Timu sita zakata tiketi AFCON 2027, Afrika Mashariki
Muktasari:
- Timu hizo zimefanikiwa kukata tiketi ya kucheza AFCON 2027, mashindano ambayo yanaandaliwa kwa ushirikiano wa Tanzania, Kenya na Uganda, huku kila moja ikibakia na mechi mbili mkononi katika kundi lake.
DAKAR, SENEGAL: RAUNDI nne za hatua ya makundi ya kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 zimefikia tamati kwa kuacha tabasamu kwa timu sita za taifa ambazo zimefanikiwa kuwa na tiketi ya kuja Afrika Mashariki.
Timu hizo zimefanikiwa kukata tiketi ya kucheza AFCON 2027, mashindano ambayo yanaandaliwa kwa ushirikiano wa Tanzania, Kenya na Uganda, huku kila moja ikibakia na mechi mbili mkononi katika kundi lake.
Zinaungana na wenyeji wenza, Tanzania, Kenya na Uganda ambazo zilishafuzu, kufanya kuwe na jumla ya timu tisa ambazo tayari zina uhakika wa kuwepo kwenye fainali hizo zitakazofanyika kuanzia Juni 19 hadi Julai 17, 2027. Senegal ilikuwa timu ya kwanza kufuzu kupitia kundi J baada ya kubebwa na ushindi wa bao 1-0 ambao Msumbiji iliupata dhidi ya Ethiopia ugenini.
Senegal sasa imefikisha pointi 10, huku Msumbiji ikiwa na saba ikiwa inapewa nafasi ya pili ya kufuzu kupitia kwenye kundi hilo, kutokana na Sudan kuwa na pointi mbili.
Katika Kundi A, ushindi wa bao 1-0 ambao Morocco iliupata dhidi ya Niger, umeifanya ifikishe pointi 12 na kufuzu kwa fainali hizo ikiwa inapewa nafasi kubwa ya kufanya tena vizuri kwenye michuano hiyo mwakani baada ya fainali zilizopita kuandaa na kufika fainali ambapo ilipoteza dhidi ya Senegal lakini ikakata rufaa.
Timu ya pili ambayo inaweza kuungana nao kwenye michezo miwili iliyobaki ni Gabon ambayo ina pointi sita hivyo itatakiwa kuchanga vyema karata zake kwenye michezo miwili iliyobaki ambayo itapigwa mwakani.
Burkina Faso iliyopata ushindi wa mabao 3-1 ugenini dhidi ya Mauritania, imeungana na Benin kufuzu kupitia kundi F ambapo kila moja ina pointi 10 ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine yoyote kwenye kundi hilo.
Hili ndiyo kundi pekee ambalo hadi sasa limeshamaliza kazi yake hivyo michezo zitakayocheza mwakani itakuwa ni aidha ya kutafuta nani atakuwa kinara wa kundi au kumaliza vizuri kwenye hatua hiyo na kujiweka kwenye nafasi bora zaidi kwenye viwango vya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
Ushindi wa mabao 3-0, ambao Cameroon iliupata ugenini dhidi ya Namibia umeifanya iongoze kundi G na kufuzu AFCON 2027, Cameroon ni moja kati ya mataifa yenye mafanikio makubwa zaidi kwenye fainali za AFCON na kufuzu kwao ni mwanzo mzuri wa kuongeza hamasa kwenye michuano ya mwakani. Timu nyingine ambayo inaweza kupata tiketi kupitia kwenye kundi hili ni Comoro ambayo ina pointi saba na kama itachanga karata zake vizuri basi itafuzu kwa fainali hizo za mwakani.
Kundi C, Ivory Coast wanaonekana kuwa kwenye nafasi nzuri ya kufuzu wakiwa na pointi 10 ambapo wanafuatiwa na Gambia wenye pointi saba huku Ghana wakiwa wanafuata wakiwa na pointi sita baada ya kuanza vibaya kwenye michezo ya mwanzoni sasa wanaonekana kuanza kupata makali baada ya kufanya vizuri kwenye michezo miwili ya mwisho.
Mali anayochezea kipa wa Yanga, Djigui Diarra nayo imefanikiwa kufuzu AFCON 2027 kupitia kundi K. Ushindi wa mabao 2-0 ugenini jijini Kigali dhidi ya wenyeji Rwanda, umeifanya Mali kufikisha pointi 12 na hivyo kuwa na uhakika wa kushiriki fainali za AFCON mwakani, hii ina maana kuwa kwa mashabiki wa Afrika Mashariki watakuwa na nafasi ya kumuona Diarra akiwa anaitumikia timu yake ya Taifa.
Rwanda bado ina nafasi ya kufuzu kwa fainali hizo ikiwa sasa ina pointi sita na inatakiwa kuhakikisha inashinda mchezo mmoja na kutoka sare mmoja kati ya miwili iliyobaki ili iweze kupata tiketi hiyo muhimu kwao.