Keyne Yamal ateka tena shoo!
Muktasari:
- Mtoto huyo aliteka kila kitu baada ya kukimbia uwanjani mara tu baada ya filimbi ya mwisho katika Uwanja wa MetLife, akiwa amevaa jezi ya Hispania yenye namba 19 ya kaka yake na jina lake mgongoni.
KEYNE ATEKA TENA SHOO!
MIAMI, MAREKANI: WAKATI mashabiki wa soka duniani wakimsifu nyota wa Hispania, Lamine Yamal, baada ya kuiongoza timu yake kutwaa ubingwa wa Kombe la Dunia kwa kuichapa Argentina bao 1-0, aliyekuwa gumzo zaidi baada ya mchezo huo hakuwa mfungaji wala nahodha wa timu, bali alikuwa mdogo wake mwenye umri wa miaka mitatu, Keyne.
Mtoto huyo aliteka kila kitu baada ya kukimbia uwanjani mara tu baada ya filimbi ya mwisho katika Uwanja wa MetLife, akiwa amevaa jezi ya Hispania yenye namba 19 ya kaka yake na jina lake mgongoni.
Alipomwona mdogo wake akimkimbilia, Yamal hakusita. Alimkumbatia kwa furaha, akambeba juu hewani kabla ya kumshusha taratibu na kumvalisha kofia nyekundu yenye maandishi ya "Lamine", jambo lililowafurahisha maelfu ya mashabiki waliokuwa uwanjani.
Lakini huo haukuwa mwisho wa burudani.
Keyne aliendelea kuzurura uwanjani hadi askari wa Jimbo la New Jersey alipovua kofia yake na kumvalisha mtoto huyo kwa muda. Baada ya kuivaa kwa tabasamu kubwa, Keyne aliirudisha kwa heshima, tukio lililozua vicheko na kushangiliwa na mashabiki.
Katika mashindano haya, Keyne amegeuka kuwa mmoja wa watu maarufu zaidi licha ya kutocheza hata dakika moja. Mara kadhaa alionekana kwenye skrini kubwa za viwanjani, huku picha zake zikisambaa kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari duniani.
Hata kabla ya mechi, mtoto huyo aliwahi kumfunga bao mshambuliaji Nico Williams wakati wa mazoezi ya kupasha misuli moto, jambo lililoongeza mvuto wake kwa mashabiki.
Jarida la Hola! la Hispania lilimwelezea Keyne kama "hisia kubwa zaidi ya mashindano", likisema si wachezaji, mabao wala kombe vilivyoteka hisia za watu, bali ni mtoto huyo mwenye umri wa miaka mitatu.
Vyombo mbalimbali vya habari vimempa majina kama "Nyota wa Kombe la Dunia 2026", "Superstar wa Hispania jukwaani" na "Mtu anayependwa zaidi kwenye mashindano."
Umaarufu wake uliongezeka zaidi baada ya robo fainali dhidi ya Ubelgiji, aliponaswa na kamera akimpungia kaka yake huku akitoa ulimi mbele ya skrini kubwa ya uwanjani.
Yamal hakuweza kujizuia kucheka alipomwona mdogo wake akifanya utani huo.
Baadaye aliwaambia waandishi wa habari kuwa tayari alikuwa amepewa taarifa.
"Nilikuwa kwa mtaalamu wa tiba, akanipigia simu kwa simu ya mama na kuniambia kesho atatoa ulimi mbele ya kamera. Nilipomwona kwenye skrini nilishindwa kujizuia kucheka," amesema Yamal.
Keyne alizaliwa Septemba 2022 na ni mtoto wa mama wa Yamal, Sheila Ebana. Ingawa hawana baba mmoja, Yamal amesema uhusiano wao ni wa kipekee.
"Mdogo wangu ana maana kubwa sana kwangu. Ninampenda mno, wakati mwingine nahisi kama ni mwanangu," amesema nyota huyo wa Barcelona.
Kwa wanaomfuatilia Yamal kwa karibu, Keyne si sura mpya.
Mara nyingi wawili hao huonekana wakicheza mpira pamoja, wakifanya video za TikTok, kusherehekea ubingwa wa Barcelona na hata kuimba wimbo wa klabu hiyo nyumbani.
Yamal pia amewahi kusema kuwa ndoto yake kubwa ni kuhakikisha mdogo wake anapata maisha mazuri na utoto ambao yeye hakuwahi kuupata.
"Mama alinipata akiwa na miaka 16. Baba alikuwa akifanya kazi yoyote ili tupate chakula. Mimi kazi yangu ni kucheza mpira na kuwafurahisha mashabiki. Ninapomwona mama akiwa na furaha na mdogo wangu akiwa na utoto mzuri, hicho ndicho kinachonifurahisha zaidi," amesema.
Katika maisha ya familia yao pia kuna simulizi ya kipekee.
Mwaka 2007, Yamal akiwa mtoto wa miezi mitano alipigwa picha maarufu akiwa anaogeshwa na Lionel Messi baada ya familia yake kushinda droo iliyoandaliwa na gazeti la Sport.
Leo hii, Yamal amekuwa mmoja wa nyota wakubwa wa soka duniani, huku mdogo wake Keyne akionekana kufuata nyayo za umaarufu wake kwa kasi kubwa.
Kwa sasa, wakati dunia ikimshangilia Lamine Yamal kwa mafanikio yake uwanjani, ni wazi kuwa Keyne ndiye "MVP" wa mioyo ya mashabiki nje ya uwanja.