Romario amvamia Ancelotti, ataka afukuzwe Brazil
Muktasari:
- Romario ambaye ni miongoni mwa wafungaji bora wa muda wote wa Brazil ametoa kauli hiyo mara ya pili ndani ya wiki moja, akionyesha kutoridhishwa na mwenendo wa timu hiyo chini ya kocha huyo raia wa Italia.
LONDON, England: GWIJI wa zamani wa Brazil, Romario amemtaka kocha mkuu wa timu ya taifa ya nchi hiyo, Carlo Ancelotti ajiuzulu au afukuzwe kazi, akidai hajafanya mabadiliko yoyote yenye manufaa tangu alipopewa jukumu la kuinoa timu hiyo.
Romario ambaye ni miongoni mwa wafungaji bora wa muda wote wa Brazil ametoa kauli hiyo mara ya pili ndani ya wiki moja, akionyesha kutoridhishwa na mwenendo wa timu hiyo chini ya kocha huyo raia wa Italia.
Mzozo huo ulianza baada ya Brazil kufungwa mabao 3-2 na Japan katika mchezo wa kirafiki, Ijumaa iliyopita, kufuatia bao la ushindi la Tatsuhiro Sakamoto katika dakika za nyongeza.
Katika mchezo huo, Ancelotti alionyeshwa kadi nyekundu kwa kupinga uamuzi wa mwamuzi, huku mshambuliaji wa Barcelona, Raphinha naye akitolewa nje kwa kadi hiyo.
Baada ya kipigo hicho, Romario alitumia ukurasa wake wa Instagram kumshambulia Ancelotti, akimtaka aondoke katika nafasi hiyo.
“Ancelotti, imetosha sasa! Kusanya virago vyako uondoke! Hakuna anayepinga historia yako. Wewe ni mmoja wa makocha wakubwa kuwahi kutokea katika soka la dunia, lakini mafanikio hayo umeyapata katika ngazi ya klabu,†aliandika Romario.
Gwiji huyo pia aligusia matokeo ya Brazil katika Kombe la Dunia la 2026, ambako timu hiyo ilitolewa na Norway katika hatua ya 16 bora, ikishindwa kufika robo fainali kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1990.
Alisisitiza kuwa Brazil haiwezi kuendelea kuhatarisha nafasi yake ya kufanya vizuri katika mashindano makubwa, akisema hawapaswi kuruhusu Kombe jingine la Dunia lipotee bila mafanikio.
Hata hivyo, Ancelotti hakukubaliana na mashambulizi hayo, akisisitiza kuwa kila mtu ana haki ya kutoa maoni yake katika nchi yenye uhuru wa kujieleza.
Akizungumza kabla ya mchezo wa kirafiki dhidi ya Singapore, Jumanne, kocha huyo alisema si jukumu lake kuamua kama kauli za Romario ni sahihi au si sahihi.
“Katika nchi ya kidemokrasia yenye uhuru wa kujieleza, kila mtu anaruhusiwa kutoa maoni yake. Si jukumu langu kusema kama anachokisema ni sahihi, si sahihi au ni upuuzi tu. Ukweli ni kwamba Romario anazungumza sana. Sana. Hiyo ni haki yake,†alisema Ancelotti.
Pamoja na kukosolewa, Ancelotti alionyesha kuridhishwa na mwelekeo wa kikosi chake, akisisitiza kuwa bado ni mradi mpya unaohitaji muda wa kuimarika.
Kocha huyo ana rekodi kubwa katika soka la klabu, akiwa ameshinda mataji matano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa kocha mkuu, huku pia akitwaa ubingwa wa ligi katika nchi zote tano kubwa za soka barani Ulaya.
Hata hivyo, rekodi yake akiwa na Brazil haijawa ya kuridhisha kwa kiwango kinachotarajiwa, kwani katika mechi 21 alizoiongoza timu hiyo, imeshinda 12, kutoka sare nne na kupoteza tano.
Lakini majibu ya Ancelotti hayakumzuia Romario kuendeleza mashambulizi yake, kwani kabla ya Brazil kucheza mchezo mwingine wa kirafiki dhidi ya Singapore, gwiji huyo alirudia msimamo wake wa kutaka kocha huyo aondoke.
Romario, ambaye alifunga mabao 784 katika historia ya soka lake, alisema ana mamlaka ya kuzungumzia masuala ya timu ya taifa kutokana na mchango wake akiwa mchezaji wa Brazil.
“Ninazungumza sana kwa sababu linapokuja suala la timu ya taifa, nina hadhi, uzito na nguvu ya kutoa maoni. Sizungumzi ili kupata wafuasi wala kutafuta kupendwa na watu. Ninasema kile ninachoamini.
“Nimevaa jezi hii kwa miaka mingi na nina uhakika nilikuwa miongoni mwa watu waliochangia kuifanya jezi hiyo ya njano ndogo iheshimiwe duniani kote,†alisema Romario.
Alisema anamheshimu Ancelotti, lakini akasisitiza kuwa kocha huyo hajaongeza kitu kipya katika timu ya taifa tangu alipopewa jukumu hilo.
“Nitasema tena, jiuzulu! Tutapata kocha mwingine atakayefanya kazi vizuri zaidi yako. Nakwambia haya moja kwa moja usoni, si kupitia ujumbe, ikiwemo kwa rais wa Shirikisho la Soka la Brazil ambaye alipaswa kuwa ameshakufukuza kazi muda mrefu uliopita,†alisema Romario.
Hata hivyo, katika mchezo wake wa mwisho wa mwaka 2026 dhidi ya Singapore, Brazil ilijibu mapigo kwa ushindi mkubwa wa mabao 7-0, huku mshambuliaji wa Real Madrid, Vinicius Junior, akifunga mabao matatu ndani ya dakika 21 za mwanzo.
Mshambuliaji wa Bournemouth, Rayan, na nyota wa Chelsea, Estevao, pia walifunga katika mchezo huo.
Ushindi huo unaweza kupunguza kwa muda mvutano kati ya Romario na Ancelotti, lakini kutokana na msimamo wa gwiji huyo wa Brazil, bado haijulikani kama vita yao ya maneno itafikia mwisho.