Jezi ya Salah Trabzonspor yaacha gumzo
Muktasari:
- Sababu ya namba hiyo si ya kawaida, bali ina uzito mkubwa kwa mashabiki wa Trabzonspor na wakazi wa jiji la Trabzon.
TRABZON, UTURUKI: KITENDO cha nyota wa Misri, Mohamed Salah, kuonekana akiwa amevaa jezi namba 61 mara baada ya kuwasili nchini Uturuki kwenda kujiunga na Trabzonspor, kimezua mjadala mkubwa, huku wengi wakijiuliza kwa nini ameachana na namba 11 aliyoitumia kwa mafanikio makubwa Liverpool na namba 10 anayoivaa katika timu ya taifa ya Misri.
Sababu ya namba hiyo si ya kawaida, bali ina uzito mkubwa kwa mashabiki wa Trabzonspor na wakazi wa jiji la Trabzon.
Katika kila mechi ya Trabzonspor, dakika ya 61 huwa ni muda maalumu wa sherehe ambapo mashabiki huwasha fataki na kuimba kwa nguvu kuisukuma timu yao mbele. Dakika hiyo imekuwa sehemu ya utamaduni wa klabu na hutengeneza mazingira ya kipekee yanayowapa presha wapinzani.
Mbali na hilo, namba 61 ndiyo msimbo wa simu (area code) wa jiji la Trabzon, jambo lililoifanya kuwa alama ya utambulisho wa mji na klabu hiyo maarufu kwa jina la Black Sea Storm.
Hata hivyo, bado haijathibitishwa kama Salah ataitumia rasmi jezi hiyo kwenye mechi za ligi au aliivaa wakati wa kuwasili kama ishara ya heshima kwa mashabiki na utamaduni wa Trabzonspor.
Salah anajiunga na Trabzonspor baada ya klabu hiyo kutangaza kuwa imefikia hatua za mwisho za mazungumzo na mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 34.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Uturuki, nyota huyo amekubali kusaini mkataba wa miaka miwili wenye thamani ya takribani euro milioni 17, hatua inayomaliza safari yake ya kutafuta klabu mpya baada ya kuondoka Liverpool mwishoni mwa msimu uliopita.
Kabla ya Trabzonspor kuibuka mshindi katika mbio hizo, Salah alikuwa akikaribia kujiunga na Beşiktaş, lakini mazungumzo yalivunjika kutokana na kutofautiana kuhusu masuala ya kifedha.
Mkurugenzi wa Beşiktaş, Önder Özen, alithibitisha kuwa walifanya mazungumzo kadhaa na Salah pamoja na wawakilishi wake, lakini makubaliano yakashindikana huku mchezaji huyo pia akihusishwa na klabu za Saudi Arabia na Ligi Kuu ya Marekani (MLS).
Salah anaanza ukurasa mpya wa maisha yake ya soka nchini Uturuki baada ya kuandika historia kubwa akiwa Liverpool, alikoitumikia kwa misimu tisa, akifunga mabao 257 katika mechi 442 na kusaidia klabu hiyo kutwaa mataji mbalimbali ikiwemo Ligi ya Mabingwa Ulaya na Ligi Kuu England mara mbili.