Ukuta wa Yanga wampa kazi Lucas Kikoti
Muktasari:
- Kikoti, ambaye hadi sasa hajafungua akaunti yake ya mabao msimu huu, anasema bado hajaanza vizuri kama alivyotarajia, huku akifichua kuwa moja ya sababu iliyomfanya achelewe kuingia kwenye kasi ni mapumziko marefu aliyoyapata nyumbani kabla ya kuanza kwa msimu.
UKUTA wa Yanga umeonekana kuwa kikwazo kwa washambuliaji wengi msimu huu, lakini kiungo mshambuliaji wa Namungo, Lucas Kikoti, tayari ameonja ugumu wake na kuweka wazi safu anayoiona kuwa ngumu zaidi kwenye Ligi Kuu Bara.
Kikoti, ambaye hadi sasa hajafungua akaunti yake ya mabao msimu huu, anasema bado hajaanza vizuri kama alivyotarajia, huku akifichua kuwa moja ya sababu iliyomfanya achelewe kuingia kwenye kasi ni mapumziko marefu aliyoyapata nyumbani kabla ya kuanza kwa msimu.
Licha ya mwanzo huo, kiungo huyo mwenye uzoefu ameweka wazi kuwa bado ana malengo ya kuisaidia Namungo kupanda kwenye nafasi za juu, huku binafsi akilenga kufunga angalau mabao matatu msimu huu.
“Kwangu msimu haujaanza vizuri kama nilivyotarajia kwa sababu nilipata mapumziko marefu zaidi nyumbani kabla ya msimu kuanza, hivyo niliporudi nilikuwa bado najitafuta. Lakini najisukuma ili nirudi kwenye kiwango changu na malengo yangu ni kuisaidia Namungo ifike nafasi za juu, pamoja na kufikisha mabao matatu,” anasema Kikoti.
UKUTA WA YANGA
Katika msimu ambao kila timu inapambana kupata matokeo, Kikoti amekutana na safu kadhaa za ulinzi, lakini anaitaja ya Yanga kuwa ndiyo ngumu zaidi kwake hadi sasa.
Anasema ubora wa safu hiyo unatokana na uwepo wa mabeki wenye uzoefu kuanzia pembeni hadi katikati, hali anayodai inawapa uwezo wa kusoma mchezo na kudhibiti mashambulizi ya wapinzani.
“Safu ngumu zaidi ambayo nimekutana nayo msimu huu ni ya Yanga. Wana wachezaji wengi wa nyuma wenye uzoefu, kuanzia full back mpaka mabeki wa kati, na uzoefu wao unawasaidia sana kutawala mchezo,” anasema Kikoti.
NZENGELI AMVUTIA
Mbali na kuitaja safu ya ulinzi ya Yanga, Kikoti pia amemchagua Maxi Nzengeli kuwa mchezaji anayemvutia zaidi katika Ligi Kuu kutokana na namna anavyojituma na kuisaidia timu yake.
Kikoti anasema kinachomfanya amfuatilie Nzengeli si uwezo wake pekee wa kucheza, bali pia namna alivyo mchezaji anayejitoa kwa ajili ya timu, huku akifichua kuwa kuna watu ambao wamekuwa wakimfananisha naye kutokana na tabia yake ya kuwa mpole.
“Maxi Nzengeli ni mchezaji ambaye nampenda kumuona akicheza kwa sababu anajitoa na anaendelea kuisaidia timu yake. Pia kuna watu wamekuwa wakinifananisha naye kwa sababu ya upole wetu,” anasema Kikoti.
VIWANJA VIMEBADILIKA
Kwa upande wa viwanja, Kikoti anaona Ligi Kuu Bara imepiga hatua ikilinganishwa na miaka ya nyuma, akisema ubora wake umeendelea kuongezeka.
Kwa mchezaji ambaye hutumia muda mwingi kwenye viwanja tofauti kutokana na ratiba ya ligi, anasema mabadiliko hayo ni jambo linaloonekana na linasaidia kuongeza mazingira mazuri ya mchezo.
“Viwanja vya sasa vimeongezeka ubora na vimeboreshwa zaidi ukilinganisha na miaka ya nyuma. Kuna tofauti kubwa ambayo inaonekana,” anasema.
RATIBA INAMCHOSHA
Hata hivyo, pamoja na kuboreka kwa viwanja, Kikoti anaona bado kuna changamoto ya muda mrefu ambayo imekuwa ikiwakabili wachezaji, nayo ni ratiba ya Ligi Kuu Bara.
Anasema wakati mwingine kucheza mechi chache ndani ya kipindi kirefu humfanya mchezaji ashindwe kudumisha kiwango chake, wakati ratiba inapobana na mechi kufuatana kwa karibu huongeza uchovu kwa wachezaji.
“Changamoto ambayo nimeiona tangu naanza kucheza ni ratiba. Unakuta mnaweza kucheza mechi moja tu ndani ya mwezi mzima, hali ambayo inafanya iwe ngumu kwa mchezaji kuendelea kudumisha kiwango. Lakini pia mechi zikifuatana sana zinachosha wachezaji,” anasema Kikoti.
NAMUNGO NA USAJILI
Kikoti pia anaeleza namna anavyoiona Namungo katika suala la ujenzi wa kikosi, akitofautisha na baadhi ya timu zinazotegemea zaidi kukuza vijana wao.
Kwa mtazamo wake, Namungo imekuwa ikijikita zaidi kwenye kusajili wachezaji wenye uwezo kutoka maeneo mbalimbali ili kujenga kikosi chenye ushindani, jambo linalofanya pia ushindani wa namba kuwa mkubwa.
“Namungo siyo timu ambayo imejikita sana kwenye kuibua na kukuza vijana. Sisi tunategemea zaidi kusajili wachezaji wenye ubora kutoka nje ili kupata ushindani. Ndiyo maana hata ushindani wa namba ni mkubwa kwa sababu tumesajili wachezaji wengi wazuri,”€ anasema.
MGUNDA ANATAKA USHINDANI
Kikoti amemuelezea kocha Juma Mgunda kama mwalimu anayependa ushindani ndani ya kikosi na uwanjani, huku akifichua ushauri alioupata kutoka kwa kocha huyo kutokana na uzoefu alionao.
Anasema Mgunda amekuwa akimtaka kutumia uzoefu wake kwa kujipanga kisaikolojia na kitekniki ili kila anapopata nafasi ya kucheza awe tayari kuitumia vizuri.
“Mgunda anapenda sana ushindani. Alinishauri kama mchezaji mwenye uzoefu ni lazima nijipange vizuri kisaikolojia na kitekniki ili nikipewa nafasi niwe tayari kufanya vizuri,”€ anasema Kikoti.
UJUMBE AZAM, SINGIDA
Kwa Azam na Singida, ambazo zinawakilisha Tanzania kwenye michuano ya CAF, Kikoti anasema jambo muhimu ni kutumia vizuri michezo ya nyumbani kwa sababu mazingira ya mashindano hayo yanahitaji timu kujenga matokeo mapema.
Anaamini timu hizo zina uwezo wa kufika hatua ya makundi, huku akisema safari baada ya hapo itategemea aina ya wapinzani watakaokutana nao kwenye droo.
“Mechi za nyumbani lazima zitumike vizuri kwa sababu CAF ni ngumu na kila timu inataka kutumia uwanja wake kupata matokeo. Naamini Azam na Singida zinaweza kufika hatua ya makundi, lakini baada ya hapo itategemea watapangwa kwenye kundi gani,” anasema Kikoti.
NAMUNGO YAMKOSESHA USINGIZI
Kikoti hakufichi kuwa Namungo imekuwa ikipitia kipindi kigumu kwenye matokeo katika misimu ya karibuni, akisema hali hiyo ya kupambana ili kuepuka kushuka daraja imekuwa na athari kubwa kwa wachezaji.
Kwa mujibu wake, unapokuwa kwenye mbio za kujiokoa, presha huongezeka na inaweza kuathiri hata maisha ya mchezaji nje ya uwanja.
“Unapokuwa unapigania kujiokoa, mchezaji anakosa amani na wakati mwingine usingizi. Pia msongo wa mawazo na migogoro ndani ya timu vinaweza kujitokeza.”
KUSTAAFU
Kikoti tayari ameshaanza kufikiria maisha baada ya soka, akifichua kuwa anatarajia kucheza kwa miaka miwili hadi mitatu zaidi kabla ya kutundika daluga.
“Sijioni nikicheza kwa muda mrefu sana. Nadhani nina miaka miwili hadi mitatu zaidi kabla ya kustaafu. Soka limenisaidia kupata nyumba, shamba na familia, na pia nimekuwa nikiwasaidia wadogo zangu wanaosoma. Kwa sasa naendelea kuwekeza kwenye vitu mbalimbali ili baadaye niishi kwa utulivu,” anasema.
Kikoti pia hana mpango wa kuingia moja kwa moja kwenye ukocha baada ya kustaafu, akisema anataka kutumia muda huo kuwa karibu zaidi na familia yake baada ya miaka mingi ya kuishi kwenye kambi, safari na majukumu ya soka.
“Baada ya kustaafu sina mpango wa kuendelea na kazi za soka kama ukocha. Nataka nipumzike na kuwa na familia yangu, kwa sababu muda mwingi nimekuwa mbali nao kutokana na kambi na safari.”