ZALI LA MENTALI: Neymar alivyopewa urithi wa mtu asiyemfahamu
Muktasari:
- Kinachoelezwa ni kwamba kuna bilionea mmoja amefariki dunia na ameacha wosia wa Pauni 846 milioni, ambazo ameelekeza apewe staa huyo wa kimataifa wa Brazil.
RIO DE JANEIRO, BRAZIL: MWENYE nacho huongezewa, usipingane na maandiko. Na hicho ndicho unachoweza kusema baada ya supastaa wa Kibrazili, Neymar kuripotiwa kwamba anajiandaa kupokea mkwanja mrefu wa pesa ya urithi kutoka kwa bilionea ambaye si ndugu yake na hajawahi kumwona.
Kinachoelezwa ni kwamba kuna bilionea mmoja amefariki dunia na ameacha wosia wa Pauni 846 milioni, ambazo ameelekeza apewe staa huyo wa kimataifa wa Brazil.
Tajiri huyo ambaye hakufahamika ni Mbrazili pia, lakini kinachoelezwa hajawahi kukutana na Neymar, ambaye aliwahi kutamba na klabu za Paris Saint-Germain na Barcelona huko Ulaya.
Tajiri huyo hana mke wala watoto kwa mujibu wa taarifa ya gazeti la Kibrazili la RIC, huku wosia wake ulihifadhiwa kwenye ofisi za kimamlaka huko Porto Alegre, Juni 12 na ulishuhudiwa na mashahidi wawili. Taarifa zinadai kwamba tajiri huyo mfanyabiashara alichagua staa huyo wa Santos kuwa mrithi wa mali zake. Kinachoelezwa ni kwamba tajiri huyo alikuwa na muunganiko na familia ya Neymar kwamba wazazi wake huko nyuma waliwahi kuwa na uhusiano mzuri na familia ya mkali huyo wa zamani wa Al Hilal, anayeshikilia rekodi ya kuwa mchezaji ghali kuwahi kusajiliwa kwa ada ya mara moja, Pauni 198 milioni.
Mahakama za Brazil sasa zipaswa kuweka mambo wazi kabla ya Neymar kutambulika rasmi kama mrithi wa mali za mfanyabiashara huyo tajiri. Wasiwasi mkubwa wa kisheria unaweza kuibuka, lakini Neymar, 33, mwenyewe bado hajasema kitu kuhusu urithi huo wa pesa nyingi.
Neymar mwenyewe maisha yake yamekuwa ni ya kifahari sana, akiwa mmoja wa wanasoka waliopata pesa nyingi duniani, ikiwamo mkwanja aliovuna huko Saudi Arabia.
Wakati Neymar akijiunga na Al Hilal mwaka 2023 mshahara wake ulikuwa Pauni 2.5 milioni kwa mwaka, lakini mkataba wake ulivunjwa kutokana na mchezaji huyo kuumia mara kwa mara.
Ukiweka kando mshahara huo mnono, Neymar alikabidhiwa pia jumba lenye vyumba 25 lenye bwawa la kuogelea, sauna tatu na wafanyakazi watano.
Si mambo hayo tu, Neymar alipewa ndege binafsi pia, magari matatu ya kifahari, zikiwamo Mercedes G Wagons nne na Mercedes van. Sambamba na hilo Neymar pia alipewa dereva wa kumwendesha kwa muda wote. Huko kwenye kikosi cha Santos, Neymar analipwa mshahara wa Pauni 135,507 kwa mwezi. Pauni 32,500 kwa wiki anayolipwa kwa sasa ni kiwango kidogo sana cha pesa kwa viwango vya pesa ambazo amekuwa akivuna supastaa huyo.
Neymar amekuwa na dili tamu pia za haki za taswira ambalo linamwingizia Pauni 819,433 kwa mwezi. Kutokana na hilo, Neymar ameamua kubaki zake Brazil hadi fainali za Kombe la Dunia 2026.