Watano kortini kuingiza gari la maiti uwanjani
Muktasari:
- Watu hao wamefikisha kizimbani baada ya tukio hilo lililofanyika mbele ya mashabiki katika mchezo wa maandalizi wa ligi ya daraja la chini mjini Northumbria, England.
NORTHUMBIA, ENGLAND; WANAUME watano wameshtakiwa baada ya gari la kubebea maiti pamoja na gari jingine kuingizwa kwenye uwanja wa mpira wa miguu na kufanya mizunguko kadhaa hali iliyosababisha mchezo uliokuwa ukiendelea kusitishwa.
Watu hao wamefikisha kizimbani baada ya tukio hilo lililofanyika mbele ya mashabiki katika mchezo wa maandalizi wa ligi ya daraja la chini mjini Northumbria, England. Tukio hilo lilitokea mwaka 2023 wakati wa mchezo wa msimu kati ya Dunston UTS na Gateshead na kusambaa kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii baada ya video za gari hilo la mazishi kuingia uwanjani.
Baada ya mizunguko kuzunguka uwanja, mashabiki walishuhudia magari hayo mawili yakivunja kizuizi na kusimama katikati ya uwanja. Wanaume waliokuwa wamejifunika nyuso zao walitoka kwenye gari la kubebea maiti ambalo lilikuwa na mabango kadhaa kwenye madirisha, na kuingia kwenye gari jingine huku wakirusha vipeperushi uwanjani, kabla ya kutokomea kwa kasi kwa kutumia gari aina ya Subaru.
Hati ya mashtaka inaeleza kwamba watu wanne kati ya watano wanadaiwa kulazimisha kufunguliwa kwa mageti ya uwanja kabla ya magari hayo kuingia uwanjani, hivyo kuhatarisha maisha ya wachezaji wa timu mbili pamoja na mashabiki waliokuwapo. Mchezo huo ulisitishwa muda mfupi baada ya mapumziko ya kipindi cha kwanza timu zikiwa zimefungana bao 1-1.
Polisi wa Northumbria walidai katika taarifa kwamba wanaume watano wamefunguliwa mashtaka mbalimbali na wote walitarajiwa kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu ya Sunderland na South Tyneside jana, Jumatano au kesho Ijumaa.
Inspekta Mkuu wa Upelelezi David Johnson wa Polisi wa Northumbria alisema: “Tumekuwa tukifanyia kazi uchunguzi mrefu na tata tangu tulipofahamu kuhusu tukio hili ambalo tumekuwa tukilichukulia kuwa lina uhusiano wa kihalifu. Timu zetu zimefanya kazi bila kuchoka pamoja na wenzetu hadi kufikia hatua hii ya kufungua mashtaka.”