Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Yamal akabidhiwa ufalme, Messi akiaga kwa machozi

YAMAL Pict

Muktasari:

  • Messi, mwenye umri wa miaka 39, alisimama kwa muda mrefu akiitazama bahari ya mashabiki wa Argentina waliokuwa wakiimba jina lake ndani ya Uwanja wa New York New Jersey, wakimtunuku heshima ambayo huenda ilikuwa ya mwisho kwenye jukwaa kubwa zaidi la soka duniani.

NEW YORK, MAREKANI: DAKIKA chache baada ya Hispania kutwaa Kombe la Dunia kwa kuichapa Argentina 1-0, tukio moja lilivuta hisia za mashabiki kuliko hata shangwe za ubingwa. Lamine Yamal alimkumbatia Lionel Messi aliyekuwa akilia, kana kwamba alikuwa akikabidhiwa rasmi ufalme wa soka la dunia.

Messi, mwenye umri wa miaka 39, alisimama kwa muda mrefu akiitazama bahari ya mashabiki wa Argentina waliokuwa wakiimba jina lake ndani ya Uwanja wa New York New Jersey, wakimtunuku heshima ambayo huenda ilikuwa ya mwisho kwenye jukwaa kubwa zaidi la soka duniani.

YAM 02

Akatokea Lamine Yamal.

Kijana huyo wa Hispania alimfuata Messi, akampa faraja kabla ya wawili hao kukumbatiana kwa hisia kubwa. Ilikuwa ni picha iliyobeba ujumbe mzito; nyota wa jana akimkabidhi kijiti nyota wa kesho.

Ni tukio lililokumbusha picha maarufu ya mwaka 2007, ambapo Messi mwenye umri wa miaka 20 alikuwa akimuogesha mtoto wa miezi sita, Lamine Yamal, kwa ajili ya kalenda ya hisani ya Barcelona. Miaka 19 baadaye, mtoto huyo ndiye aliyekuwa amesimama mbele yake akiwa bingwa wa dunia.


Yamal amaliza ndoto mapema

Akiwa ana miaka 19 na siku sita, Yamal tayari ameweka rekodi ambayo mastaa wengi huota maisha yao yote.

Baada ya kutwaa Euro 2024, sasa ameongeza Kombe la Dunia 2026, na kuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kushinda mataji hayo mawili.

Nyota huyo wa Barcelona aliingia kwenye mashindano akiwa na majeraha ya msuli wa nyuma wa paja, lakini alimaliza akiwa mmoja wa wachezaji walioangaza zaidi kwenye fainali.

Kwa ushindi huo, Hispania imeendeleza rekodi ya Yamal ya kutopoteza mechi yoyote ya ushindani akiwa na timu ya taifa.

Amecheza mechi 28 za ushindani bila kufungwa, huku akianza michezo 13 ya mashindano makubwa na kushinda yote, rekodi bora kabisa kwa mchezaji wa Ulaya.

Pamoja na beki Pau Cubarsi, wote wenye miaka 19, wameingia kwenye historia ya kuwa vijana wa nne na wa tano kuanza fainali ya Kombe la Dunia na kuibuka mabingwa, wakifuata nyayo za Pele (1958), Giuseppe Bergomi (1982) na Kylian Mbappe (2018).

Kocha wa Hispania, Luis de la Fuente, hakuficha furaha yake.

“Ninamshukuru sana Lamine. Ameonyesha kiwango kikubwa na bado ataendelea kukua. Muhimu zaidi alijitoa kwa ajili ya timu, jambo ambalo lina thamani kubwa kwangu,” amesema.

YAM 01

Hakutikiswa na Argentina

Mbali na kipaji chake kikubwa, Yamal ameonyesha ukomavu wa hali ya juu.

Katika fainali hiyo alikumbana na ubabe wa mabeki wa Argentina, hasa Nicolas Tagliafico, ambaye alimchezea kwa nguvu mara kadhaa.


Lakini Yamal hakujibu kwa hasira.

