Mastaa Mtibwa Sugar wageuka lulu sokoni
Muktasari:
- Msimu wa 2025-2026, Mtibwa imeshuka daraja kutoka Ligi Kuu Bara hadi Ligi ya Championship baada ya kumaliza nafasi ya 15 na kukusanya pointi 27, kufuatia kushinda mechi sita, sare tisa na kupoteza 15, kati ya 30, ikiungana na KMC iliyoburuza mkia na pointi tisa.
LICHA ya Mtibwa Sugar kushuka daraja msimu wa 2025-2026, lakini wachezaji wa kikosi hicho wamegeuka lulu sokoni, baada ya kupata timu mbalimbali za Ligi Kuu Bara kutokana na viwango bora walivyoonyesha vinavyoonyesha thamani kubwa kwa sasa.
Msimu wa 2025-2026, Mtibwa imeshuka daraja kutoka Ligi Kuu Bara hadi Ligi ya Championship baada ya kumaliza nafasi ya 15 na kukusanya pointi 27, kufuatia kushinda mechi sita, sare tisa na kupoteza 15, kati ya 30, ikiungana na KMC iliyoburuza mkia na pointi tisa.
Wakati hilo likiendelea, kiungo mshambuliaji wa Mtibwa Sugar, Fredrick Magata amekamilisha usajili wake wa kujiunga na maafande wa JKT Tanzania kwa mkataba wa miaka miwili, baada ya kuonyesha kiwango bora na timu hiyo msimu wa 2025-2026.
Magata aliyeongoza kwa kuifungia Mtibwa Sugar mabao matano ya Ligi Kuu Bara msimu wa 2025-2026 na kutoa asisti mbili kwa maana ya kuhusika katika mabao saba kati ya 25 yaliyofungwa na timu hiyo, amejiunga na maafande hao wa JKT Tanzania.
Msimu wa 2024-2025, Magata alichangia mabao 30 ya Mtibwa kati ya 58, baada ya kufunga tisa na kuasisti 21 na timu hiyo ilimaliza mabingwa na pointi 71, ikiungana na Mbeya City kurejea Ligi Kuu Bara iliyomaliza nafasi ya pili na pointi 68.
Magata ni mchezaji anayeshikilia rekodi ya kupandisha timu mbili kutoka Ligi ya Championship hadi Ligi Kuu Bara, ambapo nyota huyo alianza na kikosi cha Mbeya Kwanza kwa msimu wa 2021-2022, kisha akarudia na Mtibwa Sugar msimu wa 2024-2025.
Akizungumza na Mwanaspoti, Magata amesema ni kweli kuna mazungumzo na baadhi ya klabu mbalimbali yanaendelea, ingawa ni mapema kuzungumzia timu atakayoichezea kwa msimu wa 2026-2027, kwa sababu bado hakuna makubaliano rasmi yaliyofikiwa.
Licha ya kauli hiyo, Mwanaspoti linatambua Magata amekamilisha usajili huo wa kujiunga na JKT Tanzania, akiungana na wachezaji wengine waliocheza naye Mtibwa Sugar, ambao ni kipa, Constantine Malimi na kiungo mshambuliaji, Ismail Mhesa.
Wachezaji wengine walioondoka Mtibwa na kujiunga na timu nyingine za Ligi Kuu Bara ni aliyekuwa beki wa kati na nahodha, Haroun Lyawatwa aliyetua Mashujaa FC na beki wa kulia, Datius Peter aliyetimkia Geita Gold.