao wa Kenya waliofyatua wimbo wa ‘Kanumba Anarudi Tena’ Paul Leornard, alisema moja ya jambo lililowasukuma kutengeneza wimbo huo ni katika kuonesha ni namna gani walikuwa na mapenzi na upendo kwake.
Katapila alisema mbali na watu wa kawaida na wasanii kutambua kipaji chake hadi Rais wa Kenya, Uhuru Kenyata anamfahamu hasa katika filamu zake za Uncle JJ na This is It na ndio maana waliona kuna umuhimu pia wa kuwashirikisha Jenifer na Patrick katika video ya wimbo huo.
Pia, amesikitika namna ambavyo wasanii wa hapa nchini walivyo nyuma katika kumuenzi Kanumba ambaye kwao waliomuona ni msanii wa aina yake.
“Kama mtashindwa kumthamini mtu kwa kuwa hayupo duniani, ni aibu kwa Taifa hili mpaka wasanii kutoka nje kujitolea kutengeneza wimbo huo kwa heshima yake.
“Pia kwa taarifa yenu tutamsaidia zaidi mama katika kutengeneza filamu na huu wimbo ni mwanzo tu, kama nyie hamumthamini, basi watu wengine tunamthamini kwani tunajua namna gani alivyoibua wasanii maarufu nchi hii,” alisema Katapila.
MAMA KANUMBA APAGAWA
Mama Kanumba kwa upande wake alisema tangu alipopokea simu ya kutaarifiwa ujio wa wasanii hao kuja kufanya jambo hilo, aliishiwa maneno na kujiuliza maswali mengi Kanumba ni nani. Pia, alisema mbali na Wakenya tayari kuna watu kutoka Oman walishamtembelea na hapo alipo ana tiketi ya kwenda Oman kupumzika kwa siku kadhaa.
Mama Kanumba anasema hiyo yote ni kuonesha jinsi watu wanavyojali mchango wa mwanaye.
Baadhi ya wasanii waliokubali kushiriki katika video ya wimbo huo wa ‘Kanumba anarudi Tena’ akiwemo mkongwe Mohamed Fungafunga ‘Jengua’ na kusisitiza licha ya kuwashukuru Wakenya lakini amesikitishwa na kitendo cha baadhi ya wasanii wa hapa Bongo namna walivyolipokea jambo hilo tofauti. Katika maelezo yake, Jengua alisema baadhi ya wasanii waliojulishwa na mama Kanumba kushiriki tukio hilo la upigaji picha, walitaka walipwe fedha wakati Wakenya waliamua kujitolea kama njia ya kumuenzi marehemu Kanumba.
WAKENYA WAJITOLEA
Jambo hilo la wasanii kutaka wadakishwe kitu kidogo, limedhibitishwa na Mama Kanumba, Flora Mtegoa alisema wasanii kama sita aliwaosiliana nao kuhusu ishu hiyo, swali la kwanza kumuuliza ni ‘kuna hela?’ Alisema jambo hilo limemuuma ukizingatia wapo ambao hadi leo wana majina mjini ambao wamepitia katika mikono ya Kanumba, lakini ajabu hawakumbuki mchango wake.
Naye Amina Abdallah, Mwanakamati wa Maandalizi ya Siku ya Kanumba kwa mwaka huu kupitia kundi la maagizo la Soweto lililobeba shughuli hiyo, alisema kilichowagusa mbali na Kanumba kuwa mlezi wao pia, alikuwa akiwafundisha sanaa.