Wembanyama, Jaylen Brown wateuliwa akiba NBA All-Star 2025
Muktasari:
- Miongoni mwa wachezaji hao baadhi ni wapya kwenye kikosi cha All-Star akiwemo Victor Wembanyama, Jaylen Brown, Cade Cunningham, Evan Mobley na Alperen Sengun ambao wamepata nafasi ya kuonyesha vipaji katika mashindano hayo maarufu ya katikati ya msimu.
SAN FRANCISO, MAREKANI: JANUARI 31, 2025, wachezaji 14 walitangazwa kuwa wachezaji wa akiba kwa ajili ya mchezo wa All-Star wa NBA utakaopigwa Februari 16, 2025 kwenye Uwanja wa Chase Center huko San Francisco, Marekani.
Miongoni mwa wachezaji hao baadhi ni wapya kwenye kikosi cha All-Star akiwemo Victor Wembanyama, Jaylen Brown, Cade Cunningham, Evan Mobley na Alperen Sengun ambao wamepata nafasi ya kuonyesha vipaji katika mashindano hayo maarufu ya katikati ya msimu.
Kwa mara ya kwanza, mfumo wa mchezo wa NBA All-Star utabadilika. Mchezo wa 2025 utakuwa na mashindano ya timu nne zinazoshindana kwenye mechi tatu na kila timu itakuwa na wachezaji wanane.
Timu zitapangwa na wachambuzi wa TNT wakiwa ni Charles Barkley, Shaquille O’Neal na Kenny Smith ambao watakuwa kama mameneja wa timu katika mchakato wa kupiga kura kwa ajili ya kuunda vikosi.
Katika mchakato wa kuchagua wachezaji wa akiba, makocha wa NBA walikuwa na jukumu la kuchagua wachezaji saba kutoka kila mkondo kwa kugawa nafasi hizo kwa wachezaji wawili wa nafasi ya ulinzi (guards), watatu wa nafasi ya mbele (frontcourt) na mastaa wawili wanaocheza nafasi yoyote.
Ni muhimu kutambua kwamba makocha walizuiwa kuchagua wachezaji kutoka katika timu zao wanazofundisha.
MFUMO MPYA
Mwaka huu, mfumo wa All-Star utakuwa tofauti kidogo - kutakuwa na mashindano madogo ya timu. Mchezo utakuwa na mechi tatu, ambapo timu mbili zitacheza nusu fainali na timu zitakazoshinda kutoka kwenye nusu fainali zitakutana katika mchezo wa fainali. Katika kila mchezo, timu itakayofikia au kupita alama 40 itakuwa mshindi.
Wachezaji wa timu zitachaguliwa na wachambuzi wa TNT kupitia mchakato wa ‘draft’. Timu zitagawanywa kwa usawa na kila mchezaji atachaguliwa na mmoja kati ya Charles Barkley, Shaquille O’Neal au Kenny Smith ili kupenya katika kikosi husika.
ZAWADI USIPIME
Mchezo wa All -star 2025 pia utakuwa na zawadi kubwa za fedha ambapo timu itakayoshinda itapata Dola 1.8 milioni ilhali kila mchezaji wa timu inayoshinda atakunja mkwanja unaofikia kiasi cha Dola 125,000.
Timu itakayoshika nafasi ya pili itapata Dola 50,000 kwa kila mchezaji na timu zitakazoshika nafasi ya tatu na ya nne zitapata Dola 25,000 kila mchezaji.
Mabadiliko hayo katika mfumo wa NBA All-star yanatarajiwa kuleta burudani mpya kwa mashabiki wa mpira wa kikapu duniani, huku wachezaji wa akiba na wachezaji wa vikosi vya kwanza wakijivunia nafasi zao kwenye jukwaa hilo la kimataifa la mchezo huo unaopendwa zaidi nchini Marekani na Canada.