Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wayne Rooney: Nilitaka kujiua Man United

Muktasari:

  • Rooney, ambaye alijiunga na Manchester United akitokea Everton mwaka 2004, alisema alipitia kipindi kigumu cha kisaikolojia licha ya kufanya vizuri uwanjani, akieleza kuwa wakati huo alikuwa akitumia pombe kupita kiasi na kujitenga na watu kwa siku kadhaa.

LONDON, England: WAYNE Rooney aliyekuwa nahodha wa timu ya taifa ya England na mshambuliaji wa zamani wa Manchester United, amefichua kuwa aliwahi kufikia hatua ya kufikiria kujiua wakati wa kipindi chake cha mafanikio makubwa akiwa na klabu hiyo kutokana na changamoto za maisha nje ya uwanja.

Rooney, ambaye alijiunga na Manchester United akitokea Everton mwaka 2004, alisema alipitia kipindi kigumu cha kisaikolojia licha ya kufanya vizuri uwanjani, akieleza kuwa wakati huo alikuwa akitumia pombe kupita kiasi na kujitenga na watu kwa siku kadhaa.

Akizungumza na mtangazaji Gabby Logan katika podikasti ya Life at the Midpoint, Rooney alieleza kuwa wakati mwingine alikuwa akijifungia nyumbani kwa siku mbili mfululizo akinywa pombe, hali iliyokuwa ikitokea katika kipindi ambacho alikuwa katika kiwango bora cha soka lake.

Nilipokuwa nikinywa pombe, nilikuwa najifungia nyumbani kwa siku mbili na kunywa tu. Hicho ndicho kipindi ambacho ningesema kilikuwa kigumu zaidi maishani mwangu, alisema Rooney alipoulizwa kuhusu wakati mgumu zaidi aliowahi kupitia. Mshambuliaji huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 41 alisema alishindwa kukabiliana na hali hiyo, lakini baada ya kuzungumza na mkewe, Coleen, pamoja na mama yake, alitambua kuwa alihitaji msaada ili kuweza kuvuka changamoto hizo.

Alisema alifikia hatua ya kuwaza kujiua na hakutaka kuwa karibu na watu, kwenda madukani au hata kukutana na watu mitaani, licha ya kuwa uwanjani alikuwa akijisikia vizuri na mwenye kujiamini.

Nilifika mahali nikawa nawaza kujiua. Sikutaka kuwa karibu na mtu yeyote. Sikutaka kuwaona watu mitaani wala kwenda madukani. Nilikuwa najisikia vizuri kila nilipokuwa kwenye uwanja wa mpira, lakini mambo mengine yote nje ya hapo yalikuwa magumu sana kwangu, alisema.

Rooney, ambaye alifunga mabao 53 katika mechi 120 alizoichezea England, alisema aliamua kutafuta msaada wa kitaalamu kwa kuzungumza na mtaalamu wa tiba ya kisaikolojia ili kuelewa kilichokuwa kikiendelea ndani yake.

Alisema hali hiyo ilikuwa ngumu zaidi kwake kwa sababu ilikuwa wakati ambao kwa nje maisha yake yalionekana kuwa katika furaha kubwa. Alikuwa amefanikiwa kisoka, amepata mtoto wake wa kwanza, Kai, ambaye sasa ana miaka 17, na alikuwa amefunga ndoa, lakini ndani yake alikuwa akipitia wakati mgumu.

Nilikuwa nikizungumza na mtaalamu wa tiba ya kisaikolojia ili nijaribu kuelewa kilichokuwa kikiendelea kwangu. Nikitazama nyuma, huenda nilikuwa katika kilele cha mafanikio yangu ya soka, nilikuwa nimepata mtoto mdogo na nilikuwa nimeoa.

Ulipaswa kuwa wakati wenye furaha zaidi maishani mwangu, lakini haikuwa hivyo. Kwa kweli, ulikuwa wakati mgumu zaidi kutokana na mambo niliyokuwa nikiyafanya, alisema.

Aliongeza kuwa alikuwa akijitahidi kuficha hali yake halisi kwa sababu hakutaka kuonekana dhaifu, akiamini kuwa kukiri kupitia changamoto hizo kungemfanya ajione kuwa amepoteza nguvu kama mwanaume.

Hata hivyo, alisema mkewe Coleen alikuwa msaada mkubwa katika kipindi hicho, akieleza kuwa pamoja na ukubwa wa changamoto walizopitia, hakumtelekeza na aliendelea kusimama naye hadi alipoweza kuvuka hali hiyo.

Coleen alinisaidia sana. Angeweza kuondoka kwa sababu hali ilikuwa mbaya kiasi hicho, lakini aliamua kubaki nami na kunisaidia kuvuka kipindi hicho,  alisema.

Katika kipindi chake cha miaka 13 Manchester United, Rooney aliweka rekodi ya kuwa mfungaji bora wa muda wote wa klabu hiyo kwa mabao 253 katika mechi 559.

Pia alisaidia timu hiyo kutwaa mataji matano ya Ligi Kuu England, Ligi ya Mabingwa Ulaya, Europa Ligi, Kombe la FA na mataji matatu ya Kombe la Ligi kabla ya kuondoka mwaka 2017 na kurejea Everton.