Townsend:Supu ya miguu ya kuku dawa
Muktasari:
- Winga huyo wa zamani wa Tottenham na England, ambaye sasa anakipiga PT Prachuap ya Thailand, alikumbwa na tukio hilo la kushangaza wakati mashine hiyo ilipomgonga alipokuwa akifanya mazoezi ya kujiandaa na kipindi cha pili.
LONDON, England; SUPU ya miguu ya kuku aliyokula nyota Andros Townsend imekuwa gumzo baada ya mwenyewe kudai kuwa ni aina ya vyakula vya kipekee alivyokula baada ya kupata ajali ya kutisha ya kugongwa na mashine ya kusawazisha uwanja wa mpira wakati wa kujiandaa kuingia kipindi cha pili.
Winga huyo wa zamani wa Tottenham na England, ambaye sasa anakipiga PT Prachuap ya Thailand, alikumbwa na tukio hilo la kushangaza wakati mashine hiyo ilipomgonga alipokuwa akifanya mazoezi ya kujiandaa na kipindi cha pili.
Townsend, 35, alinusurika bila majeraha makubwa na cha kushangaza zaidi, aliweza kuingia uwanjani kama mchezaji wa akiba katika kipindi cha pili.
Hata hivyo, baada ya mchezo huo, goti lake lilianza kuvimba na ndipo alipoamua kuandaa mlo maalumu alioueleza kuwa sehemu ya kusaidia mwili wake katika kipindi cha kupona.
Katika video aliyoweka Instagram, Townsend alisema ndani ya saa 24 baada ya tukio hilo alikula vyakula mbalimbali alivyodai vililenga kuupa mwili virutubisho alivyohitaji.
Katika mlo wake alitumia salmoni pamoja na nyanya, kabla ya kutaja chakula ambacho huenda wengi wasikitarajie.
“Moja ya supu ninavyovipenda katika hali kama hii ni ya miguu ya kuku iliyopikwa taratibu kwa saa nane kwenye supu,” alisema.
Alieleza kuwa chakula hicho kilimpa collagen na gelatin pamoja na amino acid kama glycine na proline, ambazo alisema zinahusishwa na tishu zenye collagen kama kano, mishipa na gegedu.
“Pia, nilikuwa mayai sita. Yana protini yenye ubora inayosaidia ukarabati wa misuli,” alisema.
Townsend kisha akataja vyakula vyenye polyphenols, ikiwamo blueberries, mafuta ya zeituni na kakao mbichi, akieleza kuwa vina virutubisho vinavyohusishwa na kupunguza madhara ya uchochezi mwilini.
Baadaye alikula samaki aina ya salmoni aliyekaushwa kwa moshi, akisema ana omega-3 inayohusishwa na mchakato wa uchochezi na kusaidia mwili katika kurejesha misuli.
“Jibini mbichi linanipa calcium kwa ajili ya afya ya mifupa, huku chungwa likinipa vitamin C ambayo ni muhimu katika utengenezaji wa collagen,” alisema.
Townsend pia aliongeza kiwi, akisema kilimsaidia kupata kiasi kingine cha vitamin C.
Alipohitimisha video yake, nyota huyo wa England alisema kwa msisitizo: “Chakula ni dawa.”
Ajali hiyo ya Townsend ilisambaa kwa kasi mitandaoni baada ya picha za tukio hilo kuonekana, huku baadaye mchezaji huyo akialikwa kwenye kipindi cha Piers Morgan Uncensored kueleza kilichotokea.