Vivienne Lia: Mtanzania aliyeiumiza Tanzania Kombe la Dunia
Muktasari:
- Lia mwenye asili ya Tanzania anayecheza kama winga alionyesha kwa nini aliaminiwa kuanza katika kikosi cha England akitumia kasi na uwezo wa kupiga mipira ndani ya boksi la Tanzania.
Vivienne Lia juzi aligeuka kuwa mwiba kwa Tanzania akihusika moja kwa moja katika mabao mawili ya England iliyoichapa Tanzanite Queens 5-1 kwenye mchezo wa pili wa kundi B la Kombe la Dunia la Wanawake U-20 nchini Poland.
Lia mwenye asili ya Tanzania anayecheza kama winga alionyesha kwa nini aliaminiwa kuanza katika kikosi cha England akitumia kasi na uwezo wa kupiga mipira ndani ya boksi la Tanzania.
Dakika ya tisa, Lia alitengeneza bao la kwanza baada ya kupiga krosi nzuri iliyomkuta Princess Ademiluyi nyuma ya mabeki wa Tanzania, ambaye hakufanya makosa na kuukwamisha mpira wavuni.Lia aliendelea kuwa tishio upande wa kulia na dakika ya 47 krosi yake ilimkuta tena Ademiluyi, ambaye mpira wake uligonga mwamba. Dakika 55 baadaye, Lia alimtengenezea Vera Jones nafasi, lakini shuti lake lilipita pembeni.
Dakika ya 74, akapiga krosi nyingine iliyomkuta Jessie Gale, aliyefunga bao la tano la England na kumpa Lia asisti yake ya pili kwenye mchezo huo.
Lia alianza mchezo akiwa namba nane na alicheza hadi dakika ya 80 kabla ya nafasi yake kuchukuliwa na Layla Drury. England ilikuwa na asilimia 68 ya umiliki wa mpira, ilipiga mashuti 14, yaliyolenga lango mara 10, huku Tanzania ikiwa na asilimia 32 ya umiliki na mashuti sita, manne yakilenga lango.
Winga huyo wa anayekipiga Eintracht Frankfurt ya Ligi Kuu ya Wanawake Ujerumani huo ulikuwa mchezo wake wa kwanza katika Kombe hilo baada ya kuitwa kwenye kikosi cha England.