Kipa wa zamani wa England, Joe Hart, amesema jambo hilo ndilo lililomvutia zaidi.

“Hakutikisika hata kidogo. Hakurudisha mapigo wala kuogopa. Argentina walijaribu kila namna kumzuia, lakini alibaki mtulivu. Ukiangalia ana miaka 19 tu, unaweza kusema tayari amekamilisha kila kitu kwenye soka la kimataifa,” amesema Hart.


Bado safari yake ndiyo kwanza inaanza.

Akiwa na viongozi kama Rodri ndani ya kikosi cha Hispania, wengi wanaamini huu ni mwanzo wa mafanikio makubwa zaidi.

YAM 03

Messi aondoka kwa majonzi

Furaha ya Yamal ilikuwa kinyume kabisa na hali ya Lionel Messi.

Baada ya filimbi ya mwisho, nahodha huyo wa Argentina alionekana mwenye huzuni kubwa akiwatazama mashabiki wake, huku wengi wakiamini hiyo ndiyo ilikuwa mechi yake ya mwisho kwenye Kombe la Dunia.

Kocha Lionel Scaloni alishindwa hata kujizuia alipoulizwa kama huo ulikuwa mwisho wa Messi katika mashindano hayo.

Alianza kujibu swali hilo kabla ya kushindwa kuendelea kutokana na hisia kali na kuondoka kwenye mkutano wa waandishi wa habari akiwa analia.

YAM 06

Argentina yajichanganya yenyewe

Badala ya kucheza soka lao la kawaida lililoitoa England nusu fainali, Argentina ilitumia muda mwingi kucheza kwa mabavu na kuvuruga mchezo.

Mwamuzi Slavko Vincic aliwaruhusu mara kadhaa wachezaji wa Argentina kucheza kwa nguvu bila kutoa kadi mapema.

Alexis Mac Allister aliponea onyo baada ya kumchezea vibaya Dani Olmo, huku Lisandro Martinez akipewa kadi ya kwanza dakika ya 40 baada ya kumuangusha Mikel Oyarzabal.

Messi mwenyewe alionekana akimshinikiza mwamuzi ampe kadi nyekundu Marc Cucurella kwa madai ya kufunika mdomo alipokuwa akizungumza.

Dakika chache kabla ya muda wa nyongeza, Enzo Fernandez alimrukia Pau Cubarsi bila hata kuangalia mpira na kutolewa kwa kadi ya pili ya njano, jambo lililoizidishia matatizo Argentina.


Takwimu zilionyesha ubovu wa mchezo wao.

Katika dakika 90 za kawaida, Argentina haikupiga hata shuti moja lililolenga lango, ikiwa timu ya kwanza kufanya hivyo kwenye historia ya fainali za Kombe la Dunia.

Shuti lao la kwanza lilikuja dakika ya 117 kupitia Messi, lakini nalo halikulenga lango.

Kwa upande mwingine, Hispania ilipiga mashuti 12 yaliyolenga lango.

Katika kipindi cha kwanza pekee, Argentina ilifanya makosa tisa huku ikiwa imekamilisha pasi nane tu kwenye theluthi ya mwisho ya uwanja, ishara ya namna walivyokuwa wakitanguliza mapambano kuliko soka.

YAM 04

Mwisho mchafu

Baada ya filimbi ya mwisho, machozi ya Messi na wachezaji wenzake yaliambatana na vurugu ndogo uwanjani.

Leandro Paredes alionekana akimkamata Eric Garcia koo, huku pia akihusika katika tukio lililosababisha Gavi kuangushwa chini. Haikuwa mwisho mzuri kwa Argentina kwenye fainali ambayo ilitarajiwa kuandika historia tofauti.

Kwa Hispania, safari iliyoanza kwa sare ya kushtukiza dhidi ya Cape Verde imeishia kwa ubingwa.

Na kama enzi ya Messi inaonekana kufungwa rasmi, basi dunia ya soka sasa inaonekana kuingia zama mpya za Lamine Yamal.