Lionel Messi afungukia picha na Lamine Yamal
Muktasari:
- Baada ya Argentina kuifunga England na kutinga fainali, sasa itakutana na Hispania katika mchezo mkubwa wa Jumapili, ambapo Messi atakabiliana na nyota mwenye miaka 19 anayechukuliwa kuwa mrithi wake, Lamine Yamal.
NEW YORK, MAREKANI: NAHODHA wa Argentina, Lionel Messi, amesema picha iliyosambaa duniani ikimuonyesha akimuogesha Lamine Yamal alipokuwa mtoto wa miezi sita ni jambo la kushangaza sana, huku wawili hao wakijiandaa kukutana kwenye fainali ya Kombe la Dunia karibu miaka 20 baadaye.
Baada ya Argentina kuifunga England na kutinga fainali, sasa itakutana na Hispania katika mchezo mkubwa wa Jumapili, ambapo Messi atakabiliana na nyota mwenye miaka 19 anayechukuliwa kuwa mrithi wake, Lamine Yamal.
Baada ya kuthibitishwa kwa mchezo huo wa fainali, picha ya mwaka 2007 ilirejea tena kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii.
Picha hiyo inaonyesha Messi, aliyekuwa nyota wa Barcelona wakati huo, akishiriki picha maalumu kwa ajili ya gazeti la Diario Sport na shirika la UNICEF. Katika tukio hilo, Messi alikuwa amekaa chini akimsaidia kumuogesha Yamal kwenye beseni la plastiki la rangi ya buluu kabla ya kumbeba akiwa amefunikwa kwa taulo.
Picha hizo zilichapishwa kwenye Instagram na baba wa Yamal, Mounir Nasraoui, mwaka 2024 akiwa ameandika: "Mwanzo wa hadithi za mastaa wawili."
Siku mbili kabla ya fainali hiyo ya Kombe la Dunia, Messi aliulizwa kuhusu picha hizo alipokuwa akishiriki Fanatics Fest mjini New York.
Messi amesema:
"Picha ile ilikuwa ya kushangaza. Alikuwa mtoto mdogo kabisa, lakini sasa tunakutana uwanjani. Kwa kweli ni picha ya ajabu sana."
Aliendelea kusema:
"Namtakia kila la heri. Pia ni sehemu ya familia ya Barcelona. Tutajaribu kuwapa Hispania mchezo mgumu iwezekanavyo, lakini Lamine si mchezaji pekee mzuri waliyenaye. Tutapambana kwa nguvu zetu zote."
Kabla ya kuzungumzia picha hizo, Messi alimwelezea Yamal kuwa ni mmoja wa wachezaji bora zaidi duniani kwa sasa.
"Ana miaka 19 tu na maisha yake ya soka bado yapo mbele yake. Ana nafasi kubwa ya kuweka historia, lakini sisi pia tutapambana kwa uwezo wetu wote," amesema Messi.
Mpiga picha Joan Monfort, anayefanya kazi kama mpiga picha wa kujitegemea wa AP, ndiye aliyepiga picha hizo mwaka 2007 katika kalenda ya hisani iliyoandaliwa na gazeti la Sport kwa kushirikiana na UNICEF.
Monfort amesema:
"Sijawahi kuamini kwamba mambo fulani yamepangwa kutokea, lakini sasa naanza kuwa na mashaka. Hili linazidi maelezo yoyote ya kawaida."
Inadaiwa kuwa mama wa Yamal alipata nafasi ya kushiriki kwenye upigaji picha huo baada ya kushinda droo ya familia zilizokuwa zimejitokeza kutoka mji wa Mataró karibu na Barcelona.
Hatima ya soka ikafanya mtoto huyo aliyekuwa miezi sita tu kukutana na Messi, ambaye baadaye alikuja kuwa mmoja wa wachezaji wakubwa zaidi kuwahi kutokea duniani.
Messi alikuwa na miaka 20 tu alipokutana na Yamal, miaka michache kabla hajawa nyota mkubwa wa dunia.
Sasa akiwa na miaka 39 na akiwa hachezi tena katika moja ya ligi tano kubwa za Ulaya, Messi bado anaendelea kuonyesha kiwango cha juu baada ya kuiwezesha Argentina kufika fainali ya pili mfululizo ya Kombe la Dunia.
Wengi wanaamini Yamal ndiye atakayekuwa mrithi wake kama mchezaji bora zaidi duniani baada ya tayari kuisaidia Hispania kutwaa ubingwa wa Ulaya na kushinda mataji matatu ya Hispania akiwa na Barcelona kabla hata hajafikisha miaka 19.