Willian avunja mkataba Ugiriki
Muktasari:
- Winga huyo alisajiliwa na klabu hiyo ya Ugiriki kwa mkataba wa mwaka mmoja akitokea Fulham kwenye dirisha la majira ya kiangazi la mwaka jana.
ATHENS, UGIRIKI: STAA wa zamani wa Arsenal na Chelsea, Willian ameripotiwa kuvunja mkataba na klabu ya Olympiacos.
Winga huyo alisajiliwa na klabu hiyo ya Ugiriki kwa mkataba wa mwaka mmoja akitokea Fulham kwenye dirisha la majira ya kiangazi la mwaka jana.
Lakini, alishindwa kuonyesha kiwango bora akicheza mechi 11 kwenye kikosi cha Olympiacos, ambapo hajafunga bao lolote na ana asisti moja.
Kwa mujibu wa mwandishi wa habari, Andre Hernan winga huyo amesitisha mkataba wake. Kinachoelezwa ni kwamba Mbrazili huyo anataka kuendelea kubaki Ulaya, lakini ripoti nyingine zinadai anaweza kutimkia Marekani kukipiga kwenye MLS. Willian, 36, yupo mapumzikoni Miami, jambo linalochochea uvumi kwamba huenda ukawa mpango wa kwenda kujiunga na klabu ya Inter Miami. Wakati anaondoka Fulham, mchezaji huyo alihusishwa na mpango wa kurudi kwao Brazil, kitu ambacho kimedaiwa kinaweza kutokea pia.
Aliichezea Corinthians kwa mwaka mmoja baada ya kuondoka Arsenal kabla ya kurudi tena England kujiunga na Fulham. Lakini, anaweza kufungua milango ya kwenda kukabiliana na changamoto mpya katika ligi za MLS, Saudi Arabia na Qatar, huku mpango wake ni kuendelea kucheza soka hadi atakapofikisha umri wa miaka 40.
Alisema: “Nadhani naweza kucheza kwa miaka mitatu hadi minne zaidi, pengine hadi nitakapofikisha umri wa miaka 40. Nahamasika kwenye hilo.”