Wakala wa Rodrygo atua England
Muktasari:
- Kwa mujibu wa mwandishi wa habari kutoka Hispania, Jorge Nicola, Rodrygo yupo karibu sana kuondoka Madrid majira haya ya kiangazi na wakala wake pia ameshatua England kwa ajili ya kuzungumza na timu zinazomhitaji ili kufikia mwafaka.
LONDON, ENGLAND: WINGA wa Real Madrid, Rodrygo, ambaye kwa sasa hana nafasi kikosini, anaonekana yupo mbioni kuondoka Santiago Bernabeu na kutua Ligi Kuu England ambako timu kama Manchester City na Liverpool zinahitaji huduma yake.
Kwa mujibu wa mwandishi wa habari kutoka Hispania, Jorge Nicola, Rodrygo yupo karibu sana kuondoka Madrid majira haya ya kiangazi na wakala wake pia ameshatua England kwa ajili ya kuzungumza na timu zinazomhitaji ili kufikia mwafaka.
Mwandishi pia alieleza Kocha wa Man City, Pep Guardiola anamtaka mchezaji huyo wa kimataifa wa Brazil, lakini usajili wake utategemea iwapo Savinho atajiunga na Tottenham.
Liverpool pia o imeingia rasmi kwenye mbio za kumsajili Rodrygo, wakimtazama kama mrithi wa moja kwa moja wa Luis Diaz, ambaye alitimkia Bayern Munich mapema katika majira haya ya kiangazi.
Rodrygo amekuwa katika sintofahamu tangu Xabi Alonso alipokabidhiwa majukumu ya ukocha na hata katika mechi ya ufunguzi wa La Liga dhidi ya Osasuna Jumanne ya wiki hii, Rodrygo aliishia benchi.
Baada ya kumuacha Rodrygo benchi dhidi ya Osasuna, Alonso alieleza uamuzi wake kwa wanahabari akisema: “Rodrygo? Hakuna kinachoendelea. Namtegemea Rodrygo. Ilikuwa ni mechi tu, na huu ulikuwa uamuzi wangu.”
Rodrygo bado ana mkataba na Real Madrid hadi mwaka 2028 na klabu hiyo tayari ilishawahi kusisitiza haina haraka ya kumuuza isipokuwa kama klabu inayomtaka italeta dau la takribani Euro 100 milioni